
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limesema limejiandaa na limesimama thabiti mbele ya vitisho vya maadui, na linaendelea kujitolea kulinda mipaka ya ardhi na mfumo wa Kiislamu.
Katika taarifa ya Jumatatu, Kamandi Kuu ya Jeshi imetoa pongezi kwa wananchi wa Iran katika kuelekea kumbukumbu ya siku ya kuchukuliwa kwa ubalozi wa Marekani mnamo Novemba 4, 1979.
Taarifa hiyo imesema kuwa tukio hilo kubwa lilifichua asili ovu ya ubeberu wa kimataifa na kiwango cha uingiliaji wake wa katika masuala ya ndani ya Iran.
Aidha, taarifa hiyo ililitaja tukio hilo kama “kipindi cha mabadiliko” katika historia ya kisasa, na chanzo cha kuimarika kwa uhuru wa kisiasa wa Iran pamoja na heshima ya kitaifa.
Jeshi la Iran limesema kuwa hatua ya wanafunzi kuudhibiti ubalozi huo ilikuwa ishara ya uelewa wa kimapinduzi, ushujaa wa vijana waaminifu, na uthibitisho wa nia ya wananchi dhidi ya nguvu za ubeberu wa kimataifa.
Aidha, jeshi limetangaza upya azma ya taifa kuendelea na njia ya kudumisha uhuru na heshima yake.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Novemba 4 ni ukumbusho kwamba taifa la Iran halitaruhusu mtu yeyote kudhoofisha uhuru wake wa kitaifa wala heshima yake.
Mnamo Novemba 4, 1979, wanafunzi wa Iran, wakilalamikia njama za Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu, waliteka na kuzingira Ubalozi wa Marekani mjini Tehran, uliokuwa ukijulikana kama “Pango la Ujasusi,” kwa lengo la kuzuia dola hilo kufikia malengo yake haramu dhidi ya mapinduzi yaliyokuwa yameshinda mwezi Februari mwaka huo.
Tukio hilo baadaye lilitangazwa kuwa Siku ya Kitaifa ya Mapambano dhidi ya Ubeberu wa Kimataifa, ambayo pia huadhimishwa kama Siku ya Taifa ya Wanafunzi.
Kila mwaka, katika siku ya 13 ya mwezi wa Aban kwa kalenda ya Iran, wananchi—hasa wanafunzi—huadhimisha siku hiyo kwa kufanya maandamano ya kitaifa, wakiwahimiza Waislamu na wapigania uhuru kusimama dhidi ya nguvu za ubeberu.
Siku hiyo imeendelea kuwa ishara ya muqawama na mapambano makali dhidi ya ubeberu wa Magharibi.