Chanzo cha picha, Raees Hussain / BBC, Getty
-
- Author, Cagil Kasapoglu
- Nafasi, BBC World Service
Kati ya Lithuania na Poland kuna mkanda mdogo wa ardhi unaojulikana kama Suwałki Gap, ambao mara nyingi hufafanuliwa na wachambuzi wa kijeshi kuwa ndio eneo dhaifu zaidi la NATO maarufu pia kama “eneo la hatari”.
Iwapo mzozo wa kijeshi ungefumuka kati ya NATO na Urusi, ushoroba huu mwembamba ungewakilisha kitovu cha mivutano ya kijeshi.
Wasiwasi mkubwa ni kwamba iwapo Urusi, kwa kushirikiana na mshirika wake Belarusi, ingeuteka au kuufunga ushoroba huu, ingeweza kuyatenga mataifa ya Baltiki – Lithuania, Latvia na Estonia – kutoka kwa washirika wao wa NATO barani Ulaya.
Mnamo Juni 2025, Mkuu wa Majeshi wa Ujerumani, Jenerali Carsten Breuer, aliwaambia waandishi wa habari wa BBC kuwa nchi wanachama wa NATO lazima zijiandae kwa uwezekano wa shambulio la Urusi ndani ya kipindi cha miaka minne ijayo.
Aidha, alieleza kuwa Urusi imekuwa ikiunda mamia ya mizinga kila mwaka, na mingine inaweza kutumika kushambulia upande wa mashariki wa NATO ifikapo mwaka 2029 au hata mapema zaidi.
Jenerali Breuer alilitaja Suwałki Gap kama mojawapo ya maeneo ya kimkakati yaliyo hatarini zaidi barani Ulaya.
Suwałki Gap ni nini?

Suwałki Gap ni ukanda wa ardhi wa urefu wa takribani kilomita 65, unaotenganisha wanachama wawili wa NATO Poland na Lithuania na ambao unaiunganisha Ulaya Magharibi na mataifa ya Baltiki.
Aidha, njia hii inagawanya mshirika wa Urusi, Belarusi, na eneo la Kaliningrad ambayo ni sehemu ya Urusi yenye ulinzi mkubwa lakini iliyozungukwa na nchi za NATO.
Hii ndiyo njia pekee ya ardhi inayowezesha vikosi vya NATO kuifikia Lithuania, Latvia na Estonia.
Mataifa haya matatu yanachukuliwa kama “tumbo laini” la NATO katika ukanda wa Baltiki kwa kuwa yana uwezo mdogo wa kijeshi ikilinganishwa na mataifa mengine ya muungano.
Kwa upande mmoja wa Suwałki Gap iko Lithuania, na upande wa pili iko Poland.
Eneo hili linaitenga Kaliningrad na Urusi pamoja na mshirika wake Belarusi.
Mikey Kay, mtangazaji wa kipindi cha BBC Security Brief na mwanamikakati wa kijeshi ambaye pia aliwahi kuwa rubani wa helikopta wa Jeshi la Uingereza, anaeleza:
“Kwa sasa, Kaliningrad inaunganishwa na Urusi kwa njia ya anga pekee kupitia Ghuba ya Finland hadi St Petersburg. Kwa hivyo, Suwałki Gap ndiyo njia fupi zaidi ya kuunda njia ya ardhi kati ya Kaliningrad na Belarusi.”
Wachambuzi wengi wanaonya kuwa Urusi inaweza kulitumia eneo hili kuwatenga wanachama wa NATO katika Baltiki kwa njia ya ardhi na kisha kuanzisha mzingiro wa baharini.
Hata hivyo, mandhari ya eneo hilo misitu minene, vilima na maziwa hutoa faida kwa vikosi vya ulinzi kuliko vikosi vya uvamizi, jambo linalozuia operesheni kubwa za kijeshi kufanikiwa kwa urahisi.
