Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha huko Ghaza hadi hivi sasa zimeshaharibu asilimia 90 ya mahema wa wakimbizi wa ukanda huo tena wakati huu wa kukaribia kuingia kwenye msimu wa baridi kali.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Shirika la Ulinzi wa Mji wa Ghaza, kuharibiwa mahema hayo ya wakimbizi kunatishia maisha ya Wapalestina wengi na hadi hivi sasa hali hiyo imeshababisha vifo vya Wapalestina wengine 15, wakiwemo watoto wadogo watatu.

Hali mbaya ya hewa huko Ghaza na mafuriko kwenye mitaa na ndani ya mahema ya wakimbizi kumewasababishia matatizo mengine Wapalestina wasio na ulinzi.

Mahmoud Basal, msemaji wa Shirika la Ulinzi wa Mji wa Ghaza amesema kuwa, hali hiyo imeshapelekea asilimia 90 ya mahema wa ukanda huo kuharibiwa.

Utawala wa Kizayuni unaendelea kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia Ghaza, jambo ambalo linazidisha matatizo  na maafa makubwa ya kibinadamu katika ukanda huo.

Duru mbalimbali za Wapalestina wa eneo hilo zimesema kuwa, mahema ya wakimbizi katika eneo moja la magharibi mwa mji wa Ghaza na karibu na kitongoji cha Shuja’iyah yamezama kabisa chini ya maji. Wingi wa maji ya mvua umesababisha mafuriko yaliyoenea maeneo mbalimbali mpaka katika Hospitali ya Al-Shifa kiasi kwamba hata eneo la mapokezi la hospitali hiyo limezama kabisa chini ya maji ya mafuriko.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa, mitaa mingi huko Ghaza nayo iko chini ya maji hivi sasa, kutokana na mvua kubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *