Siku ya Jumanne utawala wa Rais Donald Trump ulitanua orodha ya nchi  ambayo raia wake wamewekewa masharti makali. Nchi 20 ikiwemo Mamlaka ya Palestina zimeongezwa kwenye orodha ya awali iliyotolewa mwezi Juni.

Watu kutoka mataifa matano pamoja na Palestina wamepigwa marufuku kabisa kuingia Marekani. Kulingana na mamlaka za Marekani wanazingatia zaidi usalama wa raia wake. Lakini watu ambao tayari wana visa za kuingia Marekani au kutambuliwa kuwa wakaazi halali walioko katika nchi hiyo hawatazuiwa kuingia Marekani. Aidha, wanadiplomasia na wanamichezo hawajazuiliwa ilimradi wana nyaraka sahihi.

Mwezi Juni marufuku ya kuingia Marekani ilitolewa kwa raia wa Afghanistan, Myanmar, Chad, Jamhuri ya Congo, Equatorial Guinea, Eritrea, Haiti, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen. Masharti makali yaliwekewa raia kutoka Burundi, Cuba, Laos, Sierra Leone, Togo, Turkmenistan na Venezuela.

Wanawake wakitembea barabarani katika kitongoji chenye wasomali wengi cha Cedar-Riverside huko Minneapolis mnamo Mei 12, 2022
Watu kutoka mataifa matano pamoja na Palestina wamepigwa marufuku kabisa kuingia MarekaniPicha: Jessie Wardarski/AP Photo/picture alliance

Siku ya Jumanne utawala wa Trump ulitangaza kuwapiga marufuku raia wa Burkina Faso, Mali, Niger, Sudan Kusini na Syria. Raia kutoka mataifa 15 wamewekewa masharti mepesi. Hao ni kutoka nchi za Angola, Antigua na Barbuda, Benin, Ivory Coast, Jamhuri ya Dominika, Gabon, Gambia, Malawi, Mauritania, Nigeria, Senegal, Tanzania, Tonga, Zambia and Zimbabwe. Masharti hayo yatawahusu wale wanaokwenda Marekani kama wageni wa muda na pia wale wanaotaka kuhamia kwenye nchi hiyo. 

Katika tangazo lake Marekani imesema maamuzi yake yanaongozwa na visa vya mataifa hayo kuhusika katika ufisadi wa kupindukia, utumiaji wa hati za raia zisizo sahihi na pia takwimu za uhalifu. Hayo yote husababisha taratibu za kuwachuja raia wa nchi hizo kuwa changamoto.

Kisa cha raia wa Afghanistan ambaye alifanya mashabulizi dhidi ya walinzi wa Ikulu ya Marekani, White House ndicho kinaonekana kusababisha Marekani kubana uhamiaji wa raia wa kigeni. Lakini kulingana na wale wanaopinga hatua hiyo ya Marekani, utawala unatumia visingizio hivyo kuwakosesha fursa watu kutoka mataifa mengine.

Vyanzo – Mashirika

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *