
Katika hafla ya kuwaenzi mashahidi wa Iran huko Khorasan Kaskazini, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad-Baqer Qalibaf, ametamka kwa msisitizo kwamba, “Iran kamwe haitasalimu amri.”
Qalibaf amesema kuwa utawala wa Israel unalenga kuyasukuma mataifa mahsusi ya Asia Magharibi katika njia mbili, ima vita vinavyolazimishwa, au amani ya hadaa. Lakini, amesisitiza kuwa, pamoja na kuwepo malengo hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitayumba wala kujisalimisha.
Katika hotuba hiyo, Spika huyo ameashiria historia ya miongo kadhaa ya mashambulizi ya kichokozi ya Israel dhidi ya mataifa ya eneo, pamoja na mikataba ya amani ambayo kwa hakika ni mbinu za kufanikisha malengo ya kijeshi yaliyoshindikana.
Qalibaf ameutaja utawala wa Israel kuwa “utawala unaojitanua na kuua watoto”, akiongeza kuwa mashambulizi ya kila siku yanayotekelezwa na Israel yanalenga kunyakua maeneo mapya kwa nguvu.
Amesisitiza: “Iran haitasalimu amri wala haitakubali kuwa mateka.” Akitolea mfano wa uimara wa taifa la Iran, amekumbusha jinsi Iran ilivyokwamisha uvamizi wa pamoja wa Israel na Marekani mwezi Juni, hatua aliyosema imeweka rekodi ya kihistoria.
Katika kujibu mashambulizi hayo, Jeshi la Iran lilitumia mikakati ya ulinzi ya hali ya juu, na baadaye likatekeleza kisasi kilichofanikiwa licha ya mashambulizi ya angani yaliyoendelea.
Qalibaf amesema kuwa katika takriban miaka 80 tangu utawala haramu wa Israel utangaze kuwepo kwake, hakuna taifa lililowahi kuukabili kwa nguvu kama Iran ilivyofanya katika vita vya siku 12. Aidha Qalibaf amedokeza kuwa, siku tano tu baada ya Iran kuanza kulipiza kisasi, maombi ya kusitisha mapigano yalikuwa yakimiminika kutoka kila pembe ya dunia.
Spika huyo pia amelaani mchango wa Marekani katika mashambulizi hayo, akisema kuwa hatua hiyo ilikwenda kinyume na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yaliyokuwa yakiendelea kati ya Tehran na Washington. Amesema: “Wakati Marekani ikizungumza kuhusu amani, ndege zake za kijeshi zilikuwa zikijiandaa kushambulia mitambo ya nyuklia ya Iran.”
Kwa kumalizia, Qalibaf amesisitiza kuwa Iran imesalia kwenye njia ya mashahidi waliotoa maisha yao tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979—kwa ajili ya usalama, heshima, na ustawi wa taifa.