j

Chanzo cha picha, PA Media

“Tutapinga kesi hii,” BBC inasema baada ya kesi ya dola bilioni 5 (pauni bilioni 3.7) kufunguliwa, kufuatia kuhaririwa kimakosa hotuba ya Donald Trump ya Januari 6, 2021 katika makala ya Panorama.

Wengi, ndani na nje ya BBC, wameniambia BBC inapaswa kupambana. Lazima itetee uandishi wake wa habari dhidi ya rais mbishi ambaye, baadhi ya watu wanadai, amekuwa akitumia hatua za kisheria dhidi ya makampuni ya vyombo vya habari vya Marekani.

Kwa hivyo jambo la muhimu – ni kumkabili Trump na kuonyesha ulimwengu kwamba haimwogopi rais na vitisho vyake vya mabilioni ya dola.

Pia unaweza kusoma

Mambo Mawili

Kesi ya Trump ina mambo mawili makuu – hadhira na nia mbaya.

Amefungua kesi Florida na anapaswa kuuthibitishia umma kwamba hadhira katika jimbo hilo imeiona makala ya kipindi cha Panorama, ili kuthibitisha kwamba makala hiyo imemchafua.

Madai katika jalada lake ni kwamba watazamaji walitazama kupitia VPN. Hata kama hiyo ni sahihi: Je, kuna idadi kubwa ya watu walitazama na kumsababishia uharibifu wa sifa yake? Je, BBC inaweza kuwajibika kwa matendo haramu ya watumiaji wa mtandao katika huduma zake?

Madai kuhusu kampuni ya Canada inayoitwa Blue Ant Media inayosambaza makala hiyo nchini Marekani yangekuwa na matatizo zaidi kwa BBC ikiwa ni kweli.

Kampuni hiyo imethibitisha kuwa ina haki ya kusambaza kipindi hicho lakini “hakuna hata mmoja wa wanunuzi wa Blue Ant aliyekirusha hewani nchini Marekani,” msemaji alisema.

Aliongeza kuwa toleo la kimataifa la kipindi cha Panorama halikuwa na kipande kinachozozaniwa katika hotuba ya Trump, kwani kipande hicho kilipunguzwa.

Ikiwa hiyo ni sahihi, hilo linaacha swali la kama hadhira ilitazama makala hiyo kupitia Britbox, kama inavyodaiwa. Bado hatujasikia majibu kutoka Britbox kuhusu jambo hilo.

BBC inasisitiza kwamba kipindi hicho hakikutangazwa Marekani.

Kesi ya rais pia inategemea madai ya nia mbaya: kwamba BBC ilikusudia kumchafua. Anadai ilichapisha makala hiyo wiki moja kabla ya uchaguzi kwa “nia ya wazi ya kuingilia kati na kujaribu kudhoofisha uwezekano wa Rais Trump kushinda uchaguzi tena.”

Sehemu ya hotuba hiyo inayozozaniwa ni sekunde 12, katika kipindi cha dakika 57. BBC inakubali kwamba marekebisho hayo yalikuwa kosa lisilo la kukusudia. Taarifa ya rais Trump inasema shirika hilo lisingeunganisha sehemu mbili za hotuba yake isipokuwa ilikusudia kufanya hivyo.

Pia anategemea mifano mingine anayodai inaonyesha BBC ina historia ya kuripoti habari zake kwa njia hasi. Jalada hilo linasema “BBC haikujali ukweli kuhusu Rais Trump” na hufanya juhudi “za kutengeneza simulizi hasi za upande mmoja dhidi ya Trump.”

BBC inakataa hili.

Changamoto kwa BBC

Ni wazi kwamba upande mmoja mbaya katika kesi hii itakuwa ni gharama kubwa ya pesa. Chris Ruddy, rafiki na mshirika wa Trump na mtendaji mkuu wa mtandao wa habari wa Marekani Newsmax, amekiambia kipindi cha BBC Radio 4 cha Today kwamba kwenda mahakamani kutagharimu dola milioni 50-100, ilhali anadai BBC inaweza kukubali fidia ya dola milioni 10.

Pendekezo lolote la kutumia fedha kutoka kwa walipa leseni kumlipa Trump kama sehemu ya suluhu litakuwa jambo gumu kwa shirika hilo. Vile vile, kutumia mamilioni ya pesa kupinga kesi mahakamani kutafanya BBC isutwe kwamba imepoteza fedha nyingi.

BBC ina bima – lakini hatujui inagharamia nini. Je, ni gharama za kisheria au gharama za suluhu pekee. Je, bima hiyo ina kiwango fulani ya ukomo?

Jambo lingine baya ni jinsi kesi hiyo itakavyo athiri BBC wakati watendaji wake wakuu watakapo fanya mazungumzo na serikali kuhusu Mkataba ujao wa BBC, ambao utaanza kazi mwishoni mwa 2027.

Huku mkurugenzi mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa habari wakiwa wamejiuzulu, badala ya kupigania mustakabali wa BBC na mfumo wake wa ufadhili, inalazimika kuingia katika vita vigumu vya kisheria katika historia ya shirika hilo. Inaweza kujaribu kufanya yote mawili – Je, itaweza kuyafanya yote mawili vizuri?

Hoja kuhusu “sheria,” kama inavyosemwa na wengi, sio kuhusu matokeo bali ni kuhusu gharama inayohitajika wakati wa kupinga kesi.

Hakuna sababu ya Trump kurudi nyuma na BBC tayari imekiri kwamba ilifanya kosa. Anaonekana kutaka kuonyesha kwamba kuna upendeleo.

Trump na vyombo vya habari

M

Chanzo cha picha, Getty Images

Ukiangalia baadhi ya kesi za nyuma za Trump – baadhi ya makampuni ya vyombo vya habari yalikubali kusuluhisha (ikiwa ni pamoja na ABC kwa dola milioni 15 na Paramount/CBS kwa dola milioni 16), hata wakati wachambuzi wa sheria waliposema wangeweza kushinda kesi zao.

Vita vingine vya Trump, ni pamoja na Wall Street Journal (WSJ) ambayo inakabiliwa na kesi ya dola bilioni 10 kuhusu habari juu ya Trump na barua ambayo iliripoti kwamba alimwandikia Jeffrey Epstein. WSJ inasema ripoti yake ni sahihi.

Gazeti la New York Times linakabiliwa na kesi ya dola bilioni 15 kutokana na madai ya rais kwamba lilitaka kudhoofisha ugombeaji wake 2024 na kuharibu sifa yake kama mfanyabiashara.

Gazeti hilo pia linapinga hilo – na linaelezea kinachoendelea ni sehemu ya shambulio kubwa la kimataifa dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari.

Serikali inaweza kuingilia?

Je, BBC ina chaguzi zingine? Mfano, BBC kumwomba waziri mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer kuingilia kati na kumpigia simu Trump na kumwomba asamehe?

Tunajua serikali hii ya Labour inaunga mkono BBC. Licha ya mfululizo wa utata na makosa ikiwa ni pamoja na makala mbili za Israeli/Gaza kupitia Panorama.

Waziri wa utamaduni siku ya Jumanne, alisifu shirika hilo kama muhimu kwa afya ya demokrasia na mwangaza katika nyakati za giza.

Lakini katika mkutano huko Downing Street, msemaji wa Waziri Mkuu hakugusia wazo kwamba bosi wake atatumia nguvu yoyote aliyokuwa nayo kumshawishi Trump arudi nyuma kuhusu kesi ya BBC.

Hatua inayofuata ni kwa BBC kujibu kesi hiyo – lakini ikiwa haitajibu, mawakili wa Trump wanaweza kuiomba mahakama kutoa uamuzi bila BBC kuwepo.

Hakuna jambo la uhakika katika kesi hii. Lakini hizi ni nyakati hatari na, chochote itakachosema hadharani, BBC itakuwa ikizingatia hatua zake zinazofuata kwa tahadhari kubwa.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *