Kukatika kwa mtandao wa intaneti kwa siku sita kunaweza kufananishwa na kuzimwa kwa pumzi ya dunia yetu ya sasa. Tulibaki kimya, tukitazamana, tukijifunza upya namna ya kuishi bila kelele za arifa, bila mwanga wa skrini, bila ule ulimwengu wa kidijitali unaotufuatilia kila dakika. Nilichogundua baada ya siku hizo sita ni jambo moja tu: Tuliishi. Haikuwa rahisi, lakini tuliweza.

Tuliolelewa enzi za karatasi na kalamu tulifunzwa nidhamu ya kazi, tulijua namna ya kuendelea hata pale mifumo ilipolegalega. Tulifahamu njia mbadala. Kulikuwa na ubunifu, kulikuwa na watu, kulikuwa na utatuzi. Watu walitatua changamoto bila kutegemea mifumo ya kiteknolojia kwa akili, uzoefu na ubunifu wa mikono yao. Tulihesabu kwa kalamu, tukarekodi kwa makabrasha, tukasafirisha habari kwa neno na barua. Hakukuwa na mitandao, lakini kulikuwa na mawasiliano pamoja na mahusiano ya watu ya ana kwa ana. Na tulisonga mbele.

Yaliyojiri mtandao ilipokatika

Mtandao ulipokatika, nilijikuta nikishukuru kwamba bado kulikuwa na pumzi fulani ya mawasiliano. Simu za sauti, ujumbe mfupi na M-Pesa vilibaki kuwa kama mishipa ya mwisho ya damu kwenye mwili uliochoka. Watu wakarudi kwenye mawasiliano ya asili, yale ya neno kwa neno, uso kwa uso. Tena, “habari kwa mdomo” ikawa nguvu kuu ya mawasiliano, jambo ambalo watangazaji wamelielewa tangu enzi.

Ujumbe ulisafiri kupitia simu, kupitia maneno, kupitia imani. Hakukuwa na “forward” wala “share”, lakini kulikuwa na uaminifu wa mtu kumweleza mwingine kile alichosikia. Ilikuwa kama kurudi nyumbani, mahali ambapo hapo zamani palitawaliwa na mawasiliano ya sauti na ana kwa ana, yenye usikivu wa kweli na uhusiano uliounganisha mioyo ya watu kupitia simu zao katika siku hizo sita.

Nilikuwa Kagera, ambako maisha yalionekana kana kwamba hayajaguswa na ile hali ya kurudishwa kwenye zama, ambazo hapo awali hazikutegemea teknolojia kwa kiasi kikubwa. Nilitembea kati ya wilaya, nikaenda kwenye matukio ya furaha na ya huzuni, nikasalimiana na watu ana kwa ana. Kulikuwa na hewa tulivu, mazungumzo marefu na siku zenye mwendo wake wa kawaida. Lakini chini ya utulivu huo, dalili za kupungua kwa kasi ya Dar es Salaam, ambayo ni kitovu cha biashara, zilianza kuonekana. Baadhi ya bidhaa zikaanza kupungua sokoni, na sauti za wasiwasi zikaanza kuzunguka mitaani.

Watu wakaanza kujipanga. Wengine waliziahirisha safari zao za kurejea Dar es Salaam, wakingoja hali itengemae. Wenye safari za kimataifa walipitia Entebbe, huku wale waliokuwa kwao wakiamua kubaki. Walijiona wako salama kijijini, miongoni mwa wanafamilia wenzao, mahali palipokuwa na utulivu na faraja waliyoihitaji katika kipindi hiki. Walikubali kwamba hali ilikuwa vile ilivyokuwa na wakaamua kuisubiri kwa amani.

Uhalisia wa muunganisho wetu

Tukio hili la kuzimwa kwa mtandao wa intaneti lilitukumbusha jinsi nchi yetu nzima ilivyoshonwa pamoja kwa nyuzi zisizoonekana za mawasiliano na biashara. Dar es Salaam ni kama moyo wa taifa, na kasi yake inapopungua au kusimama, mapigo yake husikika kote nchini. Uhusiano wa bidhaa, taarifa na imani si wa kiuchumi tu bali pia wa kisaikolojia. Mawasiliano yakipungua, biashara nayo hupungua; taarifa zikikosekana, hofu hujaza nafasi yake.

Katika zama hizi za kidijitali, mtandao wa intaneti si anasa tena, ni hewa ya uhai wa uchumi na jamii. Kutoka kwa miamala ya fedha kwa simu, biashara za mtandaoni, utafiti wa kielimu hadi mifumo ya hospitali, mtandao wa intaneti umekuwa uti wa mgongo usioonekana japo unatuunganisha kama Taifa.

Na tukio hili liliufunua udhaifu uliojificha ndani yake, udhaifu wa kutegemea teknolojia bila kujenga njia mbadala na ambazo zinaweza kustahimili kuyumba au kukosekana kwa mtandao wa intaneti, na kuzistahimili changamoto zinazotukabili.

Kurudi uchumi wa fedha taslimu

Wakati mtandao wa intaneti ulipozimika, mifumo ya kibenki nayo ikanyamaza. ATM hazikutoa pesa, programu za benki kwenye simu zikaganda, na miamala ya mtandaoni ikatoweka kana kwamba haijawahi kuwepo. Ndani ya muda mfupi, tulijikuta tumerudi kwenye uchumi wa fedha taslimu, dunia ya noti na sarafu.

Wale waliokuwa na pesa mkononi walijikuta ghafla wakiwa na nguvu mpya, huku wasiokuwa nazo wakikwama katikati ya mahitaji. Biashara zilizokuwa zimezoea malipo ya kidijitali zikaanza kusuasua. Maduka, vibanda vya soko na hata hospitali zikaanza kudai pesa taslimu pekee. Kadri siku zilivyozidi kusonga, baadhi ya bidhaa muhimu zikaanza kupungua sokoni, bei zikapanda na hali ya wasiwasi ikatanda.

Ilikuwa kama tumerejea kwenye enzi za zamani, enzi ambazo kila kitu kilitegemea uwepo wa pesa mkononi. Mfumo wa kidijitali ulipokosekana, thamani ya fedha halisi ilijitokeza tena.

Lakini zaidi ya yote, tukio hili lilifichua pengo kubwa katika uchumi wetu; utegemezi usio na uwiano kati ya teknolojia na uhalisia. Tuligundua kwamba urahisi tulioujenga kidijitali unaweza kupotea ndani ya sekunde chache, na kinachobaki ni uwezo wetu wa kujipanga, kubuni na kustahimili.

Ustahimilivu wetu

Kukatika kwa mtandao wa intaneti kwa siku sita kulikuwa kama jaribio la kitaifa la ustahimilivu wetu. Hali hiyo ilitulazimisha kurudi kuitumia misuli yetu ya zamani ya kuzungumza, kusikiliza, kuandika na kutembea. Tulikumbushwa kwamba teknolojia hutuunganisha, lakini pia hudhihirisha udhaifu wetu pale inapotokea hitilafu kama iliyotokea katika siku hizo sita. Wale waliokuwa na mbinu mbadala, wafanyabiashara waliotunza kumbukumbu kwa kalamu, familia zilizohifadhi pesa taslimu kwa dharura, waliweza kustahimili vizuri zaidi. Lakini kwa wengi, ilikuwa kama kusimama kwa wakati.

Hata hivyo, ndani ya ukimya huo kulizaliwa mwamko mpya. Jamii zilianza kuunganishwa tena kwa mawasiliano ya ana kwa ana.

Niliporejea Dar es Salaam Novemba 3, rafiki yangu alinipatia gari lake ili nifike nyumbani, lakini lilikuwa limeishiwa mafuta na siku hiyo haikuwezekana kununua mafuta. Huo ndio ulikuwa upeo wa utu na ukarimu tulioujifunza upya katika zile siku sita.

Watu walishirikiana katika kupeana taarifa, wakasaidiana kwa shida na raha, huku wakipeana matumaini. Haikuwa rahisi, lakini ilibidi utu na mahusiano ya binadamu vitawale. Tulijikumbusha kwamba uimara haujengwi kwenye kasi pekee, bali kwenye mahusiano pia.

Na kwamba nguvu ya jamii hupimwa si wakati wa utulivu, bali katika uwezo wake wa kusimama pamoja pale mambo yanapoyumba.

Mitikisiko ya kikanda, tafakuri za sera

Kukatika kwa mtandao hakukuwa tukio la ndani pekee; kulikuwa na athari zilizovuka mipaka. Tukio hilo lilifichua udhaifu wa mifumo yetu ya kikanda inayounganishwa na intaneti, kutoka bandari hadi mipaka, kutoka ofisi za forodha hadi kampuni za usafirishaji.

Dar es Salaam, kama kitovu cha biashara cha ukanda, ilipopoteza kasi, mitandao ya biashara ya Afrika Mashariki nayo ikaanza kuyumba. Mizigo ikachelewa, mawasiliano yakapungua na mashaka yakaanza kuingia hata kwenye mnyororo wa imani ya biashara.

Hali hii ilitukumbusha kwamba uchumi wa kikanda ni kama chombo kinachoelea; sehemu moja ikivuja, maji huanza kuingia kote. Tuliona kwa macho yetu jinsi sekta za usafirishaji, fedha, afya na elimu zinavyotegemea uthabiti wa mtandao wa intaneti.

Kwa miaka kadhaa, teknolojia imepanua fursa na ujumuishaji wa kifedha, ikarahisisha biashara na kuboresha maisha. Lakini tukio hili lilitufunza somo moja muhimu, kwamba mageuzi ya kidijitali bila mpango wa dharura yanaweza kuwa na gharama kubwa kuliko tulivyowahi kufikiria.

Hivyo basi, tafakuri ya sera haiwezi tena kujikita kwenye urahisi pekee wa teknolojia, bali kwenye uimara wake. Tunahitaji mifumo yenye njia mbadala, sera zinazolinda mwendelezo wa huduma na mawasiliano ya kikanda yasiyotegemea lango moja pekee.

Muunganisho wa kikanda unapaswa kuwa ishara ya nguvu, si udhaifu.

Kukatika kwa mtandao wa intaneti kwa siku hizo sita hakukuwa tu usumbufu wa kidijitali, bali ulikuwa mwaliko kwetu wa kujitafakari upya. Ulitukumbusha kwamba urahisi na kasi ya kufanya mambo si uimara, bali ni kivuli cha ustawi unaoweza kutoweka ghafla.

Tulijifunza kwamba teknolojia, licha ya kuturahisishia maisha, haiwezi kuchukua nafasi ya mahusiano ya binadamu yanayojengwa kwa mazungumzo, ushirikiano na uaminifu.

Siku hizo sita zilitufundisha thamani ya mawasiliano ya kweli, yale yasiyotegemea skrini wala ishara za mtandao. Zilitukumbusha kwamba uthabiti wa taifa letu hautokani na nguvu ya mitandao, bali na uimara wa watu wake.

Na pengine, zaidi ya yote, zilituonyesha kwamba uimara wa kidijitali unapaswa kwenda sambamba na uimara wa kijamii, kwa sababu kadiri tunavyounganishwa, ndivyo tunavyopaswa kuendelea kuwa na mahusiano zaidi ya kibinadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *