Dar es Salaam. Ukifuatia historia ya nchi hii hata kabla ya ujio wa wakoloni, wanamuziki wamekuwa na nafasi muhimu katika siasa za jamii yetu.

Kiwango cha mchango huo na sababu za mchango zimekuwa zikibadilika katika nyakati tofauti. Kabla ya ujio wa wakoloni, kulikuwako na wasanii wanamuziki katika makabila mengi ambao walikuwa wakiimba na kupiga vyombo vya muziki na kuwa na ukaribu sana na viongozi nyakati hizo.

Wanamuziki  hawa walikuwa ni sauti za wananchi zilizomtaarifu mkuu wa jamii, furaha na masikitiko ya wananchi wake. Na wasanii hao walikuwa wakifanya hivyo kwa uhuru bila kuogopa adhabu toka kwa kiongozi wao, kwani na viongozi walielewa kuwa hiyo ni moja ya njia ya kujua kinachoendelea kwa waliokuwa chini yao. 

Wasanii hawa mara nyingi walifadhiliwa na wakuu wa jamii na hivyo kuwa na nafasi muhimu katika jamii.

Ujio wa wakoloni ulieneza utamaduni wa  kuanzishwa kwa miji. Miji ilikusanya watu kutoka makabila mbalimbali, watu hawa waliungana kwa vile mbaya wao sasa alikuwa mkoloni.

Simulizi zinatuambia kuwa Wajerumani walipenda sana kutumia viboko kuamrisha wazawa, tabia hii na tabia nyingine zilizowadhalilisha na kuwanyima uhuru wazawa zilisababisha wananchi kuanza kutafuta njia za kulalamikia hali hii.

Wanamuziki wakaanza kufanya kazi hii. Wanamuziki walikuja na muziki ulioitwa Beni Ngoma. Muziki huu kwanza uliwaunganisha watu kutoka makabila mbalimbali na ulitumika kwa kuimba mengi yakiwamo maovu ya mkoloni, hata uchezaji wa ngoma yenyewe ilikuwa ni kejeli kwa taratibu za jeshi la Mjerumani.

Ngoma hii ilisambaa sehemu kubwa ya Afrika ya mashariki. Na hata leo baadhi ya ngoma kama Mganda na Malipenenga ni kati ya ngoma ambazo ni mwendelezo wa Beni Ngoma. 
Mwingereza alipomwondoa Mjerumani alikuta wanamuziki wa Beni ngoma wakiwa na nguvu na umoja hata kuweza kufanya mashindano kati ya mji mmoja na mwingine.

Muda si mrefu wakoloni waliishtukia ngoma hii kwa kuona kuwa ilikuwa inawaunganisha wananchi na wanaitumia kupashana taarifa kuhusu namna ya kumpinga mkoloni.

Muingereza aliupiga marufuku muziki huu. Na hata sheria ya kuanza kutoa vibali kwa ajili ya shughuli za sanaa zilianza wakati wa ukoloni chini ya Waingereza.

Wakati zilipopamba harakati za kupigania Uhuru miaka ya 50, muziki ulitumika sana, nchi nzima kulikuwa na wanamuziki wakitunga nyimbo kwa kutumia ngoma za asili na muziki wa dansi na Taarab nyimbo zilitungwa kuhamasisha watu kuungana na kudai Uhuru.

Mwanamuziki Frank Humplick ambaye baba yake alikuwa mzungu kutoka Austria na mama yake Mchaga na alijulikana zaidi kama kijana wa Kichaga aliwahi kutunga wimbo ulioitwa I am a democrat, wimbo huu uliokuwa  ukielezea kishairi mambo yatakavyokuwa Uhuru ukipatikana, ulimchukiza sana mkoloni. 

Amri ilitolewa na santuri za wimbo huu zilisakwa na askari nyumba kwa nyumba na kuvunjwa. Wimbo huu ulikuwa mmoja wa nyimbo zilizotumika kabla ya mikutano aliyokuwa akihutubia Mwalimu Nyerere wakati huo.

Katika mikoa ya kusini wanamuziki kama Mzee Moses Nnauye walianzisha vikundi vya muziki kuhamasisha kudai Uhuru na ujumbe uliwafikia vizuri wananchi wengi.

Desemba 9, 1961 bendi na vikundi vingi vilitunga nyimbo zilizoongelea furaha ya kupata Uhuru na Uhuru na ndoto za  wananchi baada ya uhuru, kauli mbiu wakati huo ikiwa ni Uhuru na Kazi.

Mahusiano ya muziki na siasa yaliongezeka sana baada ya Tanzania kuamua kuwa nchi ya Kijamaa, serikali iliwekeza sana katika sanaa, hasa baada ya hotuba ya Mwalimu Nyerere mwaka 1962 alipoanzisha Wizara ya Utamaduni.

Kulikuweko na Maofisa Utamaduni wa Wilaya na Mkoa kila mkoa na bajeti yao ilitoka serikali kuu, maofisa utamaduni wakahamasisha kuanzishwa vikundi vya muziki wa aina mbalimbali mpaka vijijini.

Mashirika ya umma yalihamasishwa kuanzisha vikundi vya sanaa, na ndipo kukawepo kundi la sanaa la Taifa, vikundi vya sanaa majeshini ambapo huko pia kukawa na vikundi vya taarab na dansi, mashirika kama Bima, DDC, URAFIKI na mengine mengi yakawa na vikundi vya sanaa.

Kurugenzi za mikoa Dodoma na Arusha nazo zikaanzisha vikundi, bila kusahau Women Jazz Band na baadaye Umoja wa Vijana wa TANU nao ukawa na bendi yake maarufu Vijana Jazz band. 

Vikundi vyote hivyo vilishiriki sana katika kuimba nyimbo mbalimbali za kizalendo na maendeleo. Pamoja na bendi na vikundi vya taarabu, wasanii maarufu walikuja kupatikana akina Mzee makongoro, Mzee Mwinamila, John Komba na kadhalika. 

Zama hizi ziko tofauti sana, umuhimu wa sanaa katika kuhamasisha uzalendo umepotea kabisa. Katika wiki hii, ambayo hakika haitafutika katika historia ya nchi yetu, ghafla kumesikika nyimbo mbalimbali na nzuri sana ambazo zinahamasisha uzalendo. 

Nyimbo hizo si mpya, kumbe zilikuwa hazipigwi tu, kuna haja ya vyombo vya utangazaji na jamii nzima kwa ujumla kujiuliza kuhusu nafasi yake katika kuhamasisha uzalendo kwa kutumia kazi za sanaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *