Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH, amesisitiza kwamba adui hana uthubutu wa kufanya uvamizi mpya wala uwezo wa kurudia makosa yake ya huko nyuma na kuongeza kuwa, kama adui atafanya uovu wowote mpya dhidi ya Iran, atapata jibu zito zaidi na kali mno zaidi kuliko huko nyuma na hicho ni kitu ambacho hakina chembe ya shaka.

Kwa mujibu wa shirika la habari la SEPAH News, Brigedia Jenerali Ali Mohammad Naeini ambaye pia ni Naibu wa Mahusiano ya Umma wa Ofisi ya Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema hayo kwenye kipindi cha televisheni cha “Atre Asheghi” cha Kanali ya Tabarestan na huku akiwapongeza na kuwaenzi mashujaa wa mkoa wa Mazandaran, hasa wale wa wakati wa vita vya miaka minane na vita vya siku 12, amesema, kwa kweli Jeshi la Kujitolea la Wananchi la Basij ni sehemu kuu ya nguvu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Amesema: Falsafa ya kuundwaa Basij haikuwa kuchukua nafasi ya vikosi vya kijeshi, bali lengo lake lilikuwa ni kuunda kikosi cha kukjitolea cha wananchi cha kuweza kutia nguvu katika nyanja zote.

Amefafanua zaidi kwa kusema: Basij ina kazi muhimu si tu katika uwanja wa kijeshi, lakini pia katika nyanja zote ikiwa ni pamoja na kwenye masuala ya uchumi, utamaduni, usalama, mitandao na vyombo vya habari. 

Amegusia pia mizizi ya kihistoria ya kuundwa Jeshi la Kujitolea la Basij nchini Iran na kusema: Agizo la Imam Khomeini (MA) la kuunda Basij yenye watu milioni 20 alilolitoa mwezi Desemba 1979 yaani miezi minane kabla ya utawala wa zamani wa Iraq kuanzisha vita vinane dhidi ya Iran tena katika wakati ambao vitisho havikuwa vikubwa sana, lilitokana na muono wa mbali na mikakati na busara kubwa za Imam Khomeini kwani kuundwa jeshi hilo kunaonesha faida zake kubwa hadi leo hii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *