Ajenti wa Shirikisho la Marekani alijaribu kumsajili rubani binafsi wa Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, Jenerali Bitner Villegas, katika mpango wa siri, ili kuipeleka ndege ya rais huyo huko Marekani. Hayo yamefichuliwa na shirika la habari la Associated Press.

Ripoti hiyo imesema, mpango huo, ulioongozwa na wakala wa Upelelezi wa Usalama wa Nchi, Edwin Lopez, ulimuahidi rubani huyo utajiri mkubwa na ulinzi mkakbala wa kuielekeza ndege ya Maduro kwa siri hadi mahali ambapo vikosi vya jeshi la Marekani vingeweza kumkamata.

Licha ya mawasiliano ya siri ya awali na miezi kadhaa ya jitihada hizo, Villegas hakukubali mpango huo.

Operesheni hiyo, ambayo iliendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja, ilifanana na njama za ujasusi za enzi ya Vita Baridi, na iliambatana na mikutano ya siri kwenye viwanja vya ndege, rekodi zilizofichwa na jumbe za Whatsapp zilizosimbwa.

Pia imeangazia hatua ambayo Washington imechukua ili kumng’oa madarakani Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, ambaye maafisa wa Marekani wanamshutumu kuwa anawahifadhi wafanyabiashara wa dawa za kulevya, madai ambayo yamepingwa vikali na Caracas.

Chini ya mbinu mpya ya misimamo mikali ya Rais Donald Trump, Marekani pia imeimarisha operesheni za kijeshi na kijasusi dhidi ya Venezuela, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya meli zinazodaiwa kubeba dawa za kulevya katika eneo la Caribbean ambayo yameua makumi ya watu.

Utawala wa Trump pia umeidhinisha operesheni za siri za CIA ndani ya Venezuela na kuzidisha kitita cha fedha kwa mtu atakayepelekea kukamatwa kwa Maduro hadi dola milioni 50. Nicolas Maduro anatambuliwa kuwa miongoni mwa wapinzani wakali wa sera za kibeberu za Marekani na washirika wake, na amekuwa mkosoaji na mpinzani mkubwa wa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel, ikisaidiwa na nchi za Magharibi dhidi ya watu wa Palestina. 

Maduro katika mkutano wa Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina, Caracas

Maduro anasema utawala wa Trump “unabuni” vita dhidi ya taifa hilo la Amerika Kusini ili kuiangusha serikali yake na kuchukua udhibiti wa akiba yake kubwa ya nishati.

Kiongozi huyo wa Venezuela amenusurika majaribio mengi ya mauaji yanayofadhiliwa na Marekani na njama zingine za Washington na vibaraka wake wa eneo hilo za kutaka kumuua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *