UONGOZI wa Mbeya City umefikia makubaliano ya kusitisha mkataba na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Malale Hamsini ikiwa ni saa chache tangu ichapwe bao 1-0 na Namungo katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini, Mbeya.
Katika mechi hiyo iliyopigwa juzi, mabosi wa Mbeya City walitangaza kuachana na Malale baada ya presha kubwa ya mashabiki, sambamba na wasaidizi wake kadhaa, huku Patrick Mwangata akibakishwa pekee yake na kuanikwa sababu zilizombeba ikiwamo kuiva na wachezaji wote.
Taarifa ya klabu hiyo iliyotolewa juzi usiku ilitangaza kusitisha mkataba wa kocha Malale, msaidizi wake Mussa Rashid, kocha wa makipa, Wilbert Mweta na Daktari Hashraf Mapunda, huku Mwangata akisalimika katika benchi hilo akiachwa kikosini.
Mmoja wa viongozi wa timu hiyo, aliliambia Mwanaspoti, sababu kubwa iliyochangia Mwangata abaki ni kutokana na umoja na mshikamano alionao kwa wachezaji, kwani hata kipindi kigumu ambacho wamepitia alikuwa akihusika kuwajenga kisaikolojia.
“Tulianza kufanya tathimini ya wakuu wetu wote wa benchi la ufundi kwa kushirikiana na wachezaji kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho, Mwangata ameonekana kupendwa zaidi kutokana na anavyoishi nao ndio maana tukamuacha,” amesema kiongozi huyo.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Gwamaka Mwankota, amesema kilichofanyika ni uamuzi wa kawaida na sio kwa sababu ya presha ya mashabiki, japo mchakato wa kutafuta kocha mpya unaendelea na utakapokamilika watauweka wazi.
Malale alijiunga na Mbeya City Machi 31, 2025, akichukua nafasi ya Salum Mayanga aliyejiunga na Mashujaa, ambapo kocha huyo wa zamani wa maafande wa JKT Tanzania, kwa msimu wa 2025-2026, alikiongoza kikosi hicho katika jumla ya mechi tisa.
Katika mechi hizo tisa ambazo Malale aliiongoza Mbeya City, ilishinda mbili, sare mbili na kuchapwa tano, ambapo kwa ujumla kikosi hicho kilifunga mabao saba na kuruhusu 10, huku Malale akiiacha ikiwa katika nafasi ya 10 kwa pointi nane.