Chanzo cha picha, Reuters
-
- Author, Osmond Chia
- Nafasi, Mwandishi masuala ya biashara, BBC News
Mkutano wa Jumatatu wiki hii kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin, Rais wa China Xi Jinping, na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi uliashiria mshikamano wa nadra –na ulikuwa fursa mahsusi kwa Putin kuwasiliana moja kwa moja na wanunuzi wakubwa wa mafuta ya Urusi.
India na China zilivutiwa na mafuta ya Urusi baada ya bei kushuka wakati mataifa ya Magharibi kukata mahusiano ya kibiashara na Moscow kufuatia uvamizi wa Ukraine mwaka 2022.
Hata hivyo, uhusiano kati ya Beijing, New Delhi na Moscow sasa umejikita zaidi ya biashara ya mafuta.
Mataifa haya matatu sasa yanakutana kwenye msingi wa msimamo wa pamoja dhidi ya Marekani ambayo imeiwekea Urusi vikwazo vikubwa vya kiuchumi na kutoza ushuru mkubwa kwa washirika wake wa kibiashara.
India, kwa mfano, imeathiriwa na ushuru wa juu uliowekwa na Washington kama adhabu kwa ununuzi wa mafuta kutoka Urusi.
Wakati huohuo, China bado inashughulikia makubaliano ya kuepuka ushuru unaoweza kuathiri uchumi wake na vikwazo vinavyotokana na ununuzi huo wa mafuta yasiosafishwa ya Urusi.
Viongozi hao watatu walikutana katika jiji la Tianjin, katika mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO), jukwaa la kikanda linalotafuta kutoa mbadala wa mtazamo wa mataifa ya Magharibi.
Kwa mujibu wa wachambuzi, SCO ni jukwaa litakalochochea changamoto dhidi ya ushawishi wa Marekani.
Wachambuzi waliiambia BBC kuwa jukwaa hili linatoa fursa nadra kwa viongozi hao kuimarisha ushirikiano wao katika kipindi hiki kinachoendelea cha mabadiliko na mashaka ya kiuchumi.
Kitega uchumi cha Urusi
Kwa Urusi, huu ni wakati wa kuimarisha biashara na India na China ambao ni washirika wake wakuu wa kibiashara.
India na China, nchi mbili zenye idadi kubwa ya watu duniani zimekuwa nguzo muhimu kwa uchumi wa Urusi, hasa baada ya kuwekewa vikwazo na mataifa ya Magharibi.
Mwaka 2024, China ilinunua rekodi ya zaidi ya tani milioni 100 za mafuta ghafi kutoka Urusi karibu asilimia 20 ya uagizaji wake wa nishati.
Kwa upande mwingine, India ambayo hapo awali ilikuwa mnunuzi mdogo wa mafuta ya Kirusi, sasa imeongeza ununuzi wake hadi kufikia takriban dola bilioni 140 tangu 2022.
Kwa pamoja, China na India sasa zinachukua sehemu kubwa ya mauzo ya nishati kutoka Urusi.
Kwa taifa linalotegemea mafuta na gesi kwa takriban asilimia 25 ya mapato ya bajeti yake, biashara hii ni muhimu sana kwa Urusi, hasa katika kufadhili matumizi yake ya kijeshi.
Mtaalamu wa sera za umma, Profesa Mandar Oak, aliambia BBC kuwa haitashangaza ikiwa Moscow itaendelea kutoa punguzo la bei ili kuhakikisha inaendelea kuuza kwa India na China.
Kwa India hasa, hili ni muhimu ili kuhimili shinikizo la Marekani.
India ilitoa mwanya kwa Urusi baada ya mataifa ya Magharibi kukata ununuzi wa mafuta.
Delhi ilinufaika kwa kupata nishati kwa gharama nafuu, na huenda ikaongeza ununuzi zaidi licha ya lawama kutoka Washington.
Katika mkutano huo, Modi alithibitisha ushirikiano na Moscow kwa kusema kuwa nchi hizo “zimekuwa bega kwa bega katika safari yao.”
Maafisa wa serikali ya India pia wamesisitiza kuwa nchi yao itanunua nishati kutoka kwa yeyote atakayetoa masharti bora zaidi ya bei.
Uhusiano kati ya Delhi na Washington ulifikia kiwango kibaya zaidi wakati utawala wa Donald Trump, ambapo Marekani iliweka ushuru wa ziada wa asilimia 25 kama adhabu kwa India kununua mafuta ya Urusi.
Delhi iliitaja hatua hiyo kuwa “isiyo ya haki”, ikikumbusha historia ya muda mrefu ya ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.
Chanzo cha picha, Reuters
Faida za kisiasa kwa Waziri Mkuu Modi
Kwa Waziri Mkuu Modi, msimamo huo wa kukataa shinikizo la Marekani unaonekana kuwa wa kisiasa nyumbani.
“Kisiasa, inamnufaisha Modi kukiuka msimamo wa Marekani, kwani inaonyesha kuwa India haiwezi kulazimishwa,” alisema Profesa Oak.
Kununua mafuta zaidi kutoka Urusi ni afueni kiuchumi kwani India inategemea sana wasambazaji wa kigeni kwa mafuta ghafi.
India, ambayo kwa muda mrefu ilikuwa mnunuzi mkubwa wa mafuta kutoka Mashariki ya Kati, ilibadili mwelekeo wake na kuanza kuagiza mafuta kutoka Urusi kufuatia vikwazo vya Magharibi mwaka 2022.
Kwa sasa, wasindikaji wa mafuta nchini India wananufaika na gharama ndogo kutokana na mafuta ya bei nafuu kutoka Urusi, ambayo ni nafuu zaidi kuliko yale ya Mashariki ya Kati.
China, ambayo pia imeongeza ununuzi wa mafuta kutoka Urusi, inatarajiwa kulinda maslahi yake ya nishati wakati viongozi wanapokutana kwenye mkutano wa SCO, kwa mujibu wa mtaalamu wa sera za biashara Peter Draper.
Jumanne, kampuni za gesi za Kirusi na Kichina zilitia saini makubaliano ya kuongeza usambazaji wa gesi kwa China.
Hata hivyo, Draper anasema huenda Urusi isitoe punguzo kubwa kwa China kama Putin ataweza kupata wateja zaidi kutoka India.
Chanzo cha picha, Reuters
Malengo ya kisiasa ya China na mtazamo mpya wa Dunia
Mbali na masuala ya biashara, huenda lengo kuu la China katika mkutano huu ni kuonyesha kuwa inaweza kuwa mbadala dhabiti wa Marekani, hasa baada ya sera za karibuni za Trump dhidi ya nchi washirika.
China imesimama pamoja na mataifa kama Pakistan, Myanmar na Sri Lanka, yote yakiwa yameathiriwa na ushuru wa Marekani.
Kwa muda mrefu, China imekuwa ikipigia debe mtazamo wa dunia wa madola mengi (multi-polar world) mfumo ambapo mamlaka ya kiulimwengu yanasambazwa miongoni mwa mataifa kadhaa yenye nguvu.
Prof. Oak anasema mkutano huo umezikutanisha nchi tatu ambazo uhusiano wao wa kiuchumi hapo awali ulitatizwa na mvutano wa kisiasa, lakini sasa,
“Kufuatia tishio la kiuchumi kutokana na sera za ushuru wa Marekani, nchi hizi zina sababu thabiti za kushikamana kiuchumi,”anasema Prof. Oak.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi