
Nigeria. Nyota wa muziki wa Afrobeats kutoka Nigeria, Burna Boy, anaripotiwa kufuta maonyesho yake matano yajayo katika ziara inayoendelea ya No Sign of Weakness (NSOW) huko Marekani na chanzo cha kufutwa huko kikidaiwa kuwa mauzo duni ya tiketi.
Ufafanuzi kuhusu kufutwa huko umeibuka wakati kukiwa na taarifa za tukio lenye utata ambalo huenda limeathiri mtazamo wa umma dhidi ya msanii huyo.
Maonyesho yaliyofutwa yalikuwa yamepangwa kufanyika katika miji ya Boston, Washington D.C, New York, Atlanta na Orlando.
Vyanzo vinaeleza mauzo ya tiketi kwa matukio hayo yalishuka kwa kasi baada ya video kusambaa mtandaoni ikimuonyesha Burna Boy akiwatoa mashabiki nje ya tamasha kwa madai ya ‘kulala’.
Video hiyo imeripotiwa kusababisha ukosoaji mkubwa katika mitandao ya kijamii, huku mashabiki wengi wakimtuhumu mwimbaji huyo kwa kutoheshimu hadhira yake.
Wachambuzi wanaeleza upashaji upepo huo hasi huenda umechangia kushuka kwa mauzo ya tiketi, hivyo kuilazimu timu ya ziara kufanya marekebisho ya ratiba.
Sehemu iliyobaki ya ziara ya NSOW inatarajiwa kuendelea kama ilivyopangwa, ingawa macho sasa yatakuwa katika utendaji wa maonyesho yajayo katika mauzo ya tiketi.
Burna Boy na usimamizi wake hawajatoa taarifa rasmi kuhusu kufutwa kwa maonyesho hayo au tukio lililosababisha mjadala huo.