
Bariadi. Mchakato wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu umemalizika kwa mgombea pekee wa nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Zebedayo King kupigiwa kura nyingi za hapana.
King alikuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo aliyopitishwa na kamati kuu ya CCM, chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan ambapo kura za maoni zimefanyika leo Jumatatu, Desemba 1, 2025.
Katika kura hizo za maoni, King ambaye ni Diwani wa Sima ameambulia kura nne za ndio dhidi ya 11 za hapana, matokeo yaliyoibua mshangao kwake mwenyewe, na kufanya nafasi hiyo kulazimu mchakato kuanza upya.
Wakati King hilo likitokea kwa King, Zawadi Mkilila, Diwani wa Viti Maalumu ameibuka kidedea katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi baada ya kupata kura 15 za ndiyo bila kupingwa hata kwa kura moja.
Wakati Bariadi Mji ikikosa mshindi, upande wa Bariadi Vijijini mambo yalikwenda vizuri baada ya Mayala Shiminji ambaye ni Diwani wa Kasoli kushinda kwa kura 19, dhidi ya mpinzani wake, Isack Masunga wa Kata ya Nkololo aliyeambulia kura tisa.
Daud Mayala ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa za ndani ya CCM amesema matokeo ya Bariadi Vijijini yanadhihirisha mwelekeo tofauti katika vipengele vya uongozi, kukubalika kwa Shiminji kutokana na rekodi yake ya kiutendaji na mahusiano na wajumbe.
Akizungumza na waandishi wa habari, Ibrahimu Kijanga, Katibu wa CCM Wilaya ya Bariadi na Mkurugenzi wa uchaguzi huo, amesema huo ni mchakato wa ndani ya chama.
“Siwezi kusema chochote bali, michakato ndani ya CCM tumemaliza kwa kuzingatia utaratibu wa CCM taifa, hivyo tunapeleka halmashauri ili waendelee na utaratibu. Wanalilia madaraka, ndio maana uchaguzi wa mgombea mmoja umechukua muda mrefu,” amesema.
John Masanja ambaye ni mwanachama wa CCM wilaya ya Bariadi amesema matokeo hayo yanatoa mwanga mpya kuhusu namna wajumbe wanavyochukua tahadhari na uwajibikaji kabla ya kupitisha majina ya wagombea.
“Kukosa mshindi siyo changamoto, ni ujumbe wa demokrasia. Hii ni CCM mpya,” amesema.