Viongozi wa dini wasisitizwa kuomba amani, utulivuViongozi wa dini wasisitizwa kuomba amani, utulivu

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amewaomba viongozi wa dini watoe mahubiri ya kumuomba Mungu ili nchi iendelea kuwa ya amani na utulivu. Malima ametoa rai hiyo juzi wakati wa kilele cha maadhimisho ya maonesho ya biashara ya mkoa huo ambayo yalianza Novemba 20, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

“Nimewaomba viongozi wa dini na kukubaliana wanapokwenda kutoa mahubiri hayo wamuombe Mwenyezi Mungu atutengenezee amani na utulivu Tanzania,” alisema Malima. Amewakumbusha  Watanzania na viongozi wa dini ya kwamba wana jukumu la kuhubiri amani na kujenga utulivu kwa kumwomba Mungu alijalie Tanzania iwe na amani.

Ametumia pia jukwaa hilo kuwasihi Watanzania waendelee kudumisha amani, kupendana, kuheshimiana na kujali utu wa mwingine. Malima alisema kufanyika kwa maonesho hayo ni kielelezo cha kuonesha umuhimu wa amani katika nchi.

Amesema mahala pasipo na amani shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi haziwezi kufanyika. Malima alisema maonesho hayo ya biashara alisema yalikuwa na lengo la kuuwezesha mkoa huo uwe kitovu cha uchumi wa kati kupitia biashara na uwekezaji wenye tija.

Amesema maonesho hayo ni muhimu kwa sababu husaidia wafanyabiashara wadogo na wakubwa kujenga mahusiano hivyo yafanyike kila mwaka. Ameagiza Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA), Mkoa wa Morogoro ihakikishe maonesho ya mwaka ujao yanakuwa ya kimataifa.

Malima ameagiza taasisi zikiwemo halmashari za wilaya za mkoa huo kushiriki katika maonesho yajayo ambayo yataendelea kuwa chachu ya kukuza uchumi wa mfanyabiashara na uchumi wa taifa kwa ujumla. SOMA: ‘Watanzania msikubali kutia doa taifa’

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo anayeshughulikia uwekezaji, viwanda na biashara, Beatrice Njawa amesema serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kuendeleza sekta binafsi, wajasiriamali na wafanyabiashara kwa lengo la kukuza mitaji na kuongeza mchango wao katika uchumi wa taifa.

Naye Mwenyekiti wa TCCIA wa mkoa wa huo, Muadhini Mnyanza amesema maonesho hayo ni ya kwanza kufanyika yakishirikisha washiriki 117 yakiwemo mashirika 88, kampuni binafsi 16, mashirika ya umma 10 na taasisi zisizo za kiserikali tatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *