
Misemo hii inaakisi kwa kina yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, pamoja na hatua zilizochukuliwa baadaye ikiwemo kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi.
Matukio ya Oktoba 29 hayakuwa chanzo cha matatizo, bali yalikuwa ni matokeo. Chanzo chake kilikuwepo muda mrefu kabla na kwa kiasi fulani bado kinaendelea kuwepo.
Tangu maandalizi ya uchaguzi yalipoanza, hoja mbalimbali ziliibuliwa na wadau tofauti wakiwamo wanasiasa, vyama vya siasa, asasi za kiraia, taasisi za dini na wananchi kwa ujumla wakishauri nini kifanyike ili uchaguzi uwe huru, wa haki na wa amani.
Hata hivyo, maoni hayo yalipuuzwa na wenye mamlaka ya uamuzi. Kwa mtindo wa ‘mdharau mwiba,’ taifa likajikuta ‘mguu umeota tende,’ na sasa nguvu kubwa inatumika kutafuta tiba badala ya kinga.
Kwa muda mrefu, wadau wengi wakiwamo waandishi na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, wamekuwa wakionya kuhusu nyufa katika demokrasia yetu na kusisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari mapema.
Nadhani huenda ushauri huo haukutiliwa maanani sana. Matokeo yake, ufa uliangusha ulitikisa pa kubwa kwenye ukuta wa amani na kinachoshuhudiwa sasa ni juhudi za kuujenga upya. Gharama za kudhibiti ghasia za uchaguzi, gharama zilizolipwa kwa damu ya Watanzania na uharibifu wa mali ni kubwa mno ukilinganisha na gharama ambazo zingetumika kuzuia maandamano na migogoro hiyo mapema.
Serikali ni yetu sote. Kauli ya “mchelea mwana kulia, hulia yeye” inapata maana yake hapa. Kwa nia ya kulinda na kuvumilia, taifa limejikuta likibeba maumivu makubwa zaidi.
Hata hivyo, pongezi zinastahili kutolewa kwa Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuimarisha hali ya usalama, hatua iliyosaidia kudhibiti maandamano ya vurugu zaidi, ikiwemo yale yaliyopangwa kufanyika Desemba 9, mwaka huu.
Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa kutokuwepo kwa maandamano hakumaanishi kutoweka kwa malalamiko. Dukuduku za vijana, hususan kizazi cha Gen Z, bado zipo.
Ni hatari kwa mamlaka kujisifu kudhibiti maandamano bila kushughulikia mizizi ya malalamiko. Pale panapofuka moshi, chini kuna moto.
Kunyamaza kwa waliokerwa si dalili ya amani ya kudumu, bali ni ishara ya msukumo unaohitaji kusikilizwa. Ndiyo maana wito unatolewa kwa Watanzania wote kutoa ushirikiano kwa Tume ya Uchunguzi ili ukweli ubainike na suluhu zipatikane.
Baada ya uchaguzi, ghasia na uvunjifu wa amani viliripotiwa katika miji kadhaa ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Songwe, Mara na Geita na kusababisha vifo, majeruhi, uporaji na uharibifu wa mali na miundombinu.
Kutokana na hali hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan, Novemba 20, 2025 aliunda Tume Huru ya Kuchunguza Matukio ya Ghasia chini ya Sheria ya Tume za Uchunguzi.
Lengo la Tume ni kuchunguza chanzo cha ghasia, wahusika, madhara yaliyotokea na hatua zilizochukuliwa katika kudhibiti hali hiyo, pamoja na kupendekeza maboresho ya mfumo wa uwajibikaji, utawala wa sheria, haki za binadamu na majadiliano ya kitaifa. Tume ina mamlaka ya kuwaita au kuwaalika wadau wote wenye taarifa muhimu.
Hivyo, ni wajibu wa wananchi wa kawaida, wanasiasa, waathirika, vyombo vya habari, viongozi wa dini, wafanyabiashara, vijana na watu wa makundi yote kujitoa kutoa ushahidi na maoni yao. Ingawa Tume imepewa siku 90 kukamilisha kazi yake, muda huo hupita haraka. Ushiriki wa mapema na wa dhati ndio kinga bora dhidi ya migogoro ya baadaye.
Na pia itasaidia kuirahisishia Tume hiyo kuchakata mapema kazi yake na kuja na majibu. Shime tujitokeze, tuache kulalamikia pembeni, bali tukazungumze mbele ya Tume kwa mdomo, maandishi na ushahidi mbalimbali utakaokuwapo, kupitia njia walizoelekeza kuufikisha ushahidi huo.
Mungu Ibariki Tanzania.