Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Iran amesema kwamba eneo la Magharibi mwa Asia kwa sasa limo katika na “vita halisi” na utawala wa Israel, akisisitiza kwamba hali ya eneo hilo iimekwenda mbali zaidi ya vitisho tu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari wa kila wiki mjini Tehran, Esmaeil Baqaei amesema kwamba hakuna shaka miongoni mwa nchi za kanda hii kwamba tishio kuu linatokana na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ameendelea zaidi akisema, “kutumia neno ’tishio’ si sahihi kabisa, kwani tuko katika vita halisi vya kikanda na utawala wa Kizayuni.”

Ameeleza kwamba tishio linaashiria hatua inayoweza kutukia hapo baadaye, ilhali kwa zaidi ya miaka miwili, kumekuwa na “mauaji ya kikatili” ya watu huko Palestina, mashambulizi dhidi ya nchi kadhaa za kikanda na uvamizi unaoendelea.

Amesema kuwa kuna mwafaka wa wazi wa kikanda kuhusu mambo mawili: kwamba utawala wa Israel ndio tishio kuu, na kwamba nchi za kanda ya Magharibi mwa Asia zinahitaji maelewano na makubaliano ili kuhakikisha usalama wao.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amezungumzia usitishaji mapigano uliubiniwa na Marekani huko Gaza, akisema kwamba ingawa neno “ukiukaji wa kusitisha mapigano” linatumika sasa, ukweli ni kwamba “mauaji ya kimbari na maangamizi ya umma wa Wapalestina yanaendelea huko Gaza na Ukingo wa Magharibi.”

Ameeleza kuwa tangu mazungumzo ya kusitisha mapigano yalipoanza, zaidi ya Wapalestina 200 wameuawa na zaidi ya 600 kujeruhiwa.

Akijibu maswali kuhusu mazungumzo baina ya Iran na Marekani, Baqaei amefafanua kwamba hakuna ujumbe rasmi uliopokewa kutoka upande wa Marekani kupitia Oman.

“Iran ilishambuliwa wakati wa mazungumzo ya kidiplomasia (na Marekani). Watu wa Iran hawawezi kusahau jambo hili,” amesema Baqaei akiwa na maana ya mashambuliizi ya Marekani na Israel mwezi Juni ambayo yaliwaua makamanda kadhaa wa ngazi za juu wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia na raia wa Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kwamba Marekani imethibitisha kuwa haizingatii mahitaji ya mazungumzo yanayofaa, na kwamba mazungumzo yanaweza kuzingatiwa pale pande husika zinapokubali maslahi ya kila mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *