Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema kuwa mapendekezo yanayosimamiwa na Marekani kwa ajili ya kupatikana mkataba wa kukomesha vita yanaweza kukamilishwa ndani ya siku chache zijazo na kisha wajumbe wa Washington watayafikisha Kremlin, kabla ya mkutano mwengine unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki ijayo nchini Marekani.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema chini ya hakikisho la usalama lililotolewa na Marekani kwa Ukraine baada ya kumalizika kwa vita, vikosi vya kulinda amani vya Ulaya vitaweza katika hali fulani kuwarejesha nyuma wanajeshi wa Urusi.

Berlin | Kansela Friedrich Merz akizungumza katika mkutano kuhusu Ukraine
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alipoongoza mkutano kuhusu Ukraine mjini BerlinPicha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Akihojiwa na televisheni ya umma nchini Ujerumani ya ZDF, Kansela Merz amesema hilo linawezekana, lakini matarajio hayo si ya kutegemewa mno kwa sasa na kwamba suala la kuvirejesha nyuma vikosi vya Urusi kwa mujibu wa hakikisho hilo la usalama, litafanyika ikiwa tu majeshi ya Moscow yatakiuka masharti ya makubaliano yatakayosainiwa ya  kusitisha mapigano nchini Ukraine.

Hata hivyo, Urusi bado haijaafiki suala la usitishaji mapigano ambalo Marekani na nchi za Ulaya zinalitaja kuwa nguzo ya makubaliano yoyote na vile vile Moscow inatupilia mbali wazo la uwepo wa wanajeshi wa Magharibi katika ardhi ya Ukraine ili kusaidia kuvimaliza vita hivyo. Siku ya Jumanne, Msemaji wa Ikulu ya Urusi, Kremlin Dmitry Peskov alitupilia mbali wito wa Kansela Merz wa kutaka usitishwaji mapigano katika msimu wa sikukuu ya Krismasi.

“Ikiwa Ukraine inalenga kubadili masuluhisho ya kudumu na yale yasiyo endelevu, hapana shaka sisi hatuko tayari kushiriki kwenye hayo. Tunataka amani, hatutaki makubaliano yatakayoipa Ukraine ahuweni na muda wa kujiandaa ili kuendeleza vita. Tunataka kukomesha vita hivi, kufikia malengo yetu, kulinda maslahi yetu, na kuhakikisha amani ya Ulaya kwa siku zijazo,” alisema Peskov.

Kamisheni ya kuifidia Ukraine yazinduliwa

Berlin I Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiwa na viongozi kadhaa wa Ulaya
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiwa na viongozi kadhaa wa Ulaya katika mkutano wa mjini Berlin, UjerumaniPicha: Tobias Schwarz/AFP

Umoja wa Ulaya umeanzisha Kamisheni ya Kimataifa ya Madai ya Ukraine katika juhudi za kuhakikisha kuwa Kiev inafidiwa kwa mabilioni ya dola kufuatia madhara iliyoyapata kutokana na mashambulizi ya Urusi na uhalifu wa kivita dhidi yake. Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, amesema uanzishwaji wa Kamisheni hiyo unalenga kuhakikisha kuwa  Ukraine haitaachwa katika hali ya sasa.

“Pamoja na kupatikana haki kutokana na uvunjwaji mkubwa wa sheria za kimataifa, fidia ni muhimu sana kwa ajili ya uwajibikaji. Na ikiwa kweli tunaamini kwenye amani ya haki na ya uhakika nchini Ukraine na usalama barani Ulaya, lazima tuendelee kupigania uwajibikaji,” alisisitiza Kallas.

Viongozi 34 wa  Umoja wa Ulaya  walikutana mjini The Hague, Uholanzi, hapo jana kutia saini uzinduzi wa Kamisheni hiyo ya kuifidia Ukraine uliohudhuriwa pia na Rais Zelensky. Hata hivyo, suala tete ni wapi pesa hizo zitapatikana maana hadi sasa nchi za Ulaya hazijaafikiana kuhusu kutumia mabilioni ya dola ya mali za Urusi zilizozuiwa, na viongozi wa Ulaya wanatarajiwa kukutana siku ya Alhamisi mjini Brussels kuendelea kulijadili hilo.

(Vyanzo: Mashirika)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *