Jeshi la Uganda UPDF limetangaza kuwa, limefanikiwa kuzima mlolongo wa mashambulizi yaliyoratibiwa vyema na vikundi vyenye silaha ambavyo vilishambulia vituo vya kijeshi na polisi katika maeneo ya magharibi ya nchi hiyo.

Katika taarifa iliyotolewa mjini Kampala, msemaji wa UPDF, Felix Kulayigye amesema kuwa, washambuliaji hao, wakiwa na bunduki ndogo ndogo na mapanga, walianzisha mashambulizi katika vituo vya polisi vya Lugendabara kwenye wilaya ya Kasese ya mpaka wa magharibi mwa Uganda na kushambulia maeneo ya kijeshi huko Malindi na Kakuka katika wilaya ya Bundibugyo na Skuli ya Canon Apollo huko Fort Portal katika wilaya ya Kabarole.

Kulayigye ameongeza kuwa, washambuliaji walijaribu kuvuruga vituo vya usalama na kuchochea machafuko katika eneo hilo.

“Vikosi vyetu, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi la Uganda, vilijibu haraka na kwa umakini ili kupunguza tishio hilo,” amesema msemaji huyo wa jeshi la UPDF.

Ameongeza kuwa, washambuliaji hao walizidiwa nguvu na kwamba operesheni zinaendelea hivi sasa kuwasaka wale waliokimbia. “Kwa bahati mbaya, washambuliaji walimuua mwanamke mmoja ambaye ni raia wa kawaida huko Malindi, na mwanajeshi mmoja aliuawa vitani,” amesema Kulayigye na kuongeza kuwa, uchunguzi unaendelea ili kubaini asili, nia na uhusiano wa washambuliaji hao.

Vyombo vya habari vya ndani ya Uganda vimeripoti kwamba washambuliaji wapatao 20 wanaodaiwa walikuwa na mapanga waliuawa katika wilaya hizo tatu Jumamosi asubuhi.

“Hatua za ziada za usalama zimechukuliwa ili kuimarisha utulivu na kuzuia matukio mengine kama hayo. Tunawasihi wananchi kubaki watulivu, macho na kushirikiana na vyombo vya usalama,” amesema Kulayigye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *