Wachezaji wa kandanda wa Kipalestina, vilabu na mashirika ya kimataifa wanapanga kuwasilisha malalamiko katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) dhidi ya wakuu wa mashirikisho ya kandanda duniani, FIFA na UEFA, kwa msingi kuwa wamehusika katika kusaidia uhalifu wa vita na mfumo wa ubaguzi wa rangi wa utawala haramu wa Israel.

Ripoti za hivi karibuni zinasema kesi hiyo inalenga namna marais wa Shirikisho la Soka Duniani, FIFA, Gianni Infantino na Shirikisho la  Soka Ulaya, UEFA , Aleksander Ceferin walivyoendelea kuruhusu vilabu vya kandanda kuendeleza michezo ndani ya vitongoji haramu vilivyojengwa na Israel, licha ya onyo kutoka kwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu.

Jumuiya ya kimataifa inatambua hatua ya Israel kujenga vitongozi hivyo vya walowezi wa Kizayuni kuwa ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Mikataba ya Geneva, kwa sababu vimejengwa katika ardhi ya Palestina iliyokaliwa kwa mabavu.

Mbali na ujenzi wa vitongoji hivyo haramuy, Israel imeua takribani Wapalestina 70,100—wengi wao wakiwa wanawake na watoto—tangu Oktoba 7, 2023, ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Ingawa Israel ililazimika kukubali kusitisha mapigano ya Gaza kuanzia Oktoba 10, 2025, imeendelea kukiuka makubaliano hayo kwa mashambulizi ya karibu kila siku dhidi ya eneo hilo lililozingirwa.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Serikali ya Gaza, angalau watu 894 waliokuwa wakijihusisha na michezo—wakiwemo wachezaji, makocha, waamuzi na viongozi wa vilabu—wameuawa katika mashambulizi hayo ya Israel. Zaidi ya 400 kati ya wahanga hao ni wachezaji wa kandanda.

Mashambulizi ya Israel pia yameharibu kabisa au kwa sehemu vituo 292 vya michezo ya Palestina, viwanja vya kandanda, kumbi za mazoezi na vilabu vya vijana katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Mwezi uliopita, mshauri mkuu wa kisheria wa Shirikisho la Kandanda la Palestina (PFA) alisema wakuu wa FIFA na UEFA wamekuwa wakikiuka kanuni na wajibu wao kwa kukataa kuifukuza Israel kutoka mashindano ya kimataifa, licha ya ushahidi unaoongezeka wa mauaji ya halaiki uliothibitishwa na taasisi za kimataifa zenye heshima.

Akizungumza na Shirika la Habari la Anadolu la Uturuki, Kat Vilarev alisema Infantino na Ceferin “walichagua kupuuza” ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na Israel.

Vilarev aliongeza: “Kwa kuzingatia ushiriki wa taasisi za michezo za Israel katika mauaji ya kimbari ya Gaza, FIFA na UEFA kisheria wanalazimika kuchukua hatua. Katiba zao, sera za haki za binadamu na kanuni za nidhamu zinawataka kuzingatia mwongozo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Binadamu.”

Aidha, alisema wanamichezo wengi wa Israel ni askari ambao hadharani wamekuwa wakitoa wito wa kuangamiza Gaza. Alibainisha kuwa vilabu na mashirikisho vya Israel vinaunga mkono waziwazi vikosi vya uvamizi na hata kuandaa mechi katika ardhi ya Palestina iliyokaliwa kwa mabavu—kitendo kinachosaidia moja kwa moja makazi haramu na ukaliaji wa mabavu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *