Washambuliaji wenye silaha wamewateka nyara wanawake 13 na mtoto mchanga katika hujuma mpya ya uvamizi uliofanywa usiku wa kuamkia jana Jumapili kaskazini mashariki mwa Nigeria, ukiwa ni mwendelezo wa matukio ya hivi karibuni ya utekaji nyara mkubwa unaoshuhudiwa katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Kwa mujibu wa shuhuda mmoja, bibi harusi na wapambe wake 10 walikuwa miongoni mwa watu waliotekwa nyara katika kijiji cha Chacho kilichoko kwenye Jimbo la Sokoto.

Aliyu Abdullahi, mkazi wa kijiji hicho cha Chacho amevieleza vyombo vya habari: “majambazi walivamia kijiji chetu jana usiku na kuwateka nyara watu 14, wakiwemo bibi harusi na wapambe wake wa kikwe 10, kutoka nyumba moja jirani na Zango”. 

Abdullahi ameongeza kuwa, mtoto mchanga, mama wa mtoto na mwanamke mwingine nao pia walitekwa nyara katika uvamizi huo.

Kwa mujibu wa shuhuda huyo, mnamo mwezi Oktoba pia, kijiji cha Chacho kilivamiwa na majambazi waliowateka nyara watu 13.

“Tulilazimika kulipa fidia ili kupata uhuru wao. Sasa, tunakabiliwa na hali hiyo hiyo,” ameeleza mkazi huyo.

Ripoti ya vyombo vya intelijensia vya Nigeria imethibitisha kujiri kwa shambulio hilo.

Ripoti hiyo imesema: “Sokoto imeshuhudia ongezeko kubwa la utekaji nyara ulioanzishwa na majambazi mwezi Novemba, na kufikia idadi kubwa zaidi ya mashambulizi kama hayo kwa mwaka uliopita”.

Wiki iliyopita, washambuliaji waliwateka nyara wanafunzi 25 katika Jimbo la Kebbi na zaidi ya 300 katika Jimbo la Niger. Wale waliotekwa nyara kutoka Kebbi waliokolewa na kuunganishwa na wazazi wao, huku msako ukiendelea kuwatafuta wengine waliosalia.

Wimbi la utekaji nyara limezidisha mashinikizo kwa serikali ya Nigeria, ambapo siku ya Jumatano iliyopita Rais Bola Tinubu alitangaza hali ya hatari nchini…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *