-
- Author, Moe Shreif
- Nafasi, Uchunguzi wa BBC Eye
Tahadhari: Ina picha ambazo baadhi zinaweza kukasirisha
Mwanasayansi wa kompyuta katika chuo kikuu kaskazini mwa Uingereza anachunguza picha ya maiti – akiwa katika pilkapilka za kutatua fumbo ambalo limeitesa Mashariki ya Kati kwa karibu miaka 50 kuling’amua.
“Hivi sasa ndivyo anaonekana?” anauliza kwa shaka Profesa Hassan Ugail wa Chuo Kikuu cha Bradford.
Picha ya kidijitali inaonyesha uso uliooza, na inakaribia kuingizwa kwenye algorithimu maalum kwa ajili ya uchunguzi wa BBC.
Picha hiyo ilipigwa na mwandishi wa habari aliyeiona maiti katika chumba cha siri cha kuhifadhi maiti mjini Tripoli, mji mkuu wa Libya, mwaka 2011.
Aliambiwa kuwa mwili huo huenda ulikuwa wa kiongozi wa dini mwenye ushawishi mkubwa, Musa al-Sadr, ambaye alitoweka Libya mwaka 1978.
Kupotea kwa Sadr kumetoa nafasi kwa nadharia nyingi za njama.
Wapo wanaoamini aliuawa, huku wengine wakidai bado yu hai na anashikiliwa mahali fulani nchini Libya.
Kwa wafuasi wake waaminifu, tukio hilo lina mvuto sawa na mauaji ya Rais John F. Kennedy wa Marekani mwaka 1963.
Uchunguzi huu wa muda mrefu wa BBC ulikuwa nyeti kiasi kwamba mimi na timu yangu ya BBC World Service tulizuiliwa Libya kwa siku kadhaa.
Hisia zinachochewa kwa sababu Sadr anaheshimiwa sana kwa mchango wake wa kisiasa, akiwa mtetezi wa Waislamu wa Kishia waliokuwa wakibaguliwa nchini Lebanon, na pia kama kiongozi mashuhuri wa kidini.
Wafuasi wake walimpa cheo cha “Imam”, heshima ya kipekee kwa kiongozi wa Kishia aliye hai, wakimtambua kwa kazi yake ya kuwatumikia.
Kupotea kwake kumeongeza uzito wa kihisia, kwa kuwa kunafanana na simulizi ya “Imam wa 12” aliyefichika kwa mujibu wa dhehebu la Kishia la Twelvers ambalo linaamini kuwa Imam huyo hakufa, bali atarudi mwishoni mwa wakati kuleta haki duniani.
Zaidi ya hayo, baadhi wanaamini kuwa kupotea kwa Sadr kulibadilisha mwelekeo wa siasa za Mashariki ya Kati.
Wengine wanasema kiongozi huyo mwenye asili ya Kiirani na Kilebanoni alikuwa karibu kutumia ushawishi wake kuielekeza Iran na eneo zima kwenye njia ya wastani zaidi, lakini alitoweka siku chache kabla ya Mapinduzi ya Iran.
Hivyo basi, uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Bradford ulilenga jambo la maana sana.
Mwandishi aliyepiga picha alituambia kuwa mwili huo ulikuwa mrefu sana na Sadr alikuwa anajulikana kuwa na urefu wa mita 1.98 (futi 6 na inchi 5).
Lakini uso huo haukuwa na alama nyingi za utambulisho.
Je, tunaweza hatimaye kutatua fumbo hili?
Chanzo cha picha, Imam Sadr Foundation
Mimi natoka kijiji cha Yammouneh, kilicho juu milimani mwa Lebanon, ambako hadithi bado zinasimuliwa kuhusu baridi kali ya mwaka 1968, ambapo baada ya kijiji kuharibiwa na maporomoko ya theluji, Musa al-Sadr alivuka theluji nene kuja kuwasaidia.
Wakazi wa kijiji bado husimulia tukio hilo kwa mshangao mkubwa.
Mmoja aliniambia, akikumbuka akiwa na miaka minne: “Ilikuwa kama ndoto… Alitembea juu ya theluji, akifuatiwa na wakazi wote… Nilimfuata tu ili niguse joho la Imam.”
Wakati huo, Sadr hakuwa maarufu sana katika kijiji kilichotengwa kama Yammouneh, lakini alikuwa polepole akipata umaarufu kitaifa.
Kufikia mwishoni mwa miaka ya 1960, alikuwa amekuwa mtu mashuhuri nchini Lebanon, akihimiza mazungumzo ya dini mbalimbali na mshikamano wa kitaifa.
Mwaka 1974, alianzisha harakati ya “Movement of the Deprived” (Harakati ya Wanyonge), chama cha kijamii na kisiasa kilichodai uwakilishi wa haki kwa Waislamu wa Kishia na ukombozi wa kijamii na kiuchumi kwa maskini wa dini zote.
Alikataa kabisa siasa za mgawanyiko wa kidini kiasi cha kutoa mahubiri katika makanisa ya Kikristo.
Chanzo cha picha, Imam Sadr Foundation
Tarehe 25 Agosti 1978, Sadr alisafiri kwenda Libya kwa mwaliko wa kukutana na kiongozi wa taifa hilo wakati huo, Kanali Muammar Gaddafi.
Wakati huo Lebanon ilikuwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe, na wapiganaji wa Kipalestina walikuwa wameshika maeneo mengi ya kusini, ambako ndiko wafuasi wengi wa Sadr waliishi.
Sadr alitaka Gaddafi, aliyekuwa akiunga mkono Wapalestina, aingilie kati ili kuwalinda raia wa Lebanon waliokuwa wakiteseka.
Lakini baada ya siku sita akisubiri kikao, Sadr alionekana kwa mara ya mwisho tarehe 31 Agosti, akisafirishwa kwa gari la serikali ya Libya kutoka hoteli mjini Tripoli.
Serikali ya Gaddafi ilidai kuwa Sadr alisafiri kwenda Roma, lakini uchunguzi uliofuata ulithibitisha hilo kuwa si kweli.
Katika enzi za Gaddafi, uandishi wa habari huru haukuwezekana.
Hata hivyo, mwaka 2011, wakati Walibya walipoasi wakati wa Mapinduzi ya Kiarabu, milango ya ukweli ilianza kufunguka.
Kassem Hamadé, mwandishi wa habari mwenye uraia wa Lebanon na Uswidi, ambaye aliripoti mapinduzi hayo, aliambiwa kuhusu chumba cha siri cha kuhifadhi maiti mjini Tripoli ambacho, kwa mujibu wa chanzo, kilikuwa na mwili wa Sadr.
Alionyeshwa miili 17 katika jokofu mmoja alikuwa mtoto, wengine wanaume watu wazima.
Kulingana na taarifa alizopewa, miili hiyo ilikuwa imehifadhiwa kwa takribani miaka 30 jambo linalolingana na kipindi cha kutoweka kwa Sadr.
Ni mwili mmoja tu uliokuwa na sura inayofanana na yake.
Kassem alikumbuka: “Mfanyakazi wa mochari alifungua droo moja na kuonyesha mwili, na mambo mawili yalinishangaza mara moja.” Kwanza, rangi ya ngozi, uso na nywele zilionekana bado zinafanana na za Sadr, licha ya muda mrefu kupita. Pili, ilionekana kama mtu huyo aliuawa kwa kupigwa risasi au pigo zito kwenye paji la uso.
Lakini tungewezaje kujua kwa hakika huyu alikuwa Sadr?
Ulinganisho wa kielektroniki
Chanzo cha picha, Kassem Hamadé
So we took the photo that Kassem had taken in the mortuary to a team at Bradford University which, for the past 20 years, has been developing a unique algorithm called Deep Face Recognition. It identifies complex similarities between photos, and has been shown to be extremely reliable in tests, even on imperfect images.
Ili kuthibitisha, picha hiyo ilipelekwa kwa timu ya Chuo Kikuu cha Bradford, ambayo kwa zaidi ya miaka 20 imekuwa ikitengeneza algorithimu ya kipekee ya utambuzi wa uso kwa kina yaani “Deep Face Recognition.”
Teknolojia hiyo inatambua mfanano tata hata katika picha zisizo kamilifu.
Profesa Ugail alilinganisha picha ya mochari na picha nne tofauti za Sadr akiwa hai.
Programu hiyo iliipa picha hiyo alama kati ya 60 hadi 70 ikionyesha uwezekano mkubwa kuwa huyo alikuwa Sadr au jamaa yake wa karibu.
Ili kuthibitisha zaidi, picha hiyo ililinganishwa na picha za jamaa sita wa familia ya Sadr, pamoja na picha 100 za wanaume wa Kiarabu waliokuwa na sura inayofanana na ya Sadr.
Picha za familia zilifanana zaidi kuliko zile za watu wa nasibu.
Hata hivyo, mlingano mkubwa zaidi ulikuwa kati ya picha ya mochari na zile za Sadr akiwa hai.
Hii ilionyesha kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba mwili aliouona Kassem ulikuwa wa Sadr.
Na kwa kuwa fuvu lilikuwa limeharibika, dalili zilikuwa wazi kwamba huenda aliuawa.
Machi 2023, takriban miaka minne tangu tulipoanza uchunguzi huu, tulisafiri hadi Libya kutafuta mashahidi na mwili wenyewe.
Tulikuwa tukijua hadithi hiyo ilikuwa nyeti lakini hata hivyo, tulishangazwa na majibu ya Libya.
Siku ya pili nchini humo, tukiwa Tripoli, tulijaribu kutambua eneo la mochwari.
Kassem ambaye alikuwa ameandamana na timu ya BBC, hakuweza kukumbuka jina la eneo alilolitembelea mwaka 2011, ila alikumbuka lilikuwa karibu na hospitali.
Tulipoifikia hospitali moja kwa miguu, Kassem alisema kwa uhakika: “Hii ndiyo. Najua.Hili ndo jengo lilikuwa na mochari hiyo ya siri”.
Sehemu ya nje ya jengo ndiyo ilikuwa kitu cha mwisho tulichoweza kurekodi.
Tuliomba ruhusa ya kurekodi filamu ndani, lakini vibali vyetu vilighairiwa.
Siku iliyofuata, kundi la watu wasiojulikana – ambao tungejua baadaye walikuwa maafisa wa upelelezi wa Libya – walitukamata bila maelezo.
Tulipelekwa kwenye gereza linalosimamiwa na maafisa wa kijasusi wa Libya, ambapo tulifungwa katika kifungo cha upweke, na kushutumiwa kwa ujasusi.
Tulifumbwa macho, tukahojiwa mara kwa mara, na kuambiwa kwamba hakuna mtu anayeweza kutusaidia.
Watekaji wetu walisema tutakuwa huko kwa miongo kadhaa.
Tulitumia siku sita za kiwewe kizuizini.
Hatimaye, baada ya shinikizo kutoka kwa BBC na serikali ya Uingereza, tuliachiliwa na kufukuzwa nchini.
Ilikuwa inasumbua kuhisi tumekuwa sehemu ya hadithi.
Libya bado imegawanyika katika tawala mbili zinazohasimiana na wanamgambo wanaoshindana, na wafanyakazi katika gereza hilo walikuwa wameonyesha idara ya ujasusi ya Libya inaendeshwa na wafuasi wa zamani wa Gaddafi ambao hawangetaka BBC ichunguze kupotea kwa Sadr.
Fumbo la kifo cha Musa al-Sadr
Chanzo cha picha, Getty Images
Baadhi ya watu wameamini kwa muda mrefu kwamba Musa al-Sadr aliuawa.
Daktari Hussein Kenaan, aliyewahi kuwa mhadhiri wa Lebanon aliyeishi Marekani, anasema kuwa aliitembelea Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani mjini Washington wiki ile Sadr alipotea mwaka 1978, na akaambiwa kwamba walikuwa wamepokea taarifa kuwa Sadr alikuwa tayari ameuawa.
Kauli hii inaungwa mkono na aliyekuwa Waziri wa Sheria wa Libya, Mustafa Abdel Jalil, ambaye alimwambia mwandishi wa habari Kassem mwaka 2011:
“Siku ya pili au ya tatu walighushi nyaraka zake, wakadai alikuwa safarini kuelekea Italia. Kisha wakamuua ndani ya magereza ya Libya.”
“Gaddafi ndiye aliyekuwa na kauli ya mwisho katika kila uamuzi.”
Kama Gaddafi kweli aliamuru kuuawa kwa Sadr, sababu ilikuwa ipi?
Mtaalamu wa masuala ya Iran, Andrew Cooper, anasema kwamba kuna nadharia inayodai kuwa Gaddafi aliathiriwa na wanamgambo wa Kiislamu wenye misimamo mikali kutoka Iran, ambao waliingiwa na hofu kwamba Sadr angezuia malengo yao ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Ingawa Sadr aliunga mkono wanamapinduzi waliotaka kumuangusha Shah Mohammad Reza Pahlavi, msimamo wake wa wastani ulipingana vikali na mitazamo ya wanamapinduzi wenye misimamo mikali.
Kwa hiyo, alionekana kuwa tishio kwao.
Kwa mujibu wa Cooper, wiki moja kabla ya kutoweka kwake, Sadr aliandika barua kwa Shah wa Iran akijitolea kusaidia.
Katika utafiti wake wa wasifu wa Shah, Cooper alifanya mahojiano na Parviz Sabeti, aliyekuwa mkuu wa idara ya kupambana na ujasusi ndani ya polisi ya siri ya Shah.
Sabeti alisema barua hiyo ilieleza nia ya Sadr kusaidia kuwadhibiti wanamgambo wa Kiislamu kwa kupendekeza mabadiliko ya sera ambayo yangewavutia wale wa upande wa wastani katika upinzani.
Uwepo wa barua hiyo pia unathibitishwa na balozi wa zamani wa Lebanon nchini Iran, Khalil al-Khalil, ambaye alisema Sadr alikuwa ameomba mkutano na Shah uliopangwa kufanyika tarehe 7 Septemba 1978.
Cooper anaamini kwamba taarifa kuhusu barua hiyo ilivuja na kufika mikononi mwa wanamapinduzi wa Kiirani wenye misimamo mikali, ambao waliweza kumshawishi Gaddafi kuchukua hatua.
Pande nyingine zenye maslahi
Lakini si Wairani tu walioweza kuwa na sababu ya kutaka kifo cha Sadr.
Gaddafi alikuwa akiunga mkono kijeshi wapiganaji wa Kipalestina waliokuwa wakishambulia Israel kutoka kusini mwa Lebanon.
Wakati huo, Sadr alihusiana na juhudi za kusuluhisha hali hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Ukombozi wa Palestina (PLO).
Inaaminika kuwa PLO waliogopa kuwa Sadr, ambaye alikuwa na wasiwasi kwamba wapiganaji wao waliwahatarisha raia wa Lebanon, angemshawishi Gaddafi kuwadhibiti.
Je, Sadr bado yu hai?
Wakati wengi wanaamini kuwa Sadr aliuawa, wapo wengine wanaodai kwa msimamo mkali kwamba bado yu hai.
Wanaamini wakiwemo wanachama wa shirika alilolianzisha miaka ya 1970, ambalo sasa ni chama kikubwa cha kisiasa cha Waislamu wa Kishia wa Lebanon Amal.
Kiongozi wa chama hicho, ambaye pia ni Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri, anasisitiza kwamba hakuna ushahidi wowote unaoonyesha Sadr ambaye leo angekuwa na umri wa miaka 97 amekufa.
Mwaka 2011, wakati mwandishi Kassem alipozuru mochari ya siri alipopiga picha ya mwili unaodhaniwa kuwa wa Sadr, hakukomea hapo.
Alifanikiwa pia kung’oa nywele chache zenye mizizi kwa ajili ya uchunguzi wa vinasaba (DNA), na akazikabidhi kwa maafisa waandamizi katika ofisi ya Berri ili zichunguzwe.
Mlinganisho wa DNA kati ya nywele hizo na jamaa wa familia ya Sadr ungetoa ushahidi usiopingika kuhusu utambulisho wa mwili huo.
Hata hivyo, ofisi ya Berri haikumjibu Kassem kamwe.
Jaji Hassan al-Shami, miongoni mwa maafisa walioteuliwa na serikali ya Lebanon kuchunguza kutoweka kwa Sadr, alisema kuwa chama cha Amal kilimfahamisha kwamba sampuli hiyo ya nywele “ilipotea kutokana na hitilafu ya kiufundi.”
BBC iliwasilisha matokeo ya mfumo wa utambuzi wa sura kwa mwana wa Sadr, Sayyed Sadreddine Sadr.
Alifika kwenye kikao hicho akiwa na afisa mwandamizi wa Amal, Hajj Samih Haidous, na Jaji al-Shami.
Wote kwa pamoja walikataa matokeo hayo.
Matokeo ya teknolojia yakubaliwa?
Chanzo cha picha, Imam Sadr Foundation
Sadreddine alisema kuwa ni “dhahiri” kutokana na muonekano wa mwili katika picha kuwa huyo si baba yake.
Aidha, alieleza kuwa picha hiyo “inapingana na taarifa tulizonazo baada ya mwaka 2011”, ambazo zinadai kuwa Sadr bado yupo hai na anashikiliwa katika gereza nchini Libya.
BBC haikupata ushahidi wowote unaounga mkono dai hili.
Uchunguzi wa BBC ulionesha kwamba imani kuwa Sadr bado yuko hai ni kiini cha matumaini na mshikamano kwa Waislamu wa Kishia nchini Lebanon.
Kila tarehe 31 Agosti, chama cha Amal huadhimisha kumbukumbu ya kutoweka kwake kama tukio la kitaifa.
BBC iliwasiliana mara kadhaa na ofisi ya Nabih Berri kuomba mahojiano au maoni kuhusu matokeo haya ila hawakujibu.
Vivyo hivyo, BBC iliomba maelezo kutoka kwa serikali ya Libya kuhusu uchunguzi huu, pamoja na sababu ya kukamatwa kwa timu ya BBC na maafisa wa ujasusi wa Libya lakini hakuna jibu lililotolewa.