Mwamuzi raia wa Cameroon, Antoine Essouma, ‘aliyewabeba’ Wydad AC dhidi ya Azam FC ana matatizo hayo tangu zamani.

Mwaka 2019 Shirikisho la Soka barani Afrika, CAF, lilimfungia mwaka mzima kufuatia ‘madudu’ aliyoyafanya kwenye moja ya michezo ya vilabu barani Afrika

Mchezo uliomgharimu ulikuwa wa Kombe la Shirikisho hatua ya makundi, kati ya RS Berkane na Raja Casablanca, zote za Morocco.

Baada ya mchezo huo uliomalizika kwa sare tasa, Raja wakapeleka malalamiko CAF wakisema wanaamini wangeshinda kama sio mwamuzi huyo kuubananga na kuubagaza mchezo huo.

Raja ambao walikuwa mabingwa watetezi wa Kombe la Shirikisho, walitishia kutopeleka timu uwanjani kwenye fainali ya Super Cup dhidi ya mabingwa wa ligi ya mabingwa Esperance Tunis, mjini Doha, Qatar, kwenye dimba la Thani bin Jassim.

CAF wakafanya uchunguzi wao na kubaini kwamba mwamuzi huyo hakuwa kwenye kiwango kinachostahili, na ndipo akafungiwa mwaka mmoja.

Raja wakapeleka timu kwenye Super Cup na kushinda 2-1.

Lakini hata hivyo, madudu aliyoyafanya siku ile ni nafuu kwa kulinganisha na haya aliyofanya dhidi ya Azam FC.

Aliwakatalia bao halali na kuwanyima penati ya wazi kabisa.

Kama alifungiwa mwaka mzima wakati ule, safari hii anatakiwa kuondolewa kabisa kwenye orodha ya waamuzi barani Afrika.

Antoine Essouma sio tu aliwanyima Azam bao halali na penati ya wazi, lakini aliwatoa mchezoni wachezaji kwa filimbi za mara kwa mara kwa faida ya Wydad kwenye matukio ya hamsini kwa hamsini.

Sijui Azam FC watachukua hatua gani lakini endapo madudu haya angewafanyia Wydad, muda huu tayari kesi ingekuwa CAF na leo Jumatatu taarifa ingetoka kwamba amefungiwa.

Azam FC walicheza vizuri sana mchezo huo wakiwabana vilivyo Wydad kuanzia dakika ya kwanza.

Lakini jitihada zao ndio hivyo tena, zilizimwa na mwamuzi huyo wa Cameroon.

Tukianza na bao lililofungwa na Jephte Kitambala, mshika kibendera alishalikubali na alikimbia kuelekea kati kuashiria bao limefungwa kihalali.

Lakini mwamuzi akapuliza filimbi ya kulikataa na kuashiria kuna uvunjifu wa sheria kabla bao halijafungwa.

Lakini marudio ya picha mjongeo hayaoneshi uvunjifu wowote wa sheria…ila ndio hivyo tena, mwamuzi kaona tofauti.

Tukija kwenye tukio la penati, mwamuzi aliashiria mpira uwe kona ilihali mlinzi wa Wydad hakuugusa mpira bali mguu wa Kitambala.

Hivyo ndivyo marudio ya picha mjongeo yalivyoonesha…lakini bwana Antoine Essouma aliona tofauti.

Mpira ni mchezo unaoamuliwa kwa matukio…na moja ya matukio ni hayo ambayo Essouma aliyaona na kuyaacha.

Endapo angeyatendea haki, habari ingekuwa tofauti kabisa.

Sio haki kwa Azam FC kukosa hata alama moja kwa aina ile ya uchezaji waliyoionesha.

Walistahili kikubwa zaidi ya walichokipata.

Takwimu za mchezo zinaonesha kwamba Azam FC waliielemea Wydad kwa kiasi kikubwa kuliko hata ilivyokuwa Wtdad wakipocheza dhidi ya vilabu vikubwa kama Manchester City au Juventus, kwenye klabu bingwa ya dunia.

Azam FC walipiga mashuti 20 kuelekea lango la Wydad, ilhali Wydad walipiga matano tu.

Mashuti manne ya Azam FC yalilenga lango, ilhali ya Wydad ni mawili tu.

Azam FC walipiga.mashuti 11 ndani ya eneo la hatari la Wydad, ilhali wao walipiga mashuti manne tu.

Kwenye mchezo wa klabu bingwa ya du ia dhidi Juventus, Wydad hawakukutana na mvua ya mashuti kama hii…Juventus walipiga mashuti 8 tu!

Na hata mechi dhidi ya Manchester City, Wydad walipigiwa mashuti 15 pekee.

Ndio maana matokeo ya kupoteza sio stahiki kwa Azam FC, walistahili kupata alama, angalau moja kwenye mchezo huu.

Azam FC wanapaswa kupeleka CAF malalamiko rasmi, kwa ushahidi wa video ya mchezo husika.

Haitasaidia kitu kwa mchezo ule, lakini angalau itawapa heshima kwa waamuzi wengine huko mbele.

Huyu Antoine Essouma akifungiwa, litakuwa somo kwa waamuzi wengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *