Halmashauri ya Jiji la Tehran imezindua rasmi kituo kipya cha metro (treni ya chini ya ardhi) kinachoitwa Maryam-e Moqaddas , yaani Maria Mtakatifu , kama ishara ya kuonyesha maelewano na kuishi kwa amani baina ya dini mbalimbali nchini humo.

Jengo hilo limepambwa kwa sanaa na usanifu wenye maudhui ya Kikristo na liko karibu na Kanisa Kuu la Mtakatifu Sarkis, kitovu cha jumuiya ya Wakristo wa dhehebu la Kiarmenia jijini Tehran. Kituo cha Maria Mtakatifu kilizinduliwa katika hafla iliyohudhuriwa na Meya wa Tehran, wageni wa kimataifa wakiwemo mabalozi, na maaskofu wa makundi ya kidini wachache, hususan wafuasi wa dhehebu la Kiarmenia

Kituo hiki ni sehemu ya Laini ya 6 ya Reli ya Metro 6, kikiwa katika makutano ya Barabara ya Nejatollahi na Karim Khan Zand, karibu na Kanisa la Mtakatifu Sarkis. Kimejengwa kwa kina cha mita 34 chini ya ardhi, na kina eneo la takribani mita za mraba 11,000.

Meneja wa mradi wa Laini ya 6, Abbas Fathalipour, alisema kuwa kazi ya kwanza ya sanaa iliyowekwa ndani ya kituo ni bango lenye maandishi “Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu” kwa lugha ya Kifarsi, Kiingereza, Kiarabu na Kiameni.

Aidha, kituo hicho kimepambwa na kazi za sanaa zenye nukuu za Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatulah Seyyed Ali Khamenei na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu Imam Khomeini wakimsifu Maria Mtakatifu (SA) na Nabii Isa Masihi yaani Yesu (AS). Halikadhalika katika aya kuta zake kuna aya za Qur’ani Tukufu za  Surah Maryam kuhusu kuzaliwa kwa Nabii Isa (AS.). Aidha kuna mistari ya Injili (aya ya 28 hadi 31) iliyowekwa kwa lugha ya Kiarmeni, Kiasiria na Kifarsi.

Fathalipour aliongeza kuwa kazi nyingine ya sanaa inaonyesha Nabii Isa (A.S.) akitembea juu ya maji, na sehemu nyingine ikimwonyesha Maria Mtakatifu (A.S.) akiwa katika hali ya dua, pamoja na Roho Mtakatifu aliyechorwa kama njiwa, akifuatana na matawi ya mizabibu.

Kituo hiki, alisema, kinamkumbusha mwanamke mtakatifu aliyeamsha ulimwengu kwa usafi wake na kwa kulea nabii mkubwa. Lengo la kulipa jina hilo ni kumheshimu Maria Mtakatifu na kuonyesha maelewano ya dini za Mwenyezi Mungu jijini Tehran.

Ni ishara ya maelewano ya kidini na kwamba Wakristo, Wayahudi na Wazoroastria wanalindwa kikatiba na wanaishi kwa amani katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, huku viti vya bunge vikitengwa kwa kila kundi. Hata mtandao wa treni ya chini ya ardhi jijini Tehran unabeba ujumbe huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *