Casablanca, Morocco. Mashindano ya 35 ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) yataanza Morocco, Jumapili hii huku fainali yake ikitarajia kufanyika jijini Rabat, Januari 18, 2026.

Wenyeji wa mashindano hayo, Morocco wana matumaini ya kunyakua ubingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1976, wakati Mohamed Salah anaamini atakwenda kuyaweka kando matatizo yake na Liverpool ili kuisaidia Misri kufanya kweli na kubeba taji hilo baada ya kuwahi kufanya hivyo mwaka 2010.

Wakati joto la mashindano hayo likizidi kupanda kuna orodha ya mastaa ambao unapaswa kuwatazama kwenye Afcon 2025, kwa sababu zinaweza kuwa fainali zao spesho kuonyesha mambo matamu uwanjani.

Azzedine Ounahi (kiungo, Morocco)

Azzedine Ounahi kwa sasa anakipiga kwenye kikosi cha Girona ya Hispania baada ya kutumikia msimu uliopita kwa mkopo huko Ugiriki katika timu ya Panathinaikos.

Kutokana na nahodha na mwanasoka bora wa Afrika, Achraf Hakimi kukimbizana na muda kupona majeraha yake, Morocco inahitaji mchezaji mwingine wa kuifanya itambe kwenye ardhi ya nyumbani katika Afcon 2025.

Kiungo mshambuliaji wa Real Madrid, Brahim Diaz, ndiye kinara wao wa mabao, akiwa amefunga mara saba, lakini Azzedine Ounahi, ameonyesha ufundi mwingi sana katika eneo la kiungo la kikosi hicho cha Atlas Lions.

Bila shaka ndiye mchezaji atakayevutia kutazama zaidi katika kikosi cha Morocco. Alikuwa bora pia kwenye Kombe la Dunia 2022.

Morocco imepangwa Kundi A sambamba na Comoros, Mali na Zambia na wengine wanaamini Ounahi atafanya mambo mazuri kwenye sehemu ya kiungo huku wakiwa na kipa mzoefu Yassine Bonou na straika wa mabao Youssef En-Nesyri.

Mohamed Amoura (straika, Algeria)

Straika wa Wolfsburg, Mohamed Amoura aliifungia Algeria mabao 10 wakati taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika likifanikiwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026. Ni kinara wa mabao pia kwa timu za Afrika kwenye kufuzu Kombe la Dunia na hakika mwaka 2025 kwa namna moja au nyingine umekuwa bora kwa Amoura.

Straika huyo anayekitumikia kikosi cha Wolfsburg alifunga mabao 11 katika mechi nane alizochezea nchi yake kuanzia Machi mwaka huu, ikiwamo hat-trick dhidi ya Msumbiji. Kiwango chake bora kimemfanya kuwa chaguo la kwanza kwenye kikosi cha wachezaji 25 cha kocha Les Verts.

Riyad Mahrez bado ni mchezaji muhimu kwa mabingwa hao wa Afcon 2019, lakini kwa sasa ni muda wa Amoura kuonyesha ubora wake kwa Waafrika. Amoura ana kimo cha futi 5 na inchi 7, huko Algeria imepangwa kwenye Kundi E sambamba na Sudan, Burkina Faso na Equatorial Guinea.

Victor Osimhem (straika, Nigeria)

Victor Osimhen aliisaidia Nigeria kufika kwenye mchezo wa mchujo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026, lakini kikosi hicho cha Super Eagles kikipoteza kwa mikwaju ya penalti dhidi ya DR Congo.

Ndiyo hivyo, lakini kwenye kuelekea mashindano ya Afcon 2025, Nigeria imeweka matumaini yake kwa straika Osimhen, ambaye kwa sasa anakipiga Galatasaray.

Super Eagles ilivuna pointi nne tu kati ya 15 katika mechi ilizocheza bila ya huduma ya Osimhen na hivyo iliwagharimu kwa kiasi kikubwa katika harakati zao za kufuzu Kombe la Dunia 2026.

Osimhen ni mchezaji muhimu katika kikosi cha Nigeria chini ya kocha Eric Chelle na timu hiyo ilipoteza mwelekeo kwenye mechi ya mchujo dhidi ya DR Congo baada ya kutolewa wakati wa mapumziko.

Kwa mujibu wa mchezaji mwenzake, Frank Onyeka, Osimhen amekuwa na mchango mkubwa kwenye timu na bila shaka ni mmoja wa watakaovutia wengi kwa wale watakaokipiga kwenye Afcon 2025 huko Morocco.

Nigeria imepangwa Kundi C sambamba na Tanzania, Tunisia na Uganda.

Ibrahim Mbaye (fowadi, Senegal)

Ibrahim Mbaye, 17, alicheza mechi yake ya kwanza kwenye kikosi cha Senegal dhidi ya Brazil mwezi uliopita. Mshambuliaji Sadio Mane anaendelea kubaki kama mchezaji muhimu kwa washindi hao wa Afcon 2021, wakati Iliman Ndiaye na Ismaila Sarr wanaotamba kwenye Ligi Kuu England wakiwa na msaada mkubwa katika fowadi hiyo ya Senegal.

Lakini, dunia ya wapenda soka kwa sasa itakwenda kushuhudia staa mpya wa Simba wa Teranga, Ibrahim Mbaye kwenye mechi za Kundi D la mashindano ya Afcon 2025, ambapo Senegal imepangwa sambamba na Botswana, DR Congo na Benin.

Kinda huyo aliyechezea timu ya taifa ya Ufaransa kwenye ngazi za vijana, amepandishwa kikosi cha kwanza cha Paris Saint-Germain msimu huu, ambapo alianzishwa kwenye mechi ya ushindi dhidi ya Barcelona baada ya kutokea benchini dhidi ya Tottenham.

Mbaye anasubiriwa kwa hamu kuona kile ambacho anaweza kukifanya kwenye Afcon, ambapo aliweka rekodi ya kuifungia Senegal akiwa kijana zaidi, umri wa miaka 17 na siku 298 alipofunga kwenye ushindi wa 8-0 dhidi ya Kenya.

Rogers Mato (winga, Uganda)

Rogers Mato ni miongoni mwa vinara wa mabao kwenye Ligi Kuu North Macedonia msimu huu alikofunga mabao 12.

Na sasa, staa huyo Mato atakuwa kwenye kikosi cha The Cranes ya Uganda kilichorejea kweye mashindano ya Afcon kwa mara ya kwanza tangu 2019, ambapo kilitolewa katika hatua ya 16-Bora na sasa kinachojiandaa kwa Afcon 2027, ambapo Uganda itakuwa kati ya timu mwenyeji sambamba na Tanzania na Kenya.

Kikosi hicho cha kocha Paul Put kilimaliza katika nafasi ya pili kwenye mechi za kufuzu Kombe la Dunia kwenye kundi lao, nyuma ya Algeria, ambapo Rogers Mato alifunga mabao matatu.

Winga huyo mwenye umri wa miaka 22 alifunga mara mbili kwenye ushindi dhidi ya Msumbiji, Septemba na amekuwa kwenye kiwango bora sana akiichezea Vardar ya ligi ya North Macedonia.

Uganda imepangwa kwenye kundi linalohitaji ujanja mwingi sana kwenye Kundi C pamoja na Tanzania na mabingwa wawili wa zamani wa Afcon, Nigeria na Tunisia.

Reinildo (beki, Msumbiji)

Reinildo amekuwa mchezaji wa kwanza wa Msumbiji kucheza kwenye Ligi Kuu England wakati alipochezea Sunderland, Agosti 16. Msumbiji itakwenda kwenye fainali za Afcon 2025 ikiwa na kumbukumbu ya kwamba haijawahi kufika kwenye hatua ya mtoano mara zote tano ilizowahi kucheza Afcon.

Lakini, kwa mara ya kwanza, Msumbiji itakwenda kwenye mashindano ya Afcon ikiwa na mchezaji wa Ligi Kuu England, Reinildo baada ya kujiunga na Sunderland akitokea Atletico Madrid kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Akicheza kwenye beki ya kushoto, Reinildo, 31, amesaidia Sunderland iliyorejea kwenye Ligi Kuu England msimu huu, kuonyesha kiwango bora kabisa na hivyo kuwa macho ya wengi kwenye kikosi cha Msumbiji, akiwekwa kundi moja na kinara wa mabao wa nchi hiyo, Tico Tico.

Msumbiji imepangwa kwenye Kundi F sambamba na timu ngumu sana ikiwamo Ivory Coast, Cameroon na Gabon.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *