Dar/mikoani. Wakati jiji la Dar es Salaam likipata wagombea wapya wanne wa nafasi ya umeya kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), katika baadhi ya mikoa mingine vigogo wameangushwa.

Wagombea wa CCM waliopatikana leo, Desemba 1, 2025 baada ya kushinda kura za maoni zilizofanyika nchi nzima ndani ya mchakato wa chama, sasa wataingia katika uchaguzi utakaowajumuisha pia wagombea kutoka vyama vingine vya siasa, mara mabaraza ya madiwani yatakapotangazwa na madiwani kuapishwa rasmi.

Miongoni mwa nafasi zitakazogombewa ni umeya, naibu meya, mwenyekiti wa halmashauri na makamu wake.

Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam, lenye manispaa nne ambazo ni Kigamboni, Kinondoni, Ubungo na Temeke, Manispaa ya Ilala, inayosimamiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, nayo imepata mgombea mpya wa umeya, huku meya wa Manispaa ya Kinondoni akiendelea kutetea nafasi yake.

Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, ameshindwa kutetea nafasi yake, ambayo sasa itagombewa na diwani wa Mchikichini, Nurdin Juma (Shetta).

Kwa upande wa Manispaa ya Temeke, imepata mgombea mpya ambaye ni diwani wa Tandika, Uzairu Athumani, huku diwani wa Viti Maalumu, Nuru Cassian, akiteuliwa kugombea nafasi ya naibu meya.

Kwa upande wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni, diwani wa Kibada, Amani Mzuri Sambo, ameibuka mshindi kugombea nafasi ya meya, huku Elizabeth Kimambo alichaguliwa kugombea nafasi ya naibu meya wa Kigamboni.

Kwa upande wa Manispaa ya Kinondoni, kwa mara nyingine wamemrudisha diwani wa Mwananyamala, Songoro Mnyonge, ili kugombea nafasi ya meya wa manispaa hiyo, huku Aman Balande akichaguliwa kugombea nafasi ya naibu meya.

Frank Thomas Lupimo akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi katika nafasi hiyo ya umeya.

Mkoani Dodoma

Hali kama hiyo imetokea jijini Dodoma, ambapo aliyekuwa meya, Profesa David Mwamfupe, ameangushwa kwenye kura za maoni na diwani wa Makutupora, Amon Chaula. Profesa Mwamfupe alikuwa akigombea muhula wa tatu, lakini ameshika nafasi ya tatu kati ya wagombea watatu, na hivyo kuhitimisha uongozi wake.

Nafasi ya naibu meya inagombea Bakari Fundikira, ambaye ni diwani wa Chang’ombe. Wilayani Mpwapwa, wameendeleza utamaduni wa kuachiana kati ya Jimbo la Mpwapwa na Kibakwe, ambapo Richard Maponda amechaguliwa kuwa mwenyekiti, akitokea upande wa Jimbo la Kibakwe, ambaye awali alikuwa makamu mwenyekiti.

Mkoa wa Kilimanjaro

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo wamemchagua Gilbert Tarimo kuwania nafasi ya uenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, huku mgombea wa nafasi ya mwenyekiti akichaguliwa Denis Damas.

Diwani wa Njiapanda John Meela akizungumza baada ya kutangazwa kushinda kugombe nafasi ya mwenyekiti wa Halmashauri ya Moahi

Wilaya ya Hai, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Hai, Edmund Rutaraka, ametetea nafasi hiyo baada ya kushinda kwenye kura za mchujo.

Kwa upande wa Wilaya ya Moshi Vijijini, diwani wa Njiapanda, John Meela, amechaguliwa kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Moshi kwa kupata kura 34 kati ya kura 45 zilizopigwa.

Kwa upande wa nafasi ya makamu mwenyekiti, mshindi wa kura za maoni ni diwani wa Mwika Kaskazini, Samuel Shao.

Wilaya ya Same, aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Yusto Mapande, amechaguliwa kutetea nafasi yake, huku nafasi ya mgombea wa makamu mwenyekiti wa halmashauri ikienda kwa Rashid Rashid.

Kwa Wilaya ya Mwanga, aliyeshinda nafasi ya kugombea mwenyekiti wa halmashauri ni Joseph Mrutu, huku nafasi ya makamu mwenyekiti ikichaguliwa Abas Hassan.

Katika Manispaa ya Moshi, diwani wa Njoro, Zuberi Kidumo, amechaguliwa kutetea nafasi yake.

Mkoa wa Singida

Wilaya ya Iramba imemchagua Innocent Msengi, wakati Manispaa ya Singida, aliyekuwa Naibu Meya, Godfrey Mdama, ameshinda nafasi hiyo. Wilaya ya Ikungi wamemchagua Ally Mwanga.

Kwa upande wa Halmashauri ya Singida, mgombea aliyechaguliwa kugombea nafasi ya uenyekiti ni Eliah Digha.

Mkoa wa Mbeya, Songwe

Jijini Mbeya, aliyekuwa meya awamu iliyopita, Dormohamed Issa, na naibu wake, Kephasi Mwasote, wametetea nafasi zao kwa kuchaguliwa kugombea tena.

Mshindi wa nafasi ya Meya, Dormohamed Issa (kushoto) akizungumza jambo baada ya kumalizika uchaguzi wa kuwachagua Meya na Naibu Meya, pembeni ni Naibu wake Kephasi Mwasote aliyeshinda nafasi ya Naibu Meya.

Wilaya ya Ileje mkoani Songwe, mgombea wa uenyekiti wa halmashauri amechaguliwa diwani wa Chitete, Osiwelo Chomo, huku nafasi ya makamu mwenyekiti, mgombea aliyechaguliwa, ni Hakika Kajange.

Mkoa wa Manyara

Mkoani Manyara, katika Halmashauri ya Simanjiro ameshinda Kaleya Mollel, huku Halmashauri ya Wilaya ya Babati, aliyekuwa mwenyekiti wake, John Noya, amefanikiwa kutetea nafasi hiyo.

Jijini Arusha, diwani wa Kaloleni, Maxmillian Iranghe, ameshinda na kuwa mgombea wa nafasi hiyo, huku Wilaya ya Karatu, diwani wa Mbulumbulu, Engelbert Qorro, ametangazwa mshindi.

Mkoa wa Morogoro

Katika Manispaa ya Morogoro, diwani wa Mjimkuu, Khalid Mazengo, ameibuka mshindi, huku nafasi ya naibu meya ikipata Mohamed Thabii.

Diwani wa Kata ya Mjimkuu, Manispaa ya Morogoro, Khalid Mohamed Mazengo akitoka katika chumba cha kupigia kura baada ya kuibuka mshindi katika kura za maoni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania nafasi ya Meya wa Manispaa hiyo katika uchaguzi uliofanyika katika Ofisi ya CCM Kingo mjini hapa. Picha na Juma Mtanda

Mkoani Rukwa, Diwani wa Milanzi, Frank Lupimo, amechaguliwa kugombea nafasi ya Meya wa Sumbawanga, huku upande wa naibu meya akichaguliwa John Methew.

Pia, mkoani Geita, Diwani wa Bombambili, Leonard Bugomola, amechaguliwa kugombea umeya wa Manispaa ya Geita, huku nafasi ya naibu meya, mgombea akichaguliwa Elias Ngole.

Mkoani Lindi, Twahili Mpuruji ameshinda na kuwa mgombea wa umeya, na kwa upande wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Siha, Dancan Urassa, amechaguliwa tena kutetea nafasi hiyo, huku Stanley Nkini akichaguliwa kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti.

Wilayani Mufindi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Regnant Kivinge, amechaguliwa tena kutetea nafasi yake, huku nafasi ya mgombea wa makamu mwenyekiti ikienda kwa Diwani wa Sao Hill, Steveni Msingwa.

Kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, diwani wa Igowole, Castory Masangula, amechaguliwa kugombea nafasi hiyo, huku mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti ikienda kwa Diwani wa Satanic, Saidi Mmanga.

      

Bariadi, mgombea pekee ashindwa

Wilayani Bariadi, mgombea pekee wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Zebedayo King, alipingwa na wajumbe, na kusababisha nafasi hiyo kubaki wazi.

King, ambaye ni diwani wa Sima, alipata kura nne za ndiyo dhidi ya 11 za hapana.

Jumanne Misungwi,diwani kata ya Ludete ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Geita.

Hata hivyo, kwenye uchaguzi, Zawadi Mkilila, ambaye ni diwani wa Viti Maalumu, ameibuka kidedea katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, baada ya kupata kura 15 za ndiyo bila kupingwa hata kwa kura moja.

Kwa upande wa Bariadi Vijijini, Mayala Shiminji, ambaye ni diwani wa Kasoli, ameshinda na kuwa mgombea.

Imeandikwa na Habel Chidawali (Dodoma), Janeth Joseph na Florah Temba (Moshi), Bakari Kiango, Tuzo Mapunda, Mintanga Hunda na Pawa Lufunga (Dar), Sadam Sadick (Mbeya), Filbert Rweyemamu (Arusha), Juma Mtanda (Moto), Denis Sinkonde (Ileje), Sanjito Msafiri (Kibaha), Florah Temba na Janeth Joseph (Kilimanjaro), Neema Mtuka (Rukwa), Samwel Mwanga (Bariadi), Geofrey Chubwa (Geita), Bahati Mwatesa (Lindi), Bahati Chume (Siha) na Mary Sanyiwa (Mufundi).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *