
Umoja wa Mataifa jana Ijumaa ulitoa wito kwa Washington kusimamisha mashambulizi yake dhidi ya meli na boti katika Bahari ya Karibi na mashariki mwa Pasifiki zinazotuhumiwa na Washington kuwa zinafanya biashara haramu ya dawa za kulevya, na kukomesha mauaji yanayofanywa kinyume cha sheria.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk amesema: “Mashambulizi haya na ongezeko la vifo vinavyotokana nayo, hayakubaliki”. Marekani inalazimika kukomesha mashambulizi haya na kuchukua hatua zote muhimu ili kuzuia mauaji ya watu walio ndani ya boti hizo, bila kujali mwenendo wa uhalifu unaohusishwa nao.”
Türk ametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu mashambuulizi hayo ya Marekani, akisema ofisi yake haikuona sababu yoyote ya kuyahalalisha chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kwamba anaamini “mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani kwenye meli na boti katika eneo la Karibi na Pasifiki yanakiuka sheria ya kimataifa ya haki za binadamu.”
Rais Donald Trump wa Marekani amezidisha operesheni za kijeshi na kijasusi dhidi ya Venezuela, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya meli zinazodaiwa kubeba dawa za kulevya katika eneo la Caribbean ambayo yameua makumi ya watu.
Nicolas Maduro wa Venezuela anatambuliwa kuwa miongoni mwa wapinzani wakali wa sera za kibeberu za Marekani na washirika wake, na amekuwa mkosoaji na mpinzani mkubwa wa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel, ikisaidiwa na nchi za Magharibi dhidi ya watu wa Palestina.
Maduro anasema utawala wa Trump “unabuni” vita dhidi ya taifa hilo la Amerika Kusini ili kuiangusha serikali yake na kuchukua udhibiti wa akiba yake kubwa ya nishati.
Kiongozi huyo wa Venezuela amenusurika majaribio mengi ya mauaji yanayofadhiliwa na Marekani na njama zingine za Washington na vibaraka wake wa eneo hilo za kutaka kumuua.