ILE ratiba ya CAF kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi si umeiona? Basi wakubwa Simba na Yanga wametoa tamko zito juu ya mechi hizo sita za kila timu.

Simba imepangwa kundi D lenye timu za Esperance de Tunis ya Tunisia, Petro de Luanda ya Angola na Stade Malien ya Mali.

Wekundu hao wataanzia nyumbani dhidi ya Petro de Luanda kisha itawafuata Malien na baadaye Esperance lakini utamu zaidi ni kwamba watamalizia mechi za makundi nyumbani.

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Azzim Dewji, ameiambia Mwanaspoti kuwa ratiba hiyo imewafikia na hesabu zao ni kubwa kuhakikisha wanatoboa kwenda hatua ya robo fainali kama kawaida yao.

Azzim ambaye ni mfadhili zamani wa Simba, amesema uongozi unajipanga sawasawa ikizichukulia mechi hizo kwa uzito mkubwa ambapo inataka kuanza na ushindi lakini mwisho wamalize vinara kwenye kundi hilo.

MABO 02

Bilionea huyo aliongeza kuwa haitakuwa ajabu kwa Simba kupata ushindi wa mechi za nyumbani kwani rekodi yao inajulikana lakini wanajipanga kwenda kutafuta ushindi mpaka ugenini kwenye mechi tatu dhidi ya Petro, Malien na Esperance.

“Ratiba ni kweli tumeiona, tumeridhika nayo, hatuwezi kusema ni rahisi sana lakini tunataka kujipanga sawa na hizo mechi, kila timu iliyofika hapa ni kubwa, kwa hiyo tunahitaji kujipanga, kikubwa kukabiliana nazo,” amesema Azzim.

“Kila mmoja Afrika anaijua Simba ikiwa nyumbani, hapa sio rahisi sana kushinda dhidi yetu, tuna mashabiki wanaojua kuipigania timu yao na kikosi imara kinachojua thamani ya kucheza nyumbani, kila timu ikija hapa kukutana na sisi inajua ugumu wake.

“Safari hii tunataka kufanya vizuri zaidi, tunataka kwenda kushinda hata ugenini kwenye mechi tatu za ugenini, lengo letu ni kumaliza vinara wa kundi na kwenda robo fainali.

“Uongozi tunakwenda kujipanga lakini naamini mashabiki wetu wako pamoja na timu wataendelea kujipanga kuhakikisha timu yao inafanya vizuri kama kauli yetu inavyosema Simba nguvu moja.”

Wakati Simba wakitoa kauli hiyo, mtani wake Yanga ameangukia kundi gumu kidogo la B lenye Waarabu watatu ambao ni Al Ahly ya Misri, AS FAR ya Morocco na JS Kabylie ya Algeria.

Baadhi ya mashabiki wa Yanga ni kama wameipokea ratiba hiyo kwa presha wakiona kama ni safari ngumu lakini uongozi wao umetoka hadharani na kutoa neno zito.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo, ameiambia Mwanaspoti kuwa ratiba hiyo wameipokea na sasa wanaanza hesabu za namna ya kukabiliana na mechi hizo sita.

MABO 01

Gumbo amesema hawana sababu ya kuihofia timu yoyote zaidi ya kutakiwa kuwaheshimu kwa kiasi wapinzani na kwamba watakuwa na hesabu za kimyakimya na zile za hadharani namna ya kwenda kuzicheza mechi hizo.

“Unaweza kusema ni ratiba ngumu lakini sisi ni Yanga tunajua ubora wa wapinzani wetu lakini tutajipanga kukabiliana na timu moja kwenda nyingine bila unyonge,” amesema Gumbo.

“Tuna timu imara sana na hivi karibuni mmeona tumeboresha benchi letu la ufundi kwa kumleta kocha mkubwa, tuko kwenye afya nzuri ya kwenda kushindana.

“Tunakwenda kujipanga sawasawa, tutakutana nna benchi la ufundi lakini yapo mambo yatakuwa hadharani na mambo mengine hayatakuwa wazi, sio kila taarifa ya kukabiliana na adui yako inatakiwa kufika kwa mpinzani.

“Mashabiki wetu hawatakiwi kutishwa, Yanga ni kubwa, wanaodhani tutaanguka, tunatakiwa kwenda kuwathibitishia kwa vitendo ukubwa wetu, kuna ratuba huko nyuma zilitoka tukaona tutashinda lakini tukakwama na kuna ratuba pia tuliziona ngumu baadaye tukatoboa.”

KUNDI LA YANGA
Al Ahly
Yanga
AS FAR
JS Kabylie

KUNDI LA SIMBA
Espérance Sportive de Tunis
Simba
Petro de Luanda
Stade Malien (Mali)

MABO 03

RATIBA YA YANGA
NOVEMBA 21-23, 2025
Yanga vs AS FAR

NOVEMBA 28-30, 2025
JS Kabylie vs Yanga

JANUARI 23-25, 2025
Al Ahly vs Yanga

JANUARI 30 – Februari 1, 2025
Yanga VS Al Ahly

FEBRUARI 6-8, 2025
AS FAR vs Yanga

FEBRUARI 13-15, 2025
Yanga vs JS Kabylie

MABO 04

RATIBA YA SIMBA
NOVEMBA 21-23, 2025
Simba vs Petro Luanda

NOVEMBA 28-30, 2025
Stade Malien vs Simba

JANUARI 23-25, 2025
Espérance vs Simba

JANUARI 30 – Februari 1, 2025
Simba vs Espérance

FEBRUARI 6-8, 2025
Petro Luanda vs Simba

FEBRUARI 13-15, 2025
Simba vs Stade Malien

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *