Madrid, Hispania. Kuna dalili za kutokea kwa vita mpya ya usajili baina ya Manchester United na Real Madrid, baada ya ripoti kuibuka kuwa kiungo Federico Valverde yuko tayari kuangalia uwezekano wa kutua Old Trafford kufuatia kutofautiana na kocha Xabi Alonso.

Valverde, ambaye amebakiza mkataba hadi 2029, anaripotiwa kutoridhishwa na mtindo wa uongozi wa Alonso, huku akitajwa kuwa miongoni mwa wachezaji kadhaa wa Real wasiokuwa na furaha ndani ya Bernabeu. Inadaiwa kwamba kama hali haitabadilika, huenda akafikiria kuondoka.

United yamnyemelea

Kocha wa United, Ruben Amorim, ni shabiki mkubwa wa Valverde na angependa kumleta Old Trafford ili kuimarisha safu ya kiungo. Hata hivyo, Real Madrid imeshatangaza kwamba kama nyota huyo wa Uruguay anataka kuondoka, basi dau lake ni paundi milioni 100.

United wao wanamthaminisha Valverde kwa paundi milioni 70, na hilo limefanya pande hizo mbili kuwa mbali sana katika mazungumzo ya thamani. Aidha, historia inaonyesha kuwa United hawajawahi kuwa na uhusiano mzuri na Real Madrid katika masuala ya usajili.

Moto mwingine kwa Alonso

Valverde siyo mchezaji pekee aliyepishana na Alonso. Kocha huyo mpya pia ameshawahi kuonekana akizozana na Vinicius Jr, wakati ambapo staa huyo wa Kibrazil bado yupo kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba mwingine.

Hata hivyo, Alonso anasema changamoto anazokutana nazo zilikuwa ndani ya matarajio yake:

“Ni kazi ngumu, lakini ndiyo nilivyotarajia. Kuna wakati unahitaji utulivu, na wakati mwingine unahitaji maamuzi ya haraka. Lakini naufurahia mzigo wote wa kazi hii. Hizi changamoto si mpya makocha wengi wamewahi kupitia.”

Kwa sasa Madrid wanataka kubaki na Valverde, lakini mtafaruku wake na kocha unaweza kugeuza upepo na United wanasubiri tu nafasi ifunguke.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *