
Kwa uchache watu tisa, wakiwemo watoto watatu wa familia moja, wamepoteza maisha katika maporomoko ya matope yaliyosababishwa na mvua kubwa mashariki mwa Uganda.
Chama cha Msalaba Mwekundu cha Uganda (URCS) kimetangaza habari hiyo na kulinukuu shirika la masuala ya kibinadamu la eneo hilo likithibitisha taarifa hiyo na kusema kuwa, tukio la kwanza lilitokea Alkhamisi asubuhi katika wilaya ya Bukwo, ambapo maporomoko ya matope yalizika nyumba na kuwaua watoto watatu wa familia moja.
“Maafisa wetu wa kujitolea bado wako kwenye eneo hilo wakifanya tathmini na kutafuta watu zaidi,” amesema Irene Nakasiita, msemaji wa URCS katika taarifa rasmi, akisisitiza kuwa ripoti ya kina itatolewa baadaye.
Katika tukio jingine tofauti, maporomoko mengine ya matope yaliyotokea kwenye wilaya jirani ya Kween yaliua watu sita usiku wa kuamkia jana Alkhamisi.
Msemaji wa Shirika la Msalaba Mwekundu la nchini Uganda amesema kuwa, ni vigumu sana kuyafikia maeneo ya maporomoko hayo likiwemo eneo la Bukwo kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha na hali mbaya ya barabara, ambayo imezuia shughuli za kukabiliana na hali hiyo.
Amesema kuwa, timu za uokoaji zinaendelea kufanya kazi kwa karibu na serikali za mitaa na wanajamii ili kusaidia juhudi za uokoaji.
Mashariki mwa Uganda, haswa eneo dogo la milimani la Elgon, linakumbwa na maporomoko ya ardhi ya mara kwa mara wakati wa mvua. Eneo hilo limeshuhudia maporomoko kadhaa ya matope yaliyosababisha vifo katika miaka ya hivi karibuni, ambayo mara nyingi yanahusishwa na ukataji miti ovyo suala ambalo linaifanya ardhi kukosa uimara wa kuzuia kuporomoka udongo.
