Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan amekutana hapa mjini Tehran na kufanya mashauriano na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, Spika wa Bunge Mohammad Baqer Qalibaf, na Waziri wa Mambo ya Nje Seyyed Abbas Araqchi.

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hali hasasi na nyeti iliyopo hivi sasa katika Ulimwengu wa Kiislamu na kueleza kwamba: “wakati maadui wa pamoja wa mataifa ya Kiislamu wanatafuta njia za kuzidisha mashinikizo, ingetarajiwa nchi za Kiislamu zirahisishiane hali na mazingira na kujiepusha na utatizaji wa mambo”.

Rais Pezeshkian ameyasema hayo katika mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan yaliyofanyika jana usiku hapa mjini Tehran, ambapo sambamba na kuashiria masuala ya pamoja ya historia, utamaduni, na uhusiano wa kiudugu wa muda mrefu uliopo kati ya Iran na Uturuki ameeleza kwamba, uhusiano huo umekita mizizi, ni wa dhati, na wenye fursa nyingi za kustawishwa; na akaongezea kwa kusema: “ikiwa nchi za Kiislamu zitachukua hatua kwa irada na utashi wa pamoja uliofungamana na umoja, muelekeo mmoja, na kubadilishana uzoefu na tajiriba, hakuna dola lolote litakaloweza kuyakwamisha mataifa ya Kiislamu”.

Akizungumzia tajiriba na uzoefu wa Ulaya, Rais wa Iran amekumbusha kuwa, licha ya kuwa na historia ndefu ya vita na migogoro, nchi za Ulaya leo zimeweza kuhafifisha mipaka yao, kuunda miundo ya pamoja ya kifedha na kisiasa, na kuunganisha mitandao yao ya biashara na usafirishaji; na akabainisha kuwa: kutokana na Ulimwengu wa Kiislamu kuwa na mambo mengi zaidi ya pamoja ya kiutamaduni na kiustaarabu yanayofanana, ikiwa yataweka kando tofauti na kufuata mkondo wa ushirikiano thabiti na maendeleo ya pamoja, utaweza bila shaka yoyote kusonga mbele kupitia uunganishaji wa mitandao ya biashara, utaalamu, na utamaduni.

Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) pia amesema katika kikao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki: “Utawala wa Kizayuni na Marekani kwa muda mrefu zimekuwa zikipinga kuimarishwa, umoja, ukuaji, uadilifu na maendeleo ya nchi za Kiislamu na kutaka kuzibakisha nchi za eneo hili katika migogoro mbalimbali.”

Mazungumzo ya Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyyed Abbas Araqchi pia amesema kuhusiana na mazungumzo yake na mwenzake wa Uturuki Hakan Fidan: “Katika vikao vya wazi na vya faragha, suala la Gaza na Palestina, ambalo siku zote ndilo linalozitia wasiwasi nchi zote mbili lilijadiliwa.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa: “Siasa za kichokozi na za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel katika eneo hili ambazo zimezitia wasiwasi nchi zote za eneo na kwa vyovyote vile mashambulizi ambayo umekuwa ukiyafanya katika zaidi ya nchi saba katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ni miongoni mwa masuala tuliyoyajadili.”

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki, yakiwa mataifa mawili muhimu ya kikanda, yana nafasi kubwa katika matukio ya Asia Magharibi. Suala la Palestina na Gaza siku zote limekuwa moja ya mihimili mikuu ya mijadala ya nchi hizo mbili, kwani zote zimeahidi kuwa zimejitolea kuwaunga mkono wananchi wa Palestina.

Mitazamo ya pamoja ya Iran na Uturuki inaweza kubadilisha mizani ya nguvu dhidi ya utawala wa Kizayuni na sera za Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Ukweli ni kuwa, uhusiano wa Iran na Uturuki umekita mizizi na msingi wake ni historia, utamaduni, na udugu wa pamoja. Ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kitamaduni pia unaandaa uwanja mkubwa wa maendeleo na ustawi. Hapana shaka kuuwa, kuimarisha ushirikiano huu kunaweza kusaidia kupunguza mashinikizo kutoka nje na kuongeza uhuru wa kikanda na mamlaka ya kujitawala.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyyed Abbas Araqchi  na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan katika mkutano na waandishi wa habari

Mkutano na mazungumzo ya Fidan na maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia yanaonyesha kuwa Iran na Uturuki zinataka kuimarisha maelewano ya kistratijia; muelekeo mmoja ambao hauna taathira chanya tu kwa uhusiano wa pande mbili, lakini pia unaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine za Kiislamu katika kukabiliana na uingiliaji wa kigeni.

Mielekeo ya pamoja ya Iran na Uturuki inaweza kupelekea kuundwa mrengo wenye nguvu zaidi wa kuunga mkono Palestina. Ushirikiano huu utazidisha mashinikizo ya kisiasa na kidiplomasia dhidi ya utawala wa Kizayuni na kuweka njia ya kupata uungaji mkono mpana kutoka kwa ulimwengu wa Kiislamu kwa watu wa Gaza.

Muungano wa kimkakati kati ya Iran na Uturuki unaweza kuzuia kuenea kwa migogoro na vita vya niaba katika kanda hii. Ushirikiano huu, haswa katika hali nyeti ya sasa, unaweza kusaidia kudhibiti majanga ya usalama na kibinadamu katika Asia Magharibi.

Ni dhahir shahir kwamba, ushirikiano kati ya Iran na Uturuki una umuhimu wa kistratijia sio tu kwa Palestina, bali pia kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu; muungano huu unaweza kupunguza migogoro, kuongeza uhuru na mamlaka ya kujitawala ya kikanda, na kujenga mustakabali wenye nguvu dhidi ya mashinikizo kutoka nje.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *