
Kupitia mahojiano yaliyochapishwa siku ya Jumanne (Disemba 16), mshirika huyo muhimu wa Rais Vladimir Putin wa Urusi amemsifia na kumuunga mkono Rais Donald Trump wa Marekani, akidai kuwa lau angelikuwapo tangu awali, vita hivyo kamwe visingetokea.
Lukashenko, ambaye aliruhusu nchi yake kutumiwa na Urusi kuivamia Ukraine mwaka 2022, amesema Trump ndiye anayetegemewa sasa kusitisha vita hivyo, na kwamba anahitaji kutiwa moyo.
Kauli ya Lukashenko imetolewa ikiwa ni siku moja tu baada ya mkutano wa pande tatu uliofanyika mjini Berlin, Ujerumani, ambapo wawakilishi wa Marekani, Ulaya na Ukraine walisema wamepiga hatua kubwa kuelekea makubaliano ya kukomesha vita hivyo kupitia mpango wa amani uliopendekezwa na Trump.