Iran imesema kuwa Rafael Grossi Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) anajia “kikamilifu” namana miradi ya nishati ya nyuklia ya nchi hii ilivyo ya malengo ya amani na ya kiraia; kwa hiyo anapasa kujiepusha kutoa “matamshi yasiyo na msingi” kuhudu miradi hiyo.

Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya al Jazira, Esmaeil Baqaei Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa matamshi ya awali ya Grossi yalifungua njia kwa vitendo vya kichokozi vya Marekani na utawala wa Israel dhidi ya Iran mwezi Juni mwaka huu.

Ameongeza kuwa Mkurugenzi Mkuu wa wakala wa IAEA anapasa kujiepusha na utoaji maoni yasiyo na msingi kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran.

Grossi jana Jumatano alidai kuwa wakala huo hivi karibuni umegundua harakati mpya  katika vituo vya nyuklia vya Iran baada ya kukiri kuwa Iran haionekani kuwa inarutubisha urani.

Ameongeza kuwa, licha ya kushindwa kufikia kikamilifu vituo vya nyuklia vya Iran, wakaguzi wa IAEA hawajashuhudia shughuli yoyote ya kutiliwa shaka kupitia satelaiti akiashiria kuwa Jamhuri ya Kiislamu imeharakisha uzalishaji wake wa urani iliyorutubishwa zaidi ya iliyokuwa imekusanya kabla ya vita vya siku 12 kati yake na Israel mwezi Juni mwaka huu.

Inafaa kaushiria hapa kuwa, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA alidai katika ripoti ya siri aliyoituma kwa Bodi ya Magavana wa wakala huo Mei 31 mwaka huu kwamba Iran imeshindwa kutoa taarifa kuhusu shughuli zake za nyuklia katika maeneo matatu ambayo hayajatangazwa na hivyo kuibua wasiwasi kuhusu akiba yake ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha hadi asilimia 60.

Shirika la Nishati ya Nyuklia la Iran pia lilijibu madai hayo ya Mkuu wa IAEA kwa kusema hatua ya wakala huo ya kujumuisha baadhi ya masuala yasiyo na umuhimu katika ripoti yake ni kiyume na taaluma, malengo na msingi wa wakala huo. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *