Kumeripotiwa mapigano makali na miripuko ya mabomu jana usiku kabla ya waasi wa M23 kufanikiwa hatimaye kuingia na kuchukua udhibiti wa mji wa kimkakati wa mashariki mwa DRC wa Uvira na kusababisha hali ya hofu iliyopelekea maelfu ya raia wa Kongo kukimbilia katika nchi jirani ya Burundi. Hata hivyo baadhi ya mashuhuda wamesema kuwa mapigano yalikuwa yakiendelea katika baadhi ya maeneo ya mji huo.
Kulingana na vyanzo mbalimbali vya kiusalama na kijeshi, wanamgambo hao waliingia Uvira wakitokea eneo la kaskazini, huku Marekani na mataifa kadhaa ya Ulaya yakiwahimiza waasi wa M23 kusimamisha mara moja mashambulizi yao na kuitaka Rwanda kuwaondoa wanajeshi wake kutoka eneo hilo la mashariki mwa DRC lenye utajiri mkubwa wa madini.
Corneille Nangaa, msemaji wa AFC/M23 ametetea hatua ya kundi hilo kuchukua udhibiti wa mji wa Uvira:
” Kwa zaidi ya miezi mitatu, kumekuwa na vurugu huko Uvira. Na hili ni kwa sababu ya uwepo wa vikosi tofauti visivyo na uongozi wala muelekeo. Kwa hiyo, baada ya vikosi vya Burundi kujiondoa, jeshi la Kongo na Wazalendo walianza kupigana wao kwa wao. Inavyoonekana, sasa wameamua kuuacha mji huo kutokana na hofu na kuwatelekeza raia. Labda mtu atajiuliza tutakachokifanya. Sisi tutawalinda wananchi na hatutaruhusu vurugu hizi kuendelea kwa muda mrefu. Lazima tujipange ili kurejesha hali ya utulivu, ” alisema Nangaa.
Maelfu ya raia na wanajeshi wa DRC wakimbilia Burundi
Wakati M23 ikichukua udhibiti wa ngome kubwa ya mwisho katika jimbo la Kivu Kusini, wanajeshi wengi wa Kongo walichanganyikana miongoni mwa raia waliokimbilia Burundi, nchi iliyokuwa imewatuma wanajeshi wake kusaidia DRC kupambana na Rwanda.
Chanzo kimoja kutoka serikali ya Burundi kimeliambia shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina kwamba katika kipindi cha siku mbili zilizopita kimeorodesha zaidi ya watu 8,000 wanaowasili kila siku kutoka Kongo na kwamba serikali haina uwezo wa kuwahudumia iwe kwa chakula au huduma za matibabu.
Shirika la Kimataifa la Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR limesema katika kipindi cha wiki moja pekee, watu takriban 30,000 wameingia nchini Burundi huku Umoja wa Mataifa ukisema mapema wiki hii kuwa watu 200,000 wameyakimbia makazi yao mashariki mwa Kongo katika siku za hivi karibuni.
Shambulio la hivi punde la M23 linajiri takriban mwaka mmoja tangu kundi hilo linaloungwa mkono na Rwanda kuchukua udhibiti wa miji muhimu ya Goma na Bukavu, katika eneo ambalo limekumbwa na machafuko kwa zaidi ya miongo mitatu. Haya yanajiri pia ikiwa ni siku chache tu tangu marais wa Rwanda Paul Kagame na yule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi watie saini makubaliano ya amani mjini Washington.
Wasiwasi wa Burundi baada ya M23 kuudhibiti mji wa Uvira
Kitendo cha Uvira kuanguka mikononi mwa waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda ni tishio kubwa la kiusalama kwa Burundi hasa ikizingatiwa kuwa mji huo upo ng’ambo ya Ziwa Tanganyika na unapatikana kilometa chache tu kutoka mji mkuu wa kiuchumi wa Burundi – Bujumbura.
Burundi ilituma wanajeshi wapatao 10,000 mashariki mwa DRC mnamo Oktoba mwaka 2023 kama sehemu ya makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na DRC, lakini vyanzo vya usalama vinasema kuwa idadi hiyo inaweza kufikia wanajeshi 18,000.
Baada ya miezi kadhaa ya utulivu katika uwanja wa mapigano, vikosi vya M23 vikisaidiwa na wanajeshi wa Rwanda vilianzisha mashambulizi mnamo Desemba 1, 2025 na kuulenga mji wa Uvira.
Ingawa serikali ya Kigali imekuwa ikikanusha kutoa msaada wa kijeshi kwa M23, imesema hata hivyo kwamba inakabiliwa na tishio kubwa la kiusalama kutokana na uwepo eneo hilo la Mashariki mwa DRC wa wanamgambo wa Kihutu wa FDLR wanaohusishwa na mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi ya mwaka 1994 nchini Rwanda.
(Vyanzo: AFP, AP)