Ujenzi wa taifa bora ni mchakato endelevu. Mwafaka wa nchi kikatiba ni kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano. Iliamuliwa na waasisi wa taifa la Tanzania kama mtindo wake wa kisiasa ni wa kidemokrasia.

Leo ni Uchaguzi Mkuu 2025. Watanzania mikoa yote, wilaya zote, jimbo kwa jimbo, kata hadi kata, wanapiga kura kuchagua viongozi wao wa muhula ujao wa miaka motano. Kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Wananchi wanachagua wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, halafu madiwani kata zote. Kufanyika kwa uchaguzi ni uthibitisho kuwa ndoto za waasisi wa taifa hili bado zipo hai. Walitaka mamlaka ya nchi yawe kwenye mikono ya wananchi, ndivyo maono yanavyoendelea kuishi.

Uchaguzi wa viongozi ndiyo kudhihirika kwa mamlaka ya wananchi. Hapatikani Rais mpaka wananchi waamue kwa kupiga kura. Vivyo hivyo kwa wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani. Serikali, mihimili ya uwakilishi na mamlaka za miji, havipatikani mpaka wananchi wachague.

Ilikuwa ndoto ya waasisi wa taifa la Tanzania tangu uhuru. Japo zilikuwa zama za chama kimoja, bado utaratibu wa uchaguzi ulikuwapo. Wagombea urais, ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwanini, waliwafuata wananchi na kuomba ridhaa ya uongozi wa miaka mitano.

Leo ni uchaguzi wa 13 tangu uhuru wa Tanganyika na Zanzibar. Hesabu ni hiyohiyo tokea kuzaliwa kwa dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hesabu inaanzia Uchaguzi Mkuu 1965, ambao ulikuwa wa kwanza tangu uhuru wa Tanganyika, Jamhuri ya Tanganyika kabla ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Upande wa Zanzibar, wanakwenda kufanya Uchaguzi Mkuu wa 10 tangu Mapinduzi. Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 1964, visiwa hivyo vilifanya uchaguzi kwa mara ya kwanza mwaka 1980. Huo ulikuwa mwaka wa 16 tangu Mapinduzi yalipofanyika.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uchaguzi Mkuu 2025, ni wa saba tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa Julai Mosi, 1992. Uchaguzi Mkuu 1995, ulikuwa wa kwanza kushirikisha vyama vingi vya siasa.

Uchaguzi Mkuu 2025 unaandika historia ya kipekee. Unaweka rekodi kwamba sasa Watanzania wameweza kufanya uchaguzi mara nyingi chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, kuliko wakati wa chama kimoja.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya mfumo wa chama kimoja, ilifanya uchaguzi mkuu mara sita, 1965, 1970, 1975, 1980, 1985 na 1990. Tangu vyama vingi virejeshwe, huu ni uchaguzi wa saba, 1995, 2000, 2005, 2010, 2015, 2020 na sasa 2025. Uchaguzi Mkuu 2025, haupaswi kubeba tafsiri ya pekee kwamba Tanzania ya vyama vingi inaipiku umri Tanzania ya chama kimoja, bali mantiki ielekee kwenye ukweli kwamba safari ya kujenga dola bora inaendelea.

Ndoto za uhuru, kujiongoza wenyewe na kutetea utu wetu Watanzania ina umri wa karne kwa karne. Tangu kuwakataa Waarabu na Wareno, vilevile chozi la kuukataa utumwa. Ushujaa wa Chifu Mkwawa na Lipuli yake, hadi ujasiri wa Kinjekitile na Majimaji.

Safari ya kuipata Tanzania ina umri mrefu na inapaswa kuendelea. Hata mfumo wa vyama vingi, vinara walioviasisi kwa sehemu kubwa Mungu ameshawachukua. Wamebaki wachache, ambao hawapo mstari wa mbele tena.

Ni elimu kuwa Tanzania inajengwa kwa kupokezana. Zama baada ya zama. Machampioni wanakuja, wanatoa huduma yao, kisha wanaondoka. Taifa linaendelea. Wajibu mkubwa ni kuilinda nchi. Na kuikabidhi kwa kizazi kipya ikiwa salama.

Vipindi vya uchaguzi, kihistoria, tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi, vimekuwa na tabia ya kuibua malumbano na misuguano. Kila upande ukijinasibu kushinda uchaguzi. Wengine hulalamikia kuibiwa kura. Wapo hunung’unikia uwanja wa ushindani wa kisiasa kukosa usawa.

Muhimu, kila baada ya uchaguzi inatakiwa kuketi na kuzungumza, kujadiliana, kusahihishana na kuafikiana. Lengo ni kuifanya Tanzania kuwa bora kila uchaguzi unapofanyika na kuandaa mazingira mazuri na salama kwa ajili ya uchaguzi ambao utafuata. Ujenzi wa nchi bora kwa wote ni mchakato endelevu.

Linapokuja suala la uchaguzi, mivutano na migogoro, busara pekee ambazo hunijia kichwani ni maneno ya hekima kutoka kwa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, aliyesema: “Kamwe, haitatokea tena Mkenya kufa kwa ajili ya uchaguzi.”

Ni maneno ya Raila baada ua machafuko ya kisiasa Kenya mwaka 2008. Vurugu baada ya matokeo ya uchaguzi wa rais, Desemba 2007, zilisababisha mauji ya Wakenya. Raila lilimuuma hilo, na akaapa kuwa hakuna Mkenya mwingine atakufa kwa sababu ya uchaguzi.

Hata sasa, Tanzania, wanasiasa wanatakiwa kula kiapo kuwa pamoja na kutofautiana na kuvutana, isitokee Mtanzania kufa kwa sababu ya uchaguzi. Wanaochochea machafuko waepukwe na wasipate ufuasi. Tanzania ya kesho ina neema sana, ikiwa misuaguano itamalizwa kwa mazungumzo ya amani.

Uchaguzi unakutanisha Watanzania ambao wanaipenda nchi yao na wanajali sana kesho ya taifa lao. Siyo Watanzania dhidi ya wageni au wasaliti. Au Watanzania kwa wakoloni. Ni Watanzania kwa Watanzania. Hivyo, tofauti zimalizwe Kitanzania.

Leo ni Uchaguzi Mkuu baada ya safari ya siku 61, kunguka nchi kuomba kura. Ni wiki nne na siku tano za makutano ya ana kwa ana, baina ya wagombea na wapigakura Watanzania wote. Ni miezi miwili kamili ya mawasiliano kuhusu kesho ya nchi, majimbo na kata.

Yamekuwa majuma ya wagombea kuwafikia Watanzania popote walipo, kuwaomba ridhaa ya kuendelea kuwaongoza au kupata nafasi mpya, muhimu zaidi kuwajengea matumaini mapya kutokana na ahadi ambazo kila mgombea aliziwasilisha kama mtaji wake kwa wapigakura

Nchi yetu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina ukubwa wa kilometa za mraba 947,403. Zimekuwa siku 61 za kufikia masafa yote. Leo sasa ni siku ya wananchi kufanya uamuzi wao. Ni leo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *