Kiongozi wa kisiasa na kiongozi wa chama cha upinzani cha Manidem, Anicet Ekane, amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumatatu, Desemba 1.

Habari hiyo imethibitishwa na wanasheria na familia yake mapema leo. Ekane alikamatwa Oktoba 24 huko Douala na tangu wakati huo alikuwa kizuizini katika Sekretarieti ya Wizara ya Ulinzi huko Yaoundé.

Mpinzani huyo wa Rais Paul Biya wa Cameroon alishutumiwa kwa kumuunga mkono Issa Tchiroma ambaye alikuwa amejitangaza mshindi wa uchaguzi wa urais. Serikali ililitambua tangazo la Tchiroma kuwa ni sawa na uasi. Makumi ya watu waliuawa katika ukandamiza wa vikosi vya usalama uliofuatia tangazo hilo.

Tangu wakati huo, Issa Tchiroma alikimbilia nchini Gambia.

Chama cha Ekane cha African Movement for New Independence and Democracy (Manidem) mnamo Novemba 21 kililishutumu jeshi la polisi kuwa limetwaa vifaa vya matibabu vya Ekane.

Jana Jumapili, Novemba 30, chama chake cha siasa, Manidem, kilitoa taarifa kikitaka ahamishwe haraka na kupelekwa kwenye hospitali nyingine kwa ajili ya huduma ya matibabu ambayo ilitarajiwa kuwa “muhimu na inayofaa zaidi.”

Chama hicho kimetangaza kuwa “kitauwajibisha utawala wa Yaoundé kwa matokeo ya kukataa uhamisho huo.”

Ekane alikuwa mtu muhimu katika upinzani wa mrengo wa kushoto wa Cameroon.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *