Brazil. Kutana na Rebeca Tavares (31), mwanasoka wa zamani ambaye pia ni mke na mama watoto wa kiungo mkabaji wa Al-Ittihad, Fabinho (32), kutokea Brazil, nchi kubwa zaidi Amerika Kusini.

Rebeca alifikia uamuzi wa kustaafu soka mwaka 2018 ili kumuunga mkono mume wake ikiwa ni miaka sita tangu kuanza kwa uhusiano wao uliogeuka hamasa ya kweli katika kusaka mafanikio.

Rebeca aligeuka kuwa shabiki mkubwa wa Liverpool, klabu aliyoichezea Fabinho kwa miaka mitano na kushinda mataji mengi likiwemo la Ligi Kuu England (EPL).

Ikumbukwe Fabinho alitua Anfield Mei 2018 kwa dau la Pauni 39.3 milioni akitokea AS Monaco na alishinda ubingwa wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) 2016/17.

Ukitazama ukarasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya 145,000, utaona Rebaca ni mwanamke mrembo anayependa kuishi maisha ya kifahari lakini usidanganyike mguuni vitu vimo.

Rebeca alizaliwa Brazil mnamo Desemba 2, 1994, na kuhamia Hispania akiwa na umri wa miaka sita na alikulia huko na hata kujifunza kucheza soka ikiwa ni ndoto yake.

“Familia yangu ni familia ya Kibrazili kabisa, namaanisha nyumbani tulikuwa tukitazama soka kila wakati, hivyo nilipenda soka tangu nikiwa mtoto,” Rebeca aliuambia mtandao wa Her Football Hub.

“Nakumbuka tukio moja hasa lililonifanya nianze kutazama na kucheza soka. Ni pale Ronaldinho alipoanza kucheza Ulaya. Kusema kweli mtindo wake ulinitia moyo sana kucheza mpira,” alieleza.

Utakumbuka Ronaldinho Gaucho alianza kucheza Ulaya mwaka 2001 akiwa na kikosi cha Paris Saint-Germain (PSG), kisha Barcelona na AC Milan na aliondoka 2011 na kurejea kwao Brazil.

Licha ya mapenzi yake katika mchezo huo, Rebeca anakiri mara nyingi aliwahi kuambiwa  ‘soka si kwa ajili ya wanawake’ lakini wakati huu anafurahia kuona mambo yamebadilika sana.

“Kwa sasa msichana mdogo akisema anataka kuwa mchezaji wa soka, watu wanamuunga mkono zaidi kuliko zamani na hiyo ni hatua kubwa imepigwa,” alisema Rebeca.

“Nadhani timu imara zaidi za Ulaya zipo Ufaransa. Hata hivyo, wanawake Hispania na England wanazidi kujiingiza kwenye soka, jambo ambalo ni zuri kwa maendeleo ya mchezo,” alieleza.

Baada ya kuishi kwa miaka mingi Hispania na kujifua vilivyo, Rebeca alihamia AS Monaco FF hapo Januari 2018, huku mumewe akiwa anaichezea klabu hiyo upande wa wanaume.

Hata hivyo, Rebeca alikaa miezi michache tu na timu hiyo ya Ufaransa kabla ya Fabinho kufanya uhamisho wa fedha nyingi kwenda Liverpool, kitu kilichomfurahisha sana mrembo huyo.

Na wakati huo ndipo Rebeca aliacha kucheza soka ili kumsapoti mumewe huku akidai ndoto zake za kucheza soka la kulipwa zinaendelea kutimia kupitia Fabinho, mwanafainali wa Copa America 2021.

“Kwangu mimi kumtazama Fabs akicheza katika kiwango hiki, ni kama ndoto yangu imetimia lakini kupitia miguu yake,” aliandika Rebeca kupitia X, zamani Twitter wakati akimjibu shabiki aliyemuomba kuendelea kucheza.

Alipoulizwa kama angependa kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa, alijibu; “Ni ngumu kusema, lakini nafikiri kwa sasa kulingana na nafasi yangu (familia), nitapata ugumu kujitoa kikamilifu uwanjani.”

“Sasa ni wakati wa wasichana wadogo kuendeleza urithi, kufanikisha makubwa na kukuza soka la wanawake. Kwa wanawake, soka linapaswa kuwa zaidi ya ‘mchezo wa wanaume’” alieleza.

Hivyo ndivyo Rebeca alivyochagua kuwa mama wa familia na kwa wakati huu anawalea watoto wake wawili, Israel (2022) na Alicia (2024).

Kwa sasa akiwa anaishi Jeddah, mara kwa mara Rebeca ameonekana uwanjani akimshabikia Fabinho katika mechi za Saudi Pro League, ingawa mwanzo alionyesha bado angetamani kuendelea kuishi Uingereza.

“Nahisi mapigo ya moyo wangu yanaenda kasi sana… Sikuwa tayari kuaga (na bado siko tayari) lakini haya ndiyo maisha, ndivyo soka lilivyo,” alisema Rebeca wakati huo akiwaaga mashabiki wa Liverpool.

Alikuwa na marafiki wengi huko kwani Fabinho akiwa Uingereza alijulikana kutumia muda wake na wachezaji wenzake kutokea Brazil kama Becker, Firmino, Ederson, Fred na Fernandinho pamoja na familia zao.

Mathalani kuna picha nyingi za Rebeca akiwa na wenza wa Becker na Firmino walizopiga katika uwanja wa Anfield na Fabinho alikipiga pamoja na wachezaji hao wakiitumikia Liverpool.

Baada ya hapo, Fabinho na Firmino walihamia Jeddah, Saudi Arabia. Ederson na Fred wakahamia Istanbul, Uturuki, huku Fernandinho akirejea Brazil.

Ikumbukwe uhusiano wa Fabinho na Rebeca ulianza mwaka 2013, kisha wakafunga ndoa 2015 ingawa vyanzo vingi vya habari na machapisho mbalilimbali katika mitandao ya kijamii hayajataja tarehe kamili. 

Rebeca anatumia jina la ukoo wa Fabinho ambao ni Tavares, ikiwa ni tofauti na baadhi ya wake na wapenzi wa wachezaji maarufu (WAGs) ambao huendelea kutumia majina ya familia zao hata wakiolewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *