
Kufuatia mkutano wa kuunga mkono amani katika eneo la Maziwa Makuu uliofanyika siku ya Alhamisi hii, Oktoba 30, jijini Paris, rais wa Ufaransa ametangaza msaada wa kimataifa wa zaidi ya Euro Bilioni 1.5 na kufunguliwa kwa njia salama kwa minajili ya kupeleka misaada kwa raia walionaswa na vita nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi jirani.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Nina furaha kutangaza kwamba kwa pamoja mmekusanya zaidi ya euro Bilioni 1.5 kama msaada kwa watu walio katika mazingira magumu zaidi,” ametangaza Emmanuel Macron mwishoni mwa mkutano huo, akitaja haswa utoaji wa dawa na chakula. Mpango wa majibu ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, unaokadiriwa kuwa euro bilioni 2.5, hapo awali ulifadhiliwa kwa 16% pekee.
Kwa undani, tangazo hili katika mkutano wa Paris linahitaji kutafautishwa. Kati ya euro bilioni 1.5, euro milioni 500 tayari zilitolewa mwaka huu, na sehemu yake inaendana na ahadi za awali zilizothibitishwa tena katika mkutano huo, kulingana na vyanzo kadhaa, anaripoti mwandishi wetu maalum, Patient Ligodi. Swali muhimu pia linabaki: ni lini fedha hizi zitapatikana kweli? Washiriki kadhaa wanakiri kwamba ratiba bado haijawekwa wazi.
Licha ya kutokuwa na uhakika huku, mashirika yasiyo ya kiserikali yanapongeza kama mafanikio ya kisiasa. Mkutano huo umerudisha mgogoro huu kwenye ajenda ya kimataifa. Zaidi ya wajumbe 70 walikuwepo, ikiwa ni pamoja na mataifa yote makubwa ya Magharibi, na mataifa kadhaa yametangaza ufadhili mpya wa ziada.
Rais wa Ufaransa pia ametangaza kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege wa Goma kwa ajili ya safari za ndege zinazobeba msaada wa kibinadamu “katika wiki zijazo.” Sio kwa safari zote za ndege, bali kwa safari za ndege zinazobeba msaada wa kibinadamu mchana na ndege ndogo, kutokana na ukofefu wa vifaa. Emmanuel Macron ameongeza kuwa kuanza tena kwa safari hizi za ndege kutaambatana na njia mpya za kibinadamu, hasa kutoka Burundi.
Hata hivyo Kundi la AFC/M23 limeweka masharti, na Rwanda imesema kwamba mambo haya yanapaswa kujadiliwa ndani ya mfumo wa mchakato wa Doha. Kwa hivyo tangazo hili halikubaliki kwa kauli moja. Kwa mujibu wa Corneille Nangaa, mratibu wa AFC/M23, ambaye kundi lake halikualikwa kwenye mkutano huo, uamuzi huo haufai, hauendani na ukweli uliopo, na umefanywa bila kushauriana hapo awali. Rwanda ina msimamo kama huo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe anabaini kwamba Paris si mahali wala wakati wa kuamua kuhusu hatua kama hiyo. “Sio Paris ambapo tutaamua kuhusu kufunguliwa tena kwa uwanja wa ndege wa Goma. Na jambo la pili, ambalo ni zito zaidi, ni ukweli kwamba kufunguliwa tena kwa uwanja huu wa ndege hakuwezi kufanyika katika muktadha wa sasa wa usalama.”
Alipoulizwa kuhusu mashauriano yanayowezekana na AFC/M23, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noël Barrot amefafanua matamshi ya Rais Macron. “Mkutano huu wa kimataifa umetoa fursa ya kuharakisha majadiliano kuhusu mada hii, ambayo yataendelea ndani ya mfumo wa upatanishi wa Qatar, huku msukumo mpya ukitolewa hapa Paris.” Wakati wa kufungwa kwa mkutano huo, Rais wa Kongo Félix Tshisekedi ametaka ufikiaji wa kibinadamu wa haraka, salama, na uliohakikishwa. Pia amewasihi washiriki kuishinikiza AFC/M23 kuondoka kutoka maeneo inayodhibiti, pamoja na kuondolewa kwa vikosi vya kigeni kutoka ardhi ya Kongo.
Hata hivyo, rais wa Ufaransa ametangaza kwa nguvu: “Hatuwezi kubaki kimya tukitazama janga linaloendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,” amesisitiza, akiongeza kuwa takwimu hizo “haziwezi kuvumilika,” huku mamilioni ya watu “wakilazimika kuyahama makazi yao,” “karibu watu milioni 28 wakikabiliwa na uhaba wa chakula, mwanamke akibakwa kila baada ya dakika nne, na mtoto kila baada ya dakika 30.” “Hatutavumilia vitendo hivi viovu. Ni maumivu makubwa, vilio ambavyo hakuna mtu anayeweza kupuuza,” ameogeza mwishoni mwa mkutano huu ulioandaliwa kwa ushirikiano na Ufaransa na Togo, mpatanishi aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika.
“Usimamizi ulioimarishwa wa Afrika”
Rais wa Togo Faure Gnassingbe, kwa upande wake, ameitaka Afrika kushiriki katika juhudi zake za kibinadamu, “sio tu kwa wajibu wa kimaadili, bali kwa sababu ni suala la heshima na ufanisi.” Pia amehimiza uwazi kamili kuhusu misaada ya kibinadamu.”
