Takwimu mpya zilizotolewa kwenye ripoti ya Tasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ya Stockholm (SIPRI) zinaoneysha kuwa, mapato yanayotokana na mauzo ya silaha na huduma za kijeshi ya makampuni 100 makubwa zaidi ya uundaji silaha duniani yalifikia rekodi ya dola bilioni 679 mwaka 2024,

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa leo, vita vya Ghaza na Ukraine, pamoja na mivutano ya kijiopolitiki ya kikanda na kimataifa na matumizi ya juu ya kijeshi yaliongeza mapato yanayopata makampuni yanayouza bidhaa na huduma za kijeshi kwa wateja wa ndani na nje ya nchi kwa asilimia 5.9 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.

Sehemu kubwa ya ongezeko la kimataifa imehusishwa na makampuni yaliyoko Ulaya na Marekani, ambapo makampuni ya uundaji silaha ya Lockheed Martin, Northrop Grumman na General Dynamics yaliongoza kundi hilo kwa upande wa nchini Marekani.

Ripoti ya SIPRI imeendelea kueleza kuwa, mapato ya pamoja ya silaha ya makampuni ya silaha yaliyoko kwenye orodha ya 100 bora yalikua kwa asilimia 3.8 mwaka 2024 na kufikia dola bilioni 334, huku makampuni 30 kati ya 39 ya Marekani yakiwa kwenye orodha ya yale yaliyoongeza mapato yao.

Kwa mara ya kwanza, kampuni ya SpaceX ya bilionea Elon Musk imeonekana katika orodha ya watengenezaji wakuu wa zana za kijeshi duniani, baada ya mapato yake ya silaha kuongezeka zaidi ya mara mbili ikilinganishwa na mwaka wa 2023 na kufikia dola bilioni 1.8.

Makampuni matatu ya silaha ya utawala wa kizayuni wa Israel katika orodha hiyo yaliongeza mapato yao ya pamoja ya silaha kwa asilimia 16 hadi dola bilioni 16.2 yakiwa na vita vya mauaji ya vimbari vinavyoendelea katika Ukanda wa Ghaza, ambavyo vimeshaua hadi sasa karibu Wapalestina 70,000 na kuharibu sehemu kubwa ya eneo hilo lililowekewa mzingiro.

Kampuni ya Israel ya Elbit Systems ilijipatia faida ya dola bilioni 6.28, ikifuatiwa na Israel Aerospace Industries iliyochota dola bilioni 5.19 na Rafael Advanced Defense Systems iliyopta dola bilioni 4.7…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *