
Washington imepaza sauti yake, ikisema kwamba utekelezaji wa makubaliano ya biashara yaliyofikiwa na London hauendelei haraka vya kutosha.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Uhusiano maalum” kati ya London na Washington umeingiliwa na sintofahamu. Marekani imesitisha ushirikiano wa teknolojia na Uingereza kwa misingi kwamba utekelezaji wa makubaliano ya biashara yaliyofikiwa kati ya nchi hizo mbili hauendelei haraka vya kutosha, mshauri wa sayansi na teknolojia wa Ikulu ya White House Michael Kratsios ametangaza siku ya Jumanne. Ushirikiano huu unashughulikia teknolojia kadhaa za kisasa, ikiwa ni pamoja na akili bandia (AI) na nguvu ya nyuklia ya raia.
Kutangazwa kwa makubaliano kati ya Marekani na Uingereza mapema mwezi Mei kulisababisha msukosuko, kwani haya yalikuwa makubaliano ya kwanza ya biashara yaliyohitimishwa na utawala wa Trump baada ya kutoza ushuru mapema mwezi Aprili. “Tunatumai kuendelea na kazi yetu na Uingereza mara tu watakapopiga hatua kubwa katika kutekeleza ahadi zao” kuhusiana na makubaliano ya biashara, Michael Kratsios ameandika kwenye mtandao wa kijamii X.
Kulingana na vyombo kadhaa vya habari, majadiliano bado yamekwama kuhusu masuala kadhaa, ikiwa ni pamoja na usalama wa chakula na udhibiti wa mtandao. Marekani ingependa hasa kufungua soko la Uingereza zaidi kwa mauzo yake ya nje ya kilimo. Chini ya makubaliano hayo, serikali ya Marekani imepunguza ushuru wake hadi 10% kwa bidhaa nyingi zinazosafirishwa na Uingereza kwenda Marekani.