‘Mikondo ya maslahi ya kijeshi ya NATO na Urusi hukutana hapa
Chanzo cha picha, Sean Gallup/Getty Images
Umuhimu wa Suwałki Gap unatokana na nafasi yake ya kimkakati.
Profesa Dariusz Kozerawski, kutoka Idara ya Usalama wa Taifa katika Chuo Kikuu cha Jagiellonian, Poland, anasema:
“Hili ni eneo nyeti, lililo katika makutano ya masilahi ya kimkakati ya NATO na Urusi.”
“Umuhimu wake unatokana na hatari ya kutekwa na vikosi vya Urusi, hali ambayo inaweza kuyakatiza mataifa ya Baltiki (Lithuania, Latvia na Estonia) kutoka kwenye msaada wa nchi wanachama wa NATO.”
Tangu mwaka 2015, baada ya Urusi kuivamia Crimea, wasiwasi kuhusu Suwałki Gap uliongezeka.
Luteni Jenerali Ben Hodges, kamanda wa zamani wa Jeshi la Marekani Ulaya, alilionya Pentagon kuhusu hatari za eneo hili, akitaja ongezeko la mazoezi ya kijeshi ya ghafla kutoka kwa Urusi.
Katika ripoti ya mwaka 2018 iliyobeba kichwa: “Securing the Suwałki Corridor: Strategy, Statecraft, Deterrence and Defence”, Hodges alilitambua Suwałki Gap kama eneo tete na kupendekeza hatua madhubuti za kuimarisha uwezo wa NATO katika ukanda huo.
Kwa taifa la Poland, Suwałki Gap lina umuhimu wa kiuchumi, kisiasa na kijeshi.
“Ni njia kuu ya biashara kati ya Poland na mataifa ya Baltiki, kupitia barabara na reli zilizoendelezwa,” asema Profesa Kozerawski.
Kijeshi, eneo hili lina maana kubwa kwa uhamishaji wa vikosi, silaha na vifaa.
“Katika kipindi cha amani, linawezesha usafirishaji wa wanajeshi na vifaa vyao kwenda Lithuania, Latvia na Estonia, huku vikosi vya NATO vikiwa vinahudumu kwa zamu. Pia hutoa fursa ya mafunzo ya pamoja na mazoezi ya kimataifa,” anafafanua.
“Wakati wa mgogoro au vita, udhibiti wa Suwałki Gap utakuwa muhimu kwa utoaji wa msaada wa kijeshi na kibinadamu kwa mataifa ya Baltiki.”
Jinsi nchi za kanda zimechukua hatua za kujihami
Chanzo cha picha, Sean Gallup/Getty Images
Lithuania, Latvia na Estonia zimeanza kuimarisha ulinzi kwenye mpaka wao wa mashariki, ambao ni sehemu dhaifu zaidi ya NATO.
Mnamo Januari 2024, walitangaza mpango wa pamoja unaoitwa “Baltic Defence Line Initiative”, unaojumuisha ujenzi wa mahandaki ya kuzuia magari ya kivita (vifaru).
Kwa upande wake, Poland ilizindua mpango wake wa “East Shield”, unaolenga kuimarisha mpaka wa mashariki unaopakana na Belarusi na Kaliningrad.
Ujenzi wa vizuizi, uzio na miundombinu ya kijeshi ulianza Novemba 2024 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2028.
Mnamo Aprili 2025, Bunge la Ulaya lilipitisha azimio la kuutambua East Shield na Baltic Defence Line kama miradi ya kielelezo ya usalama wa pamoja wa bara Ulaya.
Isitoshe, Poland inatarajia kutumia asilimia 4.7 ya pato la taifa kwa ulinzi mwaka huu ambacho ni kiwango cha juu zaidi miongoni mwa wanachama wa NATO.
Lithuania pia itaongeza bajeti ya ulinzi kutoka asilimia 3 hadi 5 kati ya mwaka 2026 hadi 2030.
Finland, Poland na mataifa ya Baltiki tayari yamejiondoa au yametangaza nia ya kujiondoa kwenye Mkataba wa Ottawa unaopiga marufuku matumizi ya mabomu ya ardhini yanayolenga watu, wakihofia tishio linaloongezeka kutoka taifa jirani Urusi.
Prof. Kozerawski anasisitiza haja ya kuimarisha ulinzi zaidi:
“Ili kudumisha uwezo wa kijeshi wa NATO upande wa mashariki, hasa katika eneo la Suwałki Gap, ni muhimu kuandaa mazoezi ya mara kwa mara ya mataifa wanachama kwa kiwango kikubwa.”
Hivi sasa, mazoezi makubwa ya kijeshi ya NATO hayafanyiki mara kwa mara katika eneo hili, jambo linalozua wasiwasi kwa wataalamu wa usalama.
Je, Urusi itachukua hatua wakati vita vya Ukraine vitakapokwisha?
Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images
Wachambuzi wanaamini kuwa Urusi bado ni tishio kwa usalama wa NATO, lakini uwezekano wa mashambulizi ya moja kwa moja kwa sasa ni mdogo kutokana na muendelezo wa vita vya Ukraine.
“Urusi ina malengo ya fujo dhidi ya upande wa kaskazini-mashariki wa Nato,” anasema Justyna Gotkowska, Naibu Mkurugenzi katika Kituo cha Mafunzo ya Mashariki (OSW) na mkuu wa Idara ya Usalama na Ulinzi.
“Kadiri vita vya Ukraine vikiendelea, uwezekano wa Urusi kushambulia mataifa ya Baltic, Poland, Finland, Sweden, nchi nyingine za Ulaya bado uko chini,” anaongeza.
“Lakini ikiwa tutakuwa na mwisho wa vita vya Ukraine kwa niaba ya Urusi, Urusi inaweza kuwa tayari kutoa changamoto kwa nchi za Nato hapa katika eneo letu na kuanza mashambulizi ya kawaida ya silaha kwa mataifa ya Baltic huko Poland, Finland na nchi nyingine katika kanda.”
Lakini kulingana na shirika la utangazaji la Ukraine TSN na tovuti ya uchambuzi wa kijeshi ya Tochnyi, picha za setilaiti zinaonyesha kuwa Urusi inaunda kituo cha kijasusi cha mawimbi makubwa (SIGINT) katika eneo lake la Kaliningrad ili kupanua uwezo wa ufuatiliaji wa kielektroniki karibu na ubavu wa mashariki wa Nato.
“Kutoka kwa tovuti hii, Urusi itaweza kufuatilia usambazaji wa mbinu, mitandao ya rada na hata vipengele vya miundombinu ya kiraia katika muungano,” Tochnyi aliripoti mnamo Agosti 2025.
Wakati huo huo, Belarus na Urusi zinaendelea kufanya mazoezi ya kijeshi kwenye mpaka.
Nchi zote mbili zimeripotiwa kupanga kuzindua mazoezi mapya, Zapad-2025 mwezi Septemba.
Mikey Kay anaonya kwamba mazoezi kama haya yanaweza kuzuia ujenzi wa kijeshi, kama inavyoonekana kabla ya kunyakuliwa kwa Crimea mnamo 2014 na uvamizi wa Ukraine mnamo 2022.
“Putin ameweka kielelezo kupitia oparesheni hizi zinazodhaniwa kuwa za mafunzo ili kujenga uwezo wa kijeshi na kisha kuchukua hatua kwa ukali juu ya hilo,” anasema.
Mikey Kay, pia anazua swali kuhusu jinsi Marekani inaweza kujibu vitisho vinavyoongezeka katika eneo hilo:
“Kwa nini kuna mvutano mkubwa na wasiwasi mkubwa ndani ya jumuiya, ndani ya Mataifa ya Baltic? Ni kwa sababu kuna ukosefu wa imani kwamba Marekani ingeunga mkono jibu lolote chini ya Nato kwa uchokozi wowote wa Putin,” Kay anasema.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi