KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujifua kwa ajili ya mechi mbili zijazo za Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate na Coastal Union, huku nahodha msaidizi wa timu hiyo, Dickson Job akitoa kauli ya kibabe kwa mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika wawakilishi hao wa Tanzania wakiwa Kundi B.

Katika mechi hizo za CAF, Yanga imekusanya pointi nne hadi sasa kutokana na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AS Far Rabat ya Morocco na sare ya ugenini wikiendi iliyopita mbele ya JS Kabylie ya Algeria, kitu ambacho kimemfanya Job kushindwa kuvumilia na kutoa kauli hiyo akiwatia moyo mashabiki.

Job amesema ubora na ukubwa wa klabu yao ndio uliowabeba mbele ya wapinzani na kwamba mambo bado kabisa kwa vile Yanga imejiandaa kuwafanyia sapraizi mashabiki wa mechi zijazo zitakazochezwa mwakani, tofauti na mtazamo wa wengi mara baada ya makundi kupangwa.

JO 01

Beki huyo wa kati, aliliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli Yanga ipo katika kundi gumu na la kifo, lakini hadi kufikia sasa ukweli umedhihirika kwamba, mabingwa hao wa Tanzania wapo daraja jingine ndio maana walipangwa kundi gumu lenye timu bora kwa sababu hata wao ni bora vilevile.

“Timu ikishafika hatua kama hii haipaswi kumuogopa mpinzani, kinachotakiwa kufanyika ni kujiandaa na kumheshimu mpinzani. Mechi ya kwanza iliyotupa matokeo mazuri ndio inayotupa wakati mgumu wa kupambana, tungepoteza mechi ya pili matokeo ya kwanza yasingekuwa na maana sana,” amesema Job na kuongeza;

“Sare tuliyoipata ugenini haikuwa mipango yetu sisi tulikuwa tunapambania pointi tatu, lakini bahati haikuwa upande wetu ila kwa pointi moja haikuwa haba kwetu imetuweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua inayofuata. Mashabiki wajiandae kwa sapraiz zaidi.”

JO 02

Job amesema Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wengi bora na wana kila sababu ya kuipambania timu hiyo, huku akiweka wazi kumba mbali na malengo ya klabu kuanzia uongozi hadi benchi la ufundi na wachezaji pia wana malengo kupitia mashindano hayo, kwani wanajiweka sokoni.

“Kundi ni gumu lakini tupo tayari kupambana kwa ajili ya timu huu ni mwanzo bado tuna nafasi nzuri ya kuendeleza mapambano ili kufikia malengo, najivunia kuwa sehemu ya mafanikio tunayoyapambania kwani nipo na wachezaji wenye uchu wa mafanikio wanaifia timu linapokuja suala la matokeo mazuri,” amesema Job na kuongeza;

JO 03

“Sisi kama wachezaji ni wajibu wetu kupambana ili kuweza kufikia malengo. Sio rahisi, lakini juhudi na mipango imara ndio imetufikisha hapa njiani tulipo. Tunaamini hakuna kinachoshindikana, umoja na utulivu vitatufikisha kule tunakotamani kufika. Tunawashukuru mashabiki ambao wamekuwa wakituunga mkono na kutupa motisha pale wanapoona tuna kitu tunakifanya, hii inazidi kutufanya tuwe imara.”

Job ni sehemu ya wachezaji wanaounda ukuta wa timu hiyo ulio chini ya kipa Djigui Diarra ambao hadi sasa haujaruhusu bao lolote katika hatua hiyo ya makundi, lakini hata katika mechi za raundi za awali za michuano hiyo ilifungwa bao moja ilipopoteza 1-0 ugenini kwa Silver Strikers ya Malawi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *