Baada ya mwakilishi wa Israel katika Umoja wa Mataifa kumwita Francesca Albanese, ripota maalumu wa umoja huo katika masuala ya Palestina kuwa ni mchawi, Albanese ametoa majibu makali yaliyomziba mdomo Mzayuni huyo na kumfedhehesha mbele ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Shirika la Habari la Fars limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Francesca Albanese, amekosoa jinsi jamii ya kimataifa inavyoshindwa kutekeleza majukumu yake na kuruhusu kuendelea jinai za Israel huko Palestina. Baada ya Albanese kuwasilisha ripoti yake hiyo kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa juzi Jumanne; Danny Danon mwakilishi wa utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Mataifa aliamua kumchafulia jina Albanese kwa kumwita mchawi.
Danon alisema, wewe Albanese ni “mchawi” na ripoti yako hii ni muendelezo wa vitendo vyako vya kichawi. Alijigamba kwa kusema: “Kila ukurasa wa ripoti yako hii hauna msingi na mashtaka yako hayana athari, kwa sababu umeshindwa hata katika uchawi wako huu.”

Sasa jana Jumatano gazeti la Al-Quds Al-Arabi lilichapisha majibu ya ripota huyo wa maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya Palestina yanayosema: “Ni ajabu na wakati huo huo inasikitisha kuona kwamba kundi linalolaumiwa kwa mauaji ya kimbari, badala ya kujibu ripoti yangu, linakimbilia kwenye kunituhumu mimi kwa uchawi. Kama ningekuwa na uwezo wa kutumia uchawi, nisingeutumia kulipiza kisasi, bali ningeliutumia kukomesha jinai za kundi hilo.”
Video ya majibu hayo makali ya Albanese imeenea sana kwenye mitandao ya kijamii na imepokewa kwa hisia tofauti miongoni mwa watumiaji na vyombo vya habari duniani na kumfumba mdomo vibaya mwakilishi wa Israel katika Umoja wa Mataifa.