
Iran imesema kuwa madai yoyote ya kumiliki visiwa vitatu vya Ghuba ya Uajemi yaani Tomb Kubwa, TombNdogo na Bu Musa ni ukiukaji wa kanuni za ujirani mwema na kutoheshimu mamla ya kujitawala ya nchi nyingine.
Esmaeil Baghaei Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje amelaani madai “yasiyo na msingi” yaliyotolewa katika taarifa ya pamoja kufuatia mkutano wa siku ya Jumapili kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan na mwenzake wa China, Wang Yi.
Baghaei amesisitiza kuwa visiwa hivyo vitatu ni “sehemu zisizoweza kutenganishwa za ardhi ya Iran” na kuikosoa Imarati kwa kutumia mara kwa mara matukio ya kidiplomasia kurejelea madai kwamba visiwa hivyo vitatu ni milki yake.
Visiwa vitatu vya Iran vya Tomb Kubwa, Tomb Ndogo na Bu Musa kihistoria vimekuwa sehemu ya Iran; jambo ambalo linathibitishwa na hati nyingi za kihistoria, kisheria, na kijiografia. Hata hivyo, Umoja wa Falme za Kiarabu umekariri madai yake kuhusu umiliki wa visiwa hivyo.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari, Waziri wa Mambo ya Nje wa China ameunga mkono jitihada za Imarati za kutatua kwa amani suala la visiwa hivyo vitatu kupitia mazungumzo ya pande mbili kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.
Wiki iliyopita, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge la Iran) Mohammad Baqer Qalibaf pia alipuuzilia mbali madai ya kukaririwa kuhusu visiwa vitatu vya Iran katika taarifa ya mwisho ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (GCC), ambapo aliyaonya mataifa jirani kutoijaribu azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya kulinda mamlaka yake ya kujitawala na umoja wa ardhi nzima ya nchi hii.