
Mahakama ya Kazi ya Paris leo Jumanne, Desemba 16, imeamuru Paris Saint-Germain, kumlipa takriban euro milioni 61 mchezaji wake wa zamani Kylian Mbappé katika mzozo kati ya pande hizo mbili tangu mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa aondoke kwenda Real Madrid katika msimu wa joto wa mwaka 2024.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Paris Saint-Germain siku ya Jumanne, imeamriwa na mahakama ya Kazi ya Paris kumlipa Kylian Mbappé karibu euro milioni 61 kwa marupurupu na mishahara ambayo haijalipwa tangu mwisho wa mkataba wake mwaka wa 2024. Hata hivyo, mahakama hiyo, iliyojumuisha wawakilishi wawili wa waajiri na wawakilishi wawili wa wafanyakazi, imekataa kuainishwa upya kwa mikataba yake ya muda maalum kama mkataba wa kudumu (CDI).
Mawakili wa Mbappé walikuwa wametegemea ombi hili la kuainishwa upya, hasa kudai euro milioni 263, hoja ambayo imekataliwa. Hata hivyo, PSG italazimika kuwajulisha mashabiki wake kuhusu uamuzi huo kwenye ukurasa wa mbele wa tovuti yake kwa mwezi mmoja.
Madai ya PSG yakataliwa
Kwa upande wao, madai ya PSG, yakifikia euro milioni 440 , kwa uharibifu wa taswira yake, kupoteza fursa ya kumhamisha mchezaji huyo, na nia mbaya katika utekelezaji wa makubaliano ya mwezi Agosti 2023 (yaliyolenga kuongeza mkataba wake), yamekataliwa kwa ukamilifu. Walipoulizwa kuhusu rufaa inayowezekana, mawakili wa PSG wamekataa kutoa maoni katika hatua hii.
Kwa upande mwingine, “wanasheria wa Bw. Kylian Mbappé wanakubali kwa kuridhika uamuzi uliotolewa leo na Mahakama ya Kazi,” wamesema katika taarifa kwa vyombo vya habari. “Uamuzi huu unathibitisha kwamba ahadi zilizotolewa lazima ziheshimiwe.” Inaonyesha ukweli rahisi: hata katika tasnia ya mpira wa miguu, sheria ya kazi inatumika kwa kila mtu.
Hapo awali, Kylian Mbappé ndiye ambaye, baada ya kutafuta bila mafanikio euro milioni 55 kama mishahara na marupurupu kutoka kwa mamlaka ya michezo mwishoni mwa mkataba wake katika msimu wa joto wa mwaka 2024, aliipeleka PSG kwenye Mahakama ya Kazi.