Waislamu na Wakristo wa Nigeria wamesisitiza kuishi pamoja kwa amani na maelewano na kusema kuwa vitisho vya Rais wa Marekani dhidi ya nchi hiyo kuwa havikubaliki.

Shirika la habari la IRNA jana lililinukuu shirika la habari la AFP nakuashiria radiamali ya  Waislamu na Wakristo wa Nigeria kuhusu vitisho vya Rais Donald Trumpwa Marekani vya kuingilia kijeshi nchini humo na kuandika: Wananchi wa Nigeria Waislamu na Wakristo  wanapinga vitisho vya Rais Donald Trump wa Marekani vya kutaka kuingilia kijeshi nchini humo.  

Wananchi wa Nigeria wa dini hizo mbili wamesisitiza katika mahojiano na shirika la habari la Ufaransa kwamba chanzo cha mapigano nchini Nigeria si suala la udini bali mizizo nchini humo inasababishwa na usimamizi mbovu wa ardhi, umaskini na kutowajibika taasisi za serikali; ambapo waathirika ni watu wote Wakristo na Waislamu. 

Nigeria, nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika, imegawanyika takriban sawa kati ya kusini yenye Wakristo wengi na kaskazini yenye Waislamu wengi. Katika Jimbo la Plateau na maeneo mengine ya Nigeria maarufu kama “Ukanda wa Kati,” kunashuhudiwa mapigano ya umwagaji damu  kati ya wakulima Wakristo walio wengi na wafugaji Waislamu wakigombania rasilimali na ardhi katika eneo hilo. Mapigano haya mara kwa mara yamesababisha vifo vya makumi ya watu na uharibifu wa vijiji. 

Trump alitangaza kwenye mitandao ya kijamii mwishoni mwa juma lililopita kwamba ameiamuru Wizara ya Vita ya Marekani (Pentagon) kuandaa mpango tarajiwa wa kutekeleza mashambulizi ya kijeshi “kukabiliana na mauaji makubwa ya Wakristo nchini Nigeria.”

“Tunaweza kutuma askari au kutekeleza mashambulizi ya anga; tunachunguza machaguo tofauti”, amesemaTrump katika mkutano na waandishi wa habari. 

Naye Rais Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria amejibu kauli hizi za Trump kwa kusema: “Kuishi pamoja kidini kwa maelewano ni sehemu ya utambulisho wa kitaifa wa nchi hiyo”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *