
Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) ameeleza kuwa mchakato wa amani umepiga hatuua kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosainiwa mwezi Aprili hata hivyo ametahadharisha kuwa kupunguzwa kwa bajeti ijayo kunaweza kudhoofisha mchakato huo.
Valentine Rugwabiza Mkwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema mchakato wa amani wa nchi hiyo umepiga hatua na mafanikio makubwa yameshuhudiwa tangu kutiwa saini makubaliano ya kusitisha mapigano Aprili 19 mwaka huu chini ya usuluhishi wa Chad.
Amesema makubaliano hayo yalitiwa saini na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na makundi mawili makuu yanayobeba silaha nchini humo.
Rugwabiza ambaye pia ni Mkuu wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa (MINUSCA) ameeleza kuwa utekelezaji wa makubaliano ya Aprili na upokonyaji silaha ni mafanikio katika uga wa usalama yanayoshuhudiwa kivitendo katika maeneo kadhaa katikati na kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) ametaja chaguzi za rais, ubunge, mkoa na manispaa za Disemba 28 kama “kigezo cha kupanua na kuunganisha mamlaka za serikali na kuimarisha utulivu wa kitaasisi.”
Bi Valentine ametilia mkazo uungaji mkono wa kimataifa, na kusisitiza kuwa kikosi cha kulinda amani cha MINUSCA “kinaendelea kuwa kiungo muhimu katika kuimarisha hatua za kiusalama na amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati.”