Arumeru. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura kuondoa tamko la kumtafuta Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na badala yake wamwache ajitokeze aendelee na ibada zake ili wajenge umoja wa kitaifa.
Hatua hiyo inakuja siku saba baada ya Dk Mwigulu kuagiza kufunguliwa kwa kanisa hilo, Novemba 24, 2025 ambapo alielekeza lipewe miezi sita ya uangalizi kuhusu kuzingatia miiko, masharti na sheria za uendeshwaji wake.
Agizo hilo la Serikali la kufunguliwa kwa kanisa hilo, lilikuja ikiwa zimepita siku 175 tangu Juni 2, 2025, tangu ilipotangaza kufuta usajili wa kanisa hilo kwa kile ilichoeleza limekiuka masharti ya sheria, kwa madai ya kujihusisha na masuala ya siasa.
Dk Mwigulu ametoa maagizo hayo leo Jumapili Novemba 30, 2025 alipozungumza katika mkutano wa hadhara viwanja vya Magufuli, Leganga wilayani Arumeru, baada ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na vurugu za Oktoba 29, 2025.
Amesema ibada ni ushirika kati ya Mungu na wanadamu na kuwa kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alisamehe vijana ambao walionekana wamepita kwenye mkumbo bila kujua kilichofanyika, akaelekeza msamaha na kwenye taasisi za kidini.
“Nilishasema kanisa lifunguliwe najua pale kanisani watakuwa wanasema kanisa limefunguliwa sasa baba yetu yuko wapi. Kwa kuwa baba yao hajawahi kukamatwa na polisi walitoa tamko wanamtafuta inawezekana alipo akaogopa kutoka kwa kuhofia polisi wanamtafuta.”
“Nitamke leo IGP pamoja na Jeshi la Polisi ile mliyokuwa mnasema mnamtafuta Askofu Gwajima iacheni, muacheni aendelee na ibada zake, mwacheni ajitokeze tujenge umoja wa kitaifa, tushikamane kurudisha umoja wa kitaifa,” amesema Askofu Dk Mwigulu.
Novemba 7, 2025, Jeshi la Polisi nchini lilitangaza majina ya watu 10 wanaosakwa kufuatia matukio ya vurugu, uporaji na uvunjifu wa amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025. Miongoni mwa watu hao ni Askofu Gwajima.
Mbali na Askofu Gwajima, wengine ni viongozi wa Chadema wakiwemo Brenda Jonas Rupia, John Mnyika, Godbless Jonathan Lema, Achumu Maximillian Kadutu, Deogratius Mahinyila, Boniface Jacob, Hilda Newton, Award Kalonga na Amaan Golugwa.
Baadhi waliliripoti Polisi, wakafanyiwa mahojiano na kuachiwa, lakini Askofu Gwajima hakuwahi kwenda.
Katika maelezo yake, Dk Mwigulu amesema: “Tumeongea na wenzetu wa TEC (Baraza la Maaskofu Katoliki), tulikutana kirafiki tukaongea, tumekutana na wengine tumekubaliana na hapa nitumie jukwaa hili kuwaomba viongozi wote wa dini, mila na makundi mbalimbali twendeni sote kwenye jambo hili wala tusifanye kwa uficho tujitokeze tuhamasishe Tanzania ya amani tusirudishe tena Tanzania kwenye historia ambayo haijawahi kuwepo.”
“Huu ndio wito wa kiongozi wetu mkuu wa nchi, tuongee kama Watanzania, turudishe umoja wa kitaifa sote twendeni tuambizane kwenye ibada, tukienda kwa njia hii tuliyotaka kuifuata hakuna atakayeshinda tutapoteza Taifa hakutakuwepo na mshindi,” amesema.
Mganga kubaka mgonjwa Tabora
Wakati huohuo, Dk Mwigulu amemwagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi, kumsimamisha kazi mganga mmoja mkoani Tabora, anayedaiwa kumchoma mgonjwa sindano ya usingizi kisha kumbaka.
Aidha amesema Serikali haitasita kumchukulia hatua za kisheria na kinidhamu mtumishi wa umma anayekiuka maadili, wazembe, wavivu, wala rushwa na wale wanaopiga danadana kushughulikia kero za wananchi.
Amesema watumishi walio wema wasiwe na wasiwasi ila walio wazembe, wavivu, wala rushwa, wanaopiga danadana wakishirikishwa kero za wananchi. Amefafanua kuwa ameshatoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa kote nchini kufuatilia utatuzi wa kero za wananchi.
“Mtumishi wa umma ambaye atakiuka mambo ya maadili, nidhamu kazini, kusikiliza kero na kutotatua kero, lugha mbaya na mengine wala asihamishwe afukuzwe, Watanzania wako wengi vijana wako wengi hatuna uhaba wa vijana wenye maadili,”
“Leo nimepata taarifa kule Urambo, Tabora jambo la ajabu kabisa na niwapongeze uongozi wa Mkoa wa Tabora kuanzia Mkuu wa Mkoa kwa kuchukua hatua, wasingeliona hili na kuchukua hatua ningewafukuza wao leo.
“Alikuwepo mganga mmoja pale Urambo, ameenda kumtibu binti wa miaka 18 ana tatizo la uzazi, amemaliza kumsikiliza amemdanganya anatakiwa kutibiwa kwa kuchomwa sindano ya usingizi, akiwa kwenye sindano ya usingizi amembaka. Mambo ya ajabu kabisa amembaka.”
“Mungu ni mwema dawa ya usingizi ikaisha, hajamwekea hiyo dawa, binti kaamka kaona, nesi aliyekuwa anasaidia ameona, yule binti ameolewa na mume wake alikuwepo, mambo ya ajabu kabisa, madaktari wamejiridhisha kwamba mgonjwa amebakwa,” amesema.
Dk Mwigulu amesema mganga huyo asiachiwe na afukuzwe kazi leo na kama alisoma kwa mkopo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ifuatilie ili fedha hizo zirudi.
“Hatuwezi Watanzania wakatoa kodi yao kusomesha mtu akamfanyia mwenzake unyama wa namna hiyo na madaktari wafuatilie afutiwe leseni na kwenye jambo hili maabara zingine zisijaribu kucheza nalo ule utaratibu wa zamani tuliokuwa tunaambiwa zinakamatwa dawa uchunguzi unakuja kueleza ni unga wa muhogo, wasijaribu kwenye jambo hili.”
“Nayasema haya na nawapongeza uongozi wa mkoa kwa kuliona, Katibu Mkuu chukua hatua haraka afukuzwe na hizi taasisi zingine wachunguze na kufuatilia. Hatuwezi kuruhusu mambo ya ajabu ya aina hii katika utumishi wa umma ndiyo maana tunasema watumishi wa umma walio wema wasihangaike, acha tuhangaike na wanaochafua na kugombanisha Serikali na Watanzania,” amesema.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla amesema Serikali imejipanga kuhakikisha vyombo vya ulinzi na usalama vinatimiza jukumu la kwanza kulinda raia na mali zao, na kuwahakikishia kuwa vurugu hazitokei tena mkoani humo.