Marekani. Wikiendi iliyopita moja kati ya matukio makubwa yaliyotokea ni shoo ya msanii wa R&B, Joe Thomas iliyofanyika viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam.
Shoo hiyo ni sehemu ya ziara ya dunia ya staa huyo ambaye baada ya kuitangaza ilivunja rekodi ya mauzo ya tiketi katika wiki ya kwanza tu.
Inawezekana ulikuwa miongoni mwa waliotazama shoo yake au walioshuhudia mitandaoni, hapa tunakusogezea utajiri kamili ambao fundi huyu anao kuanzia anavyopiga pesa na mali anazomiliki.
ANAPIGAJE PESA
Utajiri wa Joe Thomas unakadiriwa kufikia Dola 25 milioni na unatokana na muziki na madili yake mengine.
Joe alipata pesa nyingi kupitia mauzo ya Albamu 13 alizowahi kuzitoa, pia amekuwa akiingiza pesa pia kupitia shoo mbalimbali.
Katika kipindi alichokuwa anatamba sana miaka ya 90 na 2000, alikuwa akiingiza takribani Dola 80,000 hadi 150,000, kwa shoo moja.
Katika ziara yake ya mwaka 2024 hadi 2025 anakadiriwa kungiza Dola 5 milioni.
Mbali ya kuimba, Joe pia amekuwa akiingiza pesa kupitia uandishi wa nyimbo mbalimbali. Amewahi kuandika nyimbo za wasanii kama Mariah Carey, Big Pun, G-Unit na Kelly Rowland.
Vilevile amefanya kazi ya kuwa balozi wa kampuni kama Ciroc, Beats by Dre na Sean John Fragrance. Anapata takribani Dola 1 milioni wa mwaka kama pesa za udhamini.
Mkongwe huyu pia anamiliki studio yake binafsi Atlanta ana hisa katika migahawa kadhaa huko Atalanta.
Ana mjengo wa kifahari huko Atlanta ambao una thamani ya Dola 3 milioni ambalo ndani yake lina vyumba saba vya kulala, studio ya muziki ya ndani, Gym na Swimming pool.
Pia ana mjengo huko New Jersey yenye thamani ya Dola 1.5 milioni ambayo pia ina studio ya muziki na ofisi ya maandalizi shoo zake.
Mjengo mwingine pia upo huko Miami ambao mara nyingi huwa anaitumia wakati wake wa mapumziko. Nyumba hiyo ina thamani ya Dola 900,000.
MSAADA KWA JAMII
Joe ni miongoni mwa wanamuziki wanaopenda kufanya misaada kimya kimya. Anafanya mengi kupitia Joe Thomas Foundation, ambayo inasaidia vijana wanaotaka kusoma masuala ya muziki, wanafunzi kutoka familia zenye kipato cha chini, miradi ya kupambana na utumiaji wa dawa za kulevya na Huduma za afya kwa jamii za wahamiaji.
Mwaka 2023 pekee, taasisi yake ilitumia zaidi ya Dola 800,000 katika miradi ya kijamii.
FAMILIA NA BATA
Joe amekuwa mtu wa maisha ya utulivu. Ameoa na ana watoto wawili. Mara nyingi hutumia muda mwingi akiwa Studio.
Licha ya kuwa na zaidi ya miaka 25 katika muziki, Joe bado ni miongoni mwa wasanii wanaokubalika sana duniani.