
Mohamed Salah amerudi dimbani na ushindi baada ya kuisaidia Liverpool kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Brighton huku Chelsea ikifufua matumaini ikiichapa Everton 2-0.
Salah amekuwa nje ya kikosi katika mechi kadhaa kutokana na sintofahamu yake na Kocha Mkuu, Arne Slot.
Katika mchezo wa leo, Salah aliyeingia katika dakika ya 26 kuchukua nafasi ya Joe Gomez, alipiga pasi moja iliyozaa bao la Hugo Ekitike katika dakika ya 60.
Kabla ya hapo, Ekitike aliifungia bao la kuongoza Liverpool katika dakika ya kwanza ya mchezo akimalizia pasi ya Gomez.
Goli hilo la kwanza la Ekitike limeweka rekodi ya kuwa bao la mapema zaidi katika Ligi Kuu ya England (EPL) msimu huu.
Kwa pasi ya mwisho ambayo imezaa bao la Ekitike, Salah anakuwa mchezaji wa Liverpool aliyepiga pasi nyingi zaidi za mabao msimu huu akifikisha tatu.
Ushindi huo umeinyanyua Liverpool ambayo ilikuwa nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na kupaa hadi nafasi ya sita ikiwa na pointi 26 baada ya mechi 16.
Chelsea ambayo ilikua haijapata pointi tatu katika mechi nne, leo imeondoka na kicheko katika Uwanja wa Stamford Bridge baada ya Cole Palmer na Malo Gusto kuitungua Everton.
Chelsea imepanda hadi nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 28 baada ya mechi 16.