Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura ya kurefusha kwa mwaka mmoja muda wa kazi za ujumbe wake ulioko Sahara Magharibi (MINURSO), sambamba na kuidhinisha rasmi mpango wa serikali ya Morocco wa kutoa mamlaka ya ndani kwa eneo hilo kama msingi pekee wa kutatua mgogoro huo wa miongo kadhaa, hatua ambayo imesababisha mpasuko mkubwa katika jamii ya kimataifa.

Azimio hilo, lililowasilishwa na Marekani, limepitishwa kwa kura 11 za kuunga mkono na kura 3 za kujizuia, likiashiria kujiri mabadiliko makubwa ya kidiplomasia kwa kutambua rasmi Pendekezo la Utoaji Mamlaka la Morocco la 2007 kama “msingi pekee wa kufikia kwenye suluhisho la haki na la kudumu.”

Uamuzi huo wa Baraza la Usalama umekinzana na sisitizo la jadi la Umoja wa Mataifa kuhusu kufikiwa suluhisho la kisiasa “linalokubaliwa na pande zote” mbili litakjalofikiwa kupitia mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Morocco na harakati ya ukombozi wa Sahara Magharibi POLISARIO.

Kura ya kupitisha azimio hilo lililoandaliwa na Marekani imeibua mgawanyiko na mpasuko mkubwa. Algeria, ambayo ni muungaji mkono mkuu wa Polisario, ilijizuia kupiga kura, huku balozi wake akisema yaliyomo ndani ya azimio hilo “hayaonyeshi kwa usahihi… msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhusu uondoaji wa ukoloni.”

Naibu balozi wa Afrika Kusini katika UN ametilia nguvu hoja hiyo akisisitiza kwamba mgogoro wa Sahara Magharibi “hauwezi kutatuliwa kupitia mchakato wa amani ambao si jumuishi.”

Naye mwakilishi wa Polisario ametangaza kwamba azimio hilo la Baraza la Usalama halitambui mamlaka ya utawala wa Morocco Sahara Magharibi na kwamba mapambano yao ya kupigania kujitawala “hayataisha kamwe.”

Azimio hilo linazidisha vita vya kidiplomasia dhidi ya Sahara Magharibi, koloni la zamani la Uhispania lililokuwa likidhibitiwa kwa kiasi kikubwa na Morocco tangu 1975 lakini likichukuliwa kuwa ni eneo lisilojitawala na Umoja wa Mataifa.

Kura hiyo inaashiria kuongezeka uungwaji mkono wa Magharibi kwa mpango wa Morocco tangu Marekani chini ya Donald Trump ilipouidhinisha mpango huo kwa mara ya kwanza mwaka 2020, na hivyo kuitenga zaidi harakati ya Polisario na washirika wake huku ikiacha swali la msingi kuhusu Wasahara Magharibi kujiamulia mustakabali wao likiwa bado halijapatiwa jibu.

Itakumbukwa kuwa, Marekani ilichukua uamuzi wa kuunga mkono mpango huo wa Morocco kama njia ya kuirubuni serikali ya Rabat ianzishe uhusiano rasmi wa kidiplomasia na utawala wa kizayuni wa Israel…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